Wednesday, July 13, 2016

Vinara wa Kutengeneza nyaraka bandia za Serikali watiwa mbaroni

Watu watatu wanaosadikiwa kuwa vinara wa kutengeneza vyeti bandia pamoja na nyaraka mbalimbali za Serikali wamekamatwa eneo la Buguruni wakiwa na mitambo yao. 

Kukamatwa kwao kulitokana na msako mkali uliofanywa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam hivi karibuni na hatimaye watuhumiwa walinaswa wakiwa nyumbani wanakoishi eneo la Buguruni Ghana wakitengeneza nyaraka bandia.

Kamanda wa kanda hiyo, Simon Sirro aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Ashraff Maumba (37) mkazi wa Buguruni Ghana, Mwamba Seif (38) mkazi wa Mnyamani, na Mahmudu Zuber (24) mkazi wa Buguruni.

 Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba Julai 8, saa 4.00 usiku walifanya upekuzi katika nyumba wanayoishi na kukuta nyaraka mbalimbali vikiwamo vyeti bandia vya kidato cha nne 50 na vyeti vya vyuo vya uuguzi.

Kamanda huyo alisema nyaraka nyingine bandia zilizokamatwa ni stika 20 za Mamlaka ya Usafirishaji wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), vyeti vya kuzaliwa 10 na vya Chuo cha Ufundi (Veta).

Nyaraka nyingine zilizokamatwa, kwa mujibu wa Sirro ni leseni za biashara, stika 100 za bima za magari, mitambo na vivuli 10 bandia vya vyeti vya Chuo cha Biashara (CBE).

Katika upekuzi huo pia walikamata mihuri mbalimbali ya ofisi za Serikali na binafsi ukiwemo muhuri wa Bibi na Bwana.

“Tulifanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vya kutengenezea nyaraka zikiwamo karatasi maalumu zilizo na nembo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kutengeneza zaidi ya kadi 500 za vyombo vya moto, kompyuta nne na mashine moja ya kuchapisha,” alisema Sirro.

 Kamanda Sirro alisema watuhumiwa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi huku upelelezi ukiendelea na ukikamilika watafikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka yanayowakabili.

Katika hatua nyingine, Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo alisema Serikali haitakubali kuhujumiwa na watu wachache hivyo itachukua hatua kali kwa wote wanaojihusisha na utengenezaji vyeti bandia vya Serikali.

“Tunashukuru jeshi la polisi kuibua shina ambalo lilikuwa linatusumbua sana kutambua ni wapi wanatengeneza vyeti hivi vya bandia na tumepata taarifa za mawakala wanaofanya ujanja huo,” alisema Chibogoyo.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More