Watu
wanaodaiwa majambazi wamepora kiasi cha fedha kinachokadiriwa kuwa
zaidi ya shilingi milioni 25 katika makutano ya barabara ya Mandela na
Nyerere, eneo la Tazara, Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea jana saa 4 asubuhi wakati gari hilo likiwa kwenye foleni ya magari eneo hilo la taa za Tazara.
Watu hao wameporwa katika eneo ambalo huwa askari doria wametanda, lakini wakikamata pikipiki zinazotokea eneo la Buguruni.
Aidha
taa za Tazara yaliko makutano ya barabara kutokea Buguruni, Temeke,
Kariakoo/Posta na Gongo la Mboto ndilo eneo lenye askari wengi wakiwemo
wa usalama barabarani.
Wakati
tukio likifanyika kulikuwepo askari wenye magwanda maalumu ya askari
doria zaidi ya watano wakivurumushana na waendesha pikipiki upande wa
Barabara ya Mandela kutokesa Buguruni. Hata hivyo imeelezwa kuwa watu
hao waliokuwa wakipeleka benki hawakuwa na ulinzi kama inavyoshauriwa na
Jeshi la Polisi.
Majambazi
hao waliokuwa watatu, walipora fedha hizo katika gari ndogo aina ya
Toyota Rav4 yenye namba za usajili T 455 DFN mali ya kampuni ya
kutengeneza mabati ya Sun Share iliyokuwa ikiendeshwa na dereva
aliyejitambulisha kwa jina la Richard Charles.
Kwenye gari pia alikuwepo mfanyakazi mwingine wa kampuni hiyo, mwenye asili ya China, aliyetambulika kwa jina la Cheng Deng.
Kwa
mujibu wa dereva wa gari hiyo, Charles, walikuwa wakizipeleka fedha
hizo benki eneo la Quality Centre na ndipo walipovamiwa na watu hao
wakiwa na pikipiki aina ya boxer wakati magari yakiwa kwenye foleni
wakisubiri taa ziwaruhusu kupita kutoka barabara ya Mandela.
Charles
alisema majambazi hao walimwamrisha kufungua mlango na kuwapatia begi
la fedha lililokuwa limewekwa katika kiti cha nyuma huku wakimtishia kwa
bastola kabla ya kuvunja kioo cha nyuma cha gari hilo na kubeba fedha
hizo na kutokomea nazo.
“Kwa
kweli hata sielewi mpaka sasa hivi kilichotokea. Walikuja watu wawili
mmoja upande wangu mwingine wa bosi wangu wakinitishia kwa bastola
nifungue mlango niwape begi la fedha. Ghafla mtu mwingine akavunja kioo
cha nyuma kwa kutumia kitako cha bastola na kubeba begi la fedha na
kutokomea” alisema Richard.
Askari
wenye silaha walifika katika eneo la tukio dakika 20 baada ya tukio
hilo wakaishia kuhoji. Hata hivyo askari mmoja ambaye hakutaka
kujitambulisha jina lake alilaumu tabia ya baadhi ya watu kusafirisha
kiasi kikubwa cha fedha pasipo kuomba ulinzi wa polisi jambo
linalohatarisha usalama wao na mali zao.
“Kama
walijua wanasafirisha kiasi kikubwa hicho cha fedha kwa nini
wasingeomba hata ‘escort’ (kusindikizwa kwa ulinzi) ya polisi? Hili ni
tatizo, hasa katika kipindi hiki kigumu cha upatikanaji wa fedha, watu
wanatakiwa kuchukua tahadhari mapema.” alisema askari huyo.
Credit: Habari Leo
Credit: Habari Leo
0 comments:
Post a Comment