Friday, July 22, 2016

Kesi za Uhujumu Uchumi zaigiza Bilioni 29

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema Mahakama Kuu chini ya kitengo kinachosimamia kesi za kuhujumu uchumi imetoa adhabu ya kifungo na kulipa faini ya Sh29 bilioni kwa watu 12 baada ya kutiwa hatiani.

Pia, alisema Mahakama ya Mafisadi iliyoahidiwa na Rais John Magufuli wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, itakapoanza itashugulikia kesi za ufisadi zenye ushahidi.

Dk Mwakyembe alisema hayo jana kwenye mahojiano katika kipindi cha 360 kinachorushwa moja kwa moja, asubuhi siku za wiki na Televisheni ya Clouds.

 “Tuna kesi 176 za kuhujumu uchumi tangu Juni mwaka jana hadi sasa. Kesi 13 zimekamilika, watu 12 wamehukumiwa vifungo vya jela na tunawadai Sh29 bilioni kwa hiyo kama mtu alikuwa na ‘kastore’ tutauza tupate hiyo pesa,” alisema Dk Mwakyembe.

Aliongeza: “Nchi ilipofikia tunataka tuachane na hizi tabia za udokozi unapopewa mamlaka ya kuhudumia umma.”

 Alipoulizwa kuhusu mahakama ya mafisadi alisema: “Hatujaanzisha Mahakama, tumeanzisha divisheni (kitengo) ambacho kitasimamia kesi hizo kwa haraka na kwa weledi zaidi.”

Itakumbukwa kuwa Aprili Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipowasilisha hotuba ya makadirio na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu bungeni alisema Serikali imeanzisha Divisheni ya Rushwa na Ufisadi ya Mahakama Kuu.

Majaliwa alisema mahakama hiyo itaanza kushughulikia kesi 10. Dk Mwakyembe alipoulizwa kama kuna kesi zozote zinazohusu EPA, Escrow au Richmond zitakazo sikilizwa, alijibu: “Sheria tunayotumia ni kwamba, kesi za jinai hazina vizuizi kwa upande wa Jamhuri.Hata kama ulichukuwa miaka 20 iliyopita, kama ushahidi unapatikana tutaendelea. Lakini hatuna interest kufufua makaburi ya huko nyuma.” 

Kuhusu mchakato wa Katiba inayopendekezwa alisema: “Ni kiporo ambacho tumepokea Serikali ya awamu ya tano na lazima tukimalize.”

Alisema kinachofanyika sasa ni kufuata Katiba kwa sababu mchakato huo ulisimama kupisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

“Tusingeweza kusimamisha uchaguzi kwa ajili ya kupiga kura ya maoni. Kwa hiyo tunasubiri wenzetu NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) wawe tayari ili mchakato uweze kuendelea,” alisema.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More