Monday, August 7, 2017

MHANDISI LWENGE ATOA HEKO KWA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA KUANZISHA MFUMO RAHISI KWA WANANCHI KUPATA TAARIFA ZIHUSUZO NISHATI JADIDIFU

Na Mathias Canal, Lindi

Wizara ya Nishati na Madini imetambua kadhia iliyokuwa inawakumba wananchi kupata taarifa sahihi na za uhakika kuhusu masuala ya nishati jadidifu hapa nchini na hatimaye kuanzisha mfumo rahisishi wa taarifa unaojulikana kama Tanzania Renewable Energy Information Management System (TREIMS).

Mfumno huu utasaidia kuhakikisha kwamba taarifa sahihi za masuala ya nishati jadidifu zinapatikana ambapo pindi taarifa zinapopatikana zitakuwa zinahakikiwa kabla ya kuwafikia watumiaji.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Greyson Lwenge (Mb) amesifu mfumo huo kuwa utapunguza muda wa wadau unaotumika kutafuta taarifa zinazohusu nishati jadidifu sambamba na kufuatilia kwa urahisi maenedeleo ya miradi ya nishati jadidifu inayotekelezwa hapa nchini.

Mhe Lwenge alisema kuwa kulikuwepo na upatikanaji hafifu wa taarifa za masuala ya nishati jadidifu hapa nchini tatizo ambalo lilichangia kuwa na maendeleo kidogo katika sekta ndogo ya nishati jadidifu.

Alisema serikali isingeweza kufikia malengo kwa uduni wa taarifa lakini hatua ambao imefikiwa sasa na Wizara ya nishati na madini itakuwa mbadala wa mafanikio kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Mfumo huu unajumuisha taarifa zihusuzo sera, sheria na mifumo mingine ya kisheria inayohusika na usimamizi na uendeleaji wa sekta ndogo ya nishati jadidifu.

Mhandisi Lwenge pia amesifu Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvvuvi kwa kurejesha tena Maonesho hayo na Nanenane katika Mkoa wa Lindi ikiwa ni mara ya nne mfululizo huku akieleza kufurahishwa jinsi wananchi wanavyoendelea kujitokeza kupata elimu ya Kilimo Mifugo na Uvuvi.

Alisema kuwa kauli mbiu ya maonesho ya Nanenane kwa mwaka 2017 inayosema “Zalisha kwa Tija Mazao na Bidhaa za Kilimo Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati” inaakisi mafanikio na fursa kwa kila mwananchi kupata mbinu bora za kilimo mifugo na uvuvi.

Sikukuu ya wakulima inayofahamika kuwa Nanenane ina sherekewa nchini kote tarehe 8 Agosti kila mwaka. Sherehe hiyo inatayarishwa na kuratibiwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kuhusisha Taasisi, Wizara na mtu mmoja mmoja wanaoshughulika na kilimo. 
MWISHO.

Mgeni rasmi Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Greyson Lwenge (Mb) alipotembelea banda la Wizara ya Nishati na Madini wakati wa Maonesho ya Nanenane ambayo kitaifa yanafanyika Katika Viwanja vya Ngongo Mkoani Lindi.
Mgeni rasmi Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Greyson Lwenge (Mb) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kutembelea banda la Wizara ya Nishati na Madini wakati wa Maonesho ya Nanenane ambayo kitaifa yanafanyika Katika Viwanja vya Ngongo Mkoani Lindi.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More