WATU
watatu wamekufa papo hapo na wengine wanane kujeruhiwa baada ya basi
lenye namba za usajili T 402 CRY aina ya Scania mali ya Kampuni ya Kisbo
– Safari kupinduka mkoani Morogoro. Basi hilo lilikuwa likitoka mkoani
Tabora kwenda Dar es Salaam.
Imeelezwa
kuwa basi hilo lilipinduka wakati likijaribu kukwepa gari lingine eneo
la Kwambe, wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro kwenye barabara kuu ya
Dodoma – Morogoro.
Kaimu
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonce Rwegasira alisema kuwa
tukio hilo lilitokea majira ya saa 12: 30 jioni, juzi, mwaka huu eneo la
Kwambe, kata ya Dumila, tarafa ya Magole wilayani Kilosa mkoani
Morogoro kwenye barabara kuu ya Dodoma- Morogoro.
Alisema
basi hilo likiendeshwa na Davis Samora (38) mkazi wa Dar es Salaam
liliacha njia na kupinduka wakati likijaribu kukwepa gari lenye namba za
usajili T957 BUV aina ya Scania lenye trela namba T 919 BVA
likiendeshwa na dereva asiyefahamika akitokea Morogoro kwenda Dodoma na
ambaye alikimbia baada ya ajali kutokea.
Kwa
mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, dereva huyo
alijaribu kuyapita magari matatu mbele yake bila tahadhari na
kusababisha ajali hiyo.
Kaimu
huyo alitaja majina ya waliokufa kuwa ni Francis Shija (70) mkazi wa
Nzega, mkoa wa Tabora, mwanamke mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa
miaka 45 hadi 50 ambaye hajatambulia jina , pamoja na mtoto mdogo wa
kiume ambaye bado hajatambuliwa kwa jina na umri wake ni kati ya miaka
mitatu hadi minne.
Aliwataja
majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro ni
Kinazi Machum (38), ambaye ni Mhandisi na Mkazi wa Tabora, Mathei
Fidelis (30), mkazi wa Singida na Baraka Ruta (4) mkazi wa Mwanza.
Wengine
ni Juma Bilal (30) mkazi wa Nzega, Ebebeza Richard (22) mkazi wa Mbeya,
Hamis Mogela (30) mkazi wa Nzega, Pili Waziri (44) mkazi wa Tabora na
Prisca Shija (30) mkazi wa Nzega na wote wanaendelea vyema, wakati maiti
wakiwa wamehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali
hiyo ya Rufaa.
Kaimu
Kamanda alisema kuwa, polisi wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa ambaye ni
dereva wa gari T 957 BUV aina ya Scania lenye trela namba T 919 BVA ili
aweze kufikishwa katika vyombo vya sheria .
0 comments:
Post a Comment