WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema kuanzia sasa ni marufuku kuweka bei ya
tumbaku kwa dola za Marekani kwa sababu imechangia kuwaumiza wakulima wa
zao hilo.
Amesema
wanunuzi wa zao hilo wana uhuru wa kuweka bei zao kwa dola lakini bei
hiyo itafsiriwe kwa shilingi za Kitanzania ili wakulima waweze kutambua
bei elekezi tangu mwanzo wa msimu.
Ametoa
kauli hiyo Jumatano, Agosti 9, 2017 wakati akizungumza na wadau wa zao
la tumbaku zaidi ya 600 wakiwemo wabunge, viongozi wa dini, chama na
Serikali kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Isike-Mwanakiyungi,
mjini Tabora.
Hivi
sasa bei elekezi kwa msimu huu wa tumbaku ni dola mbili za Marekani kwa
kilo moja ya tumbaku sawa na sh. 4,400 hadi sh. 4,500 za Tanzania.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya kwanza ya ziara yake
mkoani hapa, alionya juu ya mkanganyiko unaowapata wakulima na viongozi
wa vyama vya msingi (AMCOS) kwenye kutafsiri bei ya zao hilo kutoka dola
za Marekani.
“Kwa
mfano, mkulima anapouza tumbaku anaambiwa kilo zake zina thamani ya
dola za marekani 90. Wakati anapokuja kulipwa bei ya shilingi inakuwa
imebadilika, kwa hiyo kama aliuziwa wakati thamani ya dola moja ikiwa ni
sh. 1,500/- na wakati wa kulipwa imefikia sh. 2,000/- hatalipwa kwa bei
ya sasa. Bali atalipwa kwa bei ileile ya zamani jambo ambalo
linamuumiza mkulima,” amesema.
Akiwa
hapohapo ukumbini, Waziri Mkuu aliwauliza wawakilishi wa benki za CRDB
na NMB bei ya dola moja ni sawa na shilingi ngapi kwa hapo Tabora,
alijibiwa kwamba katika benki ya CRDB, dola moja ya Marekani inauzwa kwa
sh. 2,200 ilhali katika benki ya NMB, dola moja inauzwa kwa sh. 2,167.
0 comments:
Post a Comment