Makamu
wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki Bw. Javiero Rielo
amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli kuwa maandalizi ya kuanza kwa ujenzi wa bomba la mafuta la
kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania
yanaendelea vizuri na kwamba kampuni hiyo imedhamiria kuhakikisha mradi
huo unatekelezwa kwa mafanikio.
Bw.
Javiero Rielo amesema hayo jana tarehe 24 Agosti, 2016 Ikulu Jijini Dar
es Salaam alipokutana na Rais Magufuli kwa lengo la kumpa taarifa juu
ya maendeleo ya maandalizi ya kuanza kwa ujenzi wa bomba la mafuta.
Mradi
huo utahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilometa 1,410 ambalo
litasafirisha mafuta ghafi kutoka ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari
ya Tanga nchini Tanzania na unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa
moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.
Gharama
za mradi wa ujenzi wa bomba hilo zinatarajiwa kuwa takribani Dola za
Kimarekani Bilioni 4 na Kampuni ya Total inasema fedha hizo zipo tayari.
Akizungumza
baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli amesema anaamini kuwa
mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania, Uganda, Kampuni ya
Total na nchi jirani.
Amebainisha
kuwa pamoja na kwamba Tanzania ipo katika mazingira mazuri ya
kutekeleza mradi huo, Serikali yake itatoa ushirikiano mkubwa ili
kufanikisha mradi huo.
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli amepokea hati za utambulisho kutoka kwa
mabalozi watatu wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi
waliowasilisha hati zao ni Mhe. Ian Myles – Balozi wa Canada hapa
nchini, Mhe. Prasittiporn Wetprasit – Balozi wa Thailand hapa nchini
mwenye makazi yake Mjini Nairobi nchini Kenya na Mhe. Harald Gunther –
Balozi wa Austria hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Nairobi nchini
Kenya.
Pamoja
na kuwasilisha hati zao za utambulisho Mabalozi hao wameelezea
kufurahishwa na mahusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi zao
na Tanzania na wameahidi kufanya kazi bega kwa bega na Serikali ya
Tanzania ili wananchi wa pande zote wanufaike na matokeo ya ushirikiano
huo hususani katika uwekezaji na biashara.
Kwa
upande wake Rais Magufuli amewahakikishia Mabalozi hao kuwa Serikali
yake itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na nchi
hizo na ametoa wito kwa Mabalozi hao kuzishawishi zaidi nchi zao na
wawekezaji katika nchi hizo kushirikiana na Tanzania katika ujenzi wa
viwanda, uongezaji thamani ya madini, kuendeleza kilimo hususani kilimo
cha umwagiliaji, uzalishaji wa nishati na biashara mbalimbali.
Pia
Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi wa Thailand na Austria kuanzisha
ofisi za Ubalozi hapa nchini ili kurahisisha na kuharakisha shughuli za
kibalozi.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
24 Agosti, 2016
0 comments:
Post a Comment