Nachukua
fursa hii kuwapongeza Sana kwa kazi kubwa mliyoifanya kwenye chaguzi
ndogo za udiwani na ubunge zilizomalizika hivi punde nchi nzima. Ingawa
hatukushinda hata kata moja katika kata 20 zilizokuwa zinashindaniwa,
lakini tumefanya vizuri kwenye matokeo.
Chama
chetu kilisimamisha wagombea katika Kata 5 kati ya Kata 20 nchi nzima,
Isagehe (Kahama), Kijichi (Dar es salaam), Kiwanja cha Ndege (Morogoro),
Nkome (Geita) na Tanga (Songea). Na pia tulisimamisha Mgombea katika
Uchaguzi wa Ubunge Dimani (Zanzibar).
Baada ya kufanya kampeni kubwa mzunguko wa kwanza tuliweza kutazama na kuamua kuwekeza kwa nguvu kwenye Kata 3.
Pamoja
na kuwa hatukushinda Udiwani wala Ubunge katika Uchaguzi , matokeo
yameonyesha kukua kwa kasi kubwa kwa Chama chetu. Tukishika nafasi ya 2
katika Kata ya Isagehe (Halmashauri ya Mji wa Kahama) kwa kupata mara 2
ya Kura ya zile ambazo tulipata katika Uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, hali
hiyo ipo pia katika Kata ya Kijichi jijini Dar es salaam na Nkome
mkoani Geita.
Ni
dhahiri kuwa sauti yetu imesikika, Kampeni zetu zilizojikita juu ya
masuala ya wananchi zimeleta matunda kiasi.Nawapongeza sana viongozi
wetu wa Chama katika Jimbo la Kahama Mjini kwa kazi kubwa tulioifanya na
kupiga hatua kubwa. Nawaomba wasikate Tamaa bali wawekeze kwenye
kuimarisha uongozi wa Chama Jimbo zima, kwenye kata zote ili kuwa tayari
kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Katika
Kata za Nkome mkoani Geita na Kijichi mkoani Dar Es salaam tumefanya
kazi kubwa Sana. Wagombea na viongozi wetu wa Chama wa mikoa hii na kata
hizi wamepigana kwenye mazingira magumu sana ya ushindani mkali wa
kisiasa. Kata hizi zimetupa fundisho kuwa wananchi wanataka ushirikiano
wa vyama vya upinzani. Ujumbe huo umefika na nawaomba viongozi wetu wa
Chama wajiandae kufanya kazi na vyama vingjne. Ubinafsi, roho mbaya,
chuki na kukomoana hakuwezi kutusaidia. Lazima tubadilike sisi wenyewe
kwanza kabla ya kutaka kuleta mabadiliko kwa wananchi.
Katika
Kata ya Tanga Manispaa ya Songea na kata ya Kiwanja cha Ndege Manispaa
ya Morogoro wanachama wetu na viongozi walifanya kazi kubwa kuonyesha
uwepo wa Chama kwenye maeneo yao. Wamepanda mbegu za Chama na kwa uwezo
wa mungu mbegu hizi zitamea na kuzaa matunda.
Ni
muhimu kukemea hali ya uchaguzi ya Dimani, Naibu Katibu wa Itikadi,
Uenezi na Mawasiliano ya Umma – Zanzibar, ndugu Seif Hamad, ni miongoni
mwa waliojeruhiwa kutokana na kipigo baada ya kutolewa Kituoni alipokuwa
Wakala wa Chama kwa kupinga udanganyifu wa uchaguzi. Bado uchaguzi kwa
upande wa Zanzibar hauendeshwi katika misingi ya haki na demokrasia.
Nawapongeza
na kuwashukuru sana wanachama wote wa ACT Wazalendo mliojitoa kwa Hali
na Mali kushiriki kampeni katika uchaguzi huu. Shukran za dhati Kabisa
kwa madiwani wetu waliotumia gharama zao kwenda kuishi vijijini kutafuta
kura za Chama chetu. Sina cha kuwalipa mungu atawalipa. Mmeonyesha
mapenzi ya dhati kwa Chama chenu. Mmeonyesha uzalendo wa dhati kwa
vitendo.
Nawapongeza
viongozi wa Chama wote wakiwemo wale kwa Kitaifa kuanzia Mwenyekiti
wetu – Mama Anna Elisha Mghwira, Makamu Mwenyekiti – Mzee Shaaban Mambo,
Kaimu Katibu Mkuu – ndugu Said Sanani, na Naibu Katibu Mkuu – ndugu
Msafiri Mtelemwa kwa kazi kubwa walioiafanya. Nawapongeza pia makatibu
wa Kamati za Makao Makuu ya Chama kwa kuwa waratibu wa kata
zilizoshiriki uchaguzi na kwa wale waliokuwa makao makuu kwa kufanya
kazi kubwa ya kuwasadia wenzao waliokuwa kwenye mapambano. Kwa Kweli
tumefanya kazi kama timu na sote tumechangia matokeo haya tuliyoyapata.
Uchaguzi
umekwisha. Badala ya kutumia muda wetu kujadili matokeo, tukubali
tumeshindwa na kuanza kujipanga kujenga Chama kwenye maeneo yetu.
Tuwaunge mkono walioshinda lakini pia tuwakosoe wanaposhindwa
kuwajibika. Tusiache kuwasemea wananchi na kuhangaika na changamoto zao
za maisha – msingi wetu wa Siasa zinazojikita juu ya masuala ya wananchi
ni muhimu sana.
Ndio
kazi yetu hii Kama Chama cha siasa. Tulitumia fursa ya kampeni za
chaguzi ndogo kupaza sauti kwenye masuala ya kitaifa na tulifanikiwa
Sana kwenye masuala mbalimbali na kutengeneza ajenda za kitaifa.
Tusichoke kuendelea kuwa Chama cha masuala na sio matukio. Chama cha
hoja Badala ya viroja. Chama cha UTU.
Tuendelee
kutaka shughuli za kisiasa kuendelea kwa mujibu wa Sheria. Tuendelee
kulaani vikali uamuzi wa Serikali kuzuia vyama vya siasa kufanya
mikutano ya hadhara.
Ahsanteni Sana
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama (KC)
ACT Wazalendo
Januari 23, 2017
0 comments:
Post a Comment