Mkulima
wa tumbaku aliyesafiri kutoka Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, Moshi
Rubibi akitafuta upenyo wa kumfikishia Rais John Magufuli kilio cha
wakulima, alifanikiwa kufanya hivyo mjini Bukoba wa kutumia staili
iliyomvuta Rais kumsikiliza.
Awali,
mkulima huyo anayewakilisha wenzake zaidi ya 60 alikwama kufanya hivyo
wakati Rais Magufuli alipokuwa kwenye mapumziko wilayani Chato mkoani
Geita baada ya kuzuiwa na walinzi lakini bila kukata tamaa alimfuata
Rais mjini Bukoba baada ya kusikia anafanya ziara.
Utaratibu
wa Rais Magufuli kutaka kusalimiana na wananchi baada ya mkutano ndiyo
uliofanikisha mpango wa mkulima huyo kwani aliamua kupiga kelele
mfululizo kwa mbali akilitaja jina la Rais huku akipunga hewani mkono
uliokuwa na bahasha ya kaki.
Pamoja
na kudhibitiwa na walinzi, sauti ya mkulima huyo ilizidi kuchomoza kwa
nguvu hali iliyomfanya Rais Magufuli aliyekuwa anaondoka kwenye eneo la
mkutano kupiga hatua kadhaa nyuma na kuwaambia walinzi wake wamuache
amsikilize.
Huku
akitweta na kuhema kwa nguvu baada ya kuruhusiwa kumfikia Rais
Magufuli, mkulima huyo alimwambia kuwa yeye ni mwenyeji wa Urambo,
Tabora na amemtafuta ili kumfikishia malalamiko ya wakulima wa tumbaku
wanaopigwa chenga kulipwa mafao yao.
Alisema
wakulima hao wanadai zaidi ya dola za Marekani 98,000 (zaidi ya Sh200
milioni) za mauzo ya tumbaku waliyouza kupitia Bodi ya Tumbaku tangu
Septemba, 2015 na kuwa wanashawishiwa kutoa rushwa ili wapewe haki yao.
Alimwambia
Rais kuwa wameambiwa watoe dola 10,983 ili waweze kulipwa fedha zao
kupitia tawi la Benki ya CRDB Urambo na kuwa kati ya kiwango wanachodai
cha mauzo ya tumbaku wakubali kulipwa dola 87,017 tu.
Mkulima
huyo alisema wamefikisha suala hilo kwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo na
kukosa ufumbuzi na kuwa walilipeleka pia kwa aliyekuwa Waziri wa Kilimo
na Mifugo, Mwigulu Nchemba ambaye alionyesha kuwa tayari kulishughulikia
lakini kabla ya kufanya hivyo, alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi.
Baada
ya kumsikiliza takribani kwa dakika nne, Rais Magufuli alimkabidhi
mkulima huyo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Jenista Mhagama na kuagiza apewe
taarifa baada ya siku tano jinsi walivyoshughulikia suala hilo.
0 comments:
Post a Comment