Msajili wa Hazina amaliza maneno kuhusu Twiga Bancorp, asema itaendelea kuhudumia wateja kama kawaida
Kumekuwepo na maneno mengi ambayo yamekuwa yakizungumzwa kuhusu benki ya Twiga Bancorp, tangu Rais John Magufuli alipoiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuchukua hatua kwa benki zote ambazo zimekuwa hazifanya vizuri ikiwepo benki ya Twiga na hivyo wananchi wengi wakawa wakiamini kuwa benki hiyo itafutwa
Akielezea kuhusu hatua zinazochukuliwa kwa benki hiyo, Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru alisema kuwa ni kweli Rais Magufuli aliagiza jambo hilo lakini alikuwa na maana nyingine tofauti na watu wengi ambavyo wamekuwa wakizunguzia jambo hilo ambalo kwa namna kubwa anaamini linachangiwa na vyombo vya habari.
Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru akitoa ufafanuzi kuhusu jambo hilo mbele ya waandishi wa habari. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Twiga Bancorp, Cosmas Kimario. (Picha zote na Rabi Hume, Mo Blog)
Alisema kuwa rais aliagiza BoT kuzisimamia benki ambazo zimekuwa hazitoi faida ili ziweze kusimama zenyewe na kuacha kutumia pesa ya umma ambayo imekuwa haizalishi faida yoyote na hivyo kuonekana inafanya matumizi mabaya ya fedha za serikali.
"Rais alitaka hatua zichukuliwe ili kuzifanya benki hizo ikiwepo Twiga kusimamiwa ili ziweze kuwa na tija na mwenyewe aliweka wazi kuwa hayupo tayari pesa ya umma kutumiwa bila faida,
"Baada ya hilo tumeanza kutafuta njia mbadala kuona ni jinsi gani itaweza kufanya vizuri kama ikishindikana tutatafuta hata wawekezaji lakini biashara itaendelea kuwepo kama kawaida," alisema Mafuru.
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo wa kupata maelezo kutoka kwa Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru kuhusu benki ya Twiga Bancorp.
Aidha alieleza kuwa kumekuwepo na taarifa kuwa wateja wa benki hiyo wapo katika hatari ya kupoteza pesa zao kutokana na benki hiyo kuwa katika hasara na hivyo kuwatoa hofu kuwa benki ipo na pesa zipo salama na wasiwe na wasiwasi kuhusu hilo.
Pia Mafuru aliongeza kuwa pamoja na kuwa katika mpango wa kutafuta mbinu mpya ya kutumia ili kuifanya benki hiyo kuwa na tija lakini pia taarifa ambayo imetolewa wiki iliyopita inaonyesha kuwa kwa mara ya kwanza benki hiyo imeingiza faida na hivyo kuwa na matumaini mapya kuwa kuna uwezekano wa benki hiyo kuanza kufanya vizuri katika biashara.
Na Rabi Hume, Mo Blog
0 comments:
Post a Comment