Tuesday, July 5, 2016

Mbunge wa Mwibara Kangi Lugola Aionya Jamhuri Kumsotesha Mahakamani

KANGI Lugala, Mbunge wa Mwibara ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa onyo kwa Jamhuri kwa kukwamisha kuwasomea maelezo ya awali katika kesi inayowakabili.

Lugola, Victor Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa na Murad Sadiq, Mbunge wa Mvomero wanatuhumiwa kuomba rushwa ya Sh. 30 mil kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Gairo tarehe 15 Machi mwaka huu.

Lugola alitoa madai hayo jana mbele ya Thomas Simba, Hakimu Mkazi katika mahakama hiyo baada ya wakili wa serikali Denis Lekayo kueleza kuwa, waendesha mashtaka wa kesi hiyo hawapo.

Wakili Lekayo alidai kuwa, shauri hilo liliitishwa kwa ajili maelezo ya awali lakini waendesha mashtaka hawakupo.

Kutokana na maelezo hayo Lugola aliiomba mahakama ikemee tabia hiyo ya kuahirishwa kesi mara kwa mara.

Lugola alisema kitendo hicho kinawanyima haki yao ya msingi ya kufanya shughuli zao za Bunge.

Baada ya Lugola kueleza hayo, wakili wa Serikali, Denis Lekayo aliiomba mahakama radhi na kusema ‘tutafanya haraka kesi iendelee.’

Hakimu Simba alisema, kauli iliyotolea na mshitakiwa ni ya msingi. Baada ya kueleza hayo aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe 12 Julai mwaka huu kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More