Meneja wa mkoa wa Dawasco -Tegeta Alpha Ambokile akizungumza na wakazi wa mtaa wa Upendo Salasala jijini Dar es Salaam ambao wameanza kupata huduma ya maji safi katika maeneo yao.
Bomba likitoa maji katika moja ya mitaa ya Salasala jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wakazi wa Salasala wakimsikiliza Meneja wa Dawasco-Tegeta Alpha Ambokile (hayupo pichani)
Hivi ndivyo hali ilivyokuwa kabla ya kuanza kupatikana kwa huduma ya maji katika eneo la Salasala ambapo kwa sasa wakazi wa eneo hilo wanapata huduma ya maji.
Na Dixon Busagaga wa Michuzi blog.
WANANCHI zaidi ya 265 wa mtaa wa Upendo, Mbezi Salasala wilayani Kinondoni
wamelishukuru Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASCO), kwa
kuwafikishia huduma ya Majisafi waliyoipatia shida kwa zaidi ya miaka 10
iliyopita.
Akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja wa serikali za mitaa na DAWASCO,
Mjumbe wa mtaa wa Upendo Bw. Robert Massawe amepongeza juhudi zilizofanywa na
Dawasco za kuwapatia huduma ya Maji wananchi wa
eneo lake na kwamba juhudi hizo zinaendana na kauli ya serikali ya awamu ya
tano inayosema hapa kazi tu.
Akieleza historia fupi ya eneo hilo Bw. Massawe alisema tangu watu waanze
kuhamia eneo hilo huduma ya Maji ilikuwa ni ya kununua kutoka mtaa mwingine wa
mbali ambao ulikuwa umefikiwa na huduma hiyo ya Maji.
“Ilifikia kipindi gharama ya kununua Maji ni kubwa kuliko gharama ya
chakula, na wananchi wengi walikuwa wakitumia muda wao mwingi kuhangaika
kutafuta Maji jambo ambalo lilikuwa likikwamisha kutekeleza majukumu mengine ya
kujenga nchi” alisema Massawe.
Nae mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Bi. Sofia alisema; “Kweli DAWASCO imemtua
mama ndoo ya Maji kichwani, sisi akina mama ndio tuliokuwa tukiteseka zaidi na
suala la Maji, lakini akina mama wa mtaa huu tulijitoa ili kupambana na janga
la Maji ambalo lilikuwa likitukabili, na hatimaye tumefanikiwa kupata huduma ya
Maji”
Kwa upande wa Dawasco, Meneja wa Mkoa wa Tegeta, Bw. Alpha Ambokile
amewataka wakazi wa mtaa huo kujitokeza kwa wingi kufanya maombi ya kuungiwa
huduma ya Maji kwa kuwa tayari huduma hiyo imefika katika makazi yao, baada ya
kuhangaika kwa muda mrefu wakisaka huduma hiyo, na ameahidi kuwaunganishia
huduma Maji mapema na kwa uharaka zaidi, mara tu baada ya kupokea maombi yao ya
kuungiwa huduma.
“Ninawaomba mjitokeze kwa wingi ili kwa pamoja tuweze kuwaunganishia huduma
ya Maji, nitawatengea siku yenu maalum ambayo timu yangu ya ufundi itakuja
kuwafanyia maunganisho ya Maji, ambao bado hamjafanya maombi, fanyeni haraka
ili tuweze kuwaunganishia wote kwa pamoja huduma ya Maji” alisema Ambokile
PICHANI: Sehemu ya wakazi wa mtaa wa Upendo, Mbezi salasala wakiwa na Mjumbe
wa mtaa huo, Bw. Robert Massawe (aliyevaa shati ya bluu), wakisikiliza kwa
makini katika kikao cha pamoja na uongozi wa Shirika la Maji safi na Majitaka
Dar es salaam (DAWASCO) kutoka mkoa wa Tegeta, baada ya mtaa huo kufikiwa na
huduma ya Majisafi na salama kwa mara ya kwanza tangu waanze kuhamia katika
makazi hayo, jijini Dar es salaam.
0 comments:
Post a Comment