Mgombea wa Urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad
amemuomba Rais Jakaya Kikwete na Rais Ali Mohamed Shein kubeba dhamana
ya uongozi katika siku hizi chache zilizobaki za uongozi wao kwa
kusimamia katiba na sheria za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mtendeni Maalim Seif
amesema marais hao wawili kuheshimu maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya
tarehe 25 Oktoba na kuwataka washirikiane nae katika kuinusuru
Zanzibar.
“Nawaomba sana Rais Kikwete na Rais Shein kukwepa matumizi ya nguvu na
badala yake tushirikiane kutunza amani na haki za wananchi. Mimi niko
tayari kushirikiana nao kama ambavyo nimekuwa nikifanya mara zote.
Tushirikiane kuiepushia Zanzibar na Tanzania fedheha ya kimataifa”.
Alisema Maalim Seif.
Akizungumzia kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi iwapo ni halali au sio
halali Maalim Seif amesema lile lilikuwa ni tamko binafsi la Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha ambapo Chama Cha
Wananchi (CUF) kimetiwa nguvu na tamko la Makamishna wawili wa Tume
waliothibitisha kwamba tamko lile ni lake binafsi.
“Ni kwamba hakukuwa na kikao cha Tume kilichokaa kuamua yaliyosemwa na
Jecha, na kwamba hakuna misingi ya kikatiba na kisheria ya tamko lile”
alisema Maalim Seif na kuongeza kwamba.
“Jana jopo la wanasheria wa CUF lilikutana kuangalia kwa kina kama kuna
misingi ya kikatiba na kisheria ya tamko lile binafsi la Jecha Salim
Jecha, na limetoa hoja za msingi zifuatazo kwa kuanzia muundo wa Tume
ambapo Kifungu 119(1) kinaanzisha Tume ya Uchaguzi yenye wajumbe saba
(7) akiwemo Mwenyekiti wao.
Alisema (1) Kifungu 119 (10) kinatamka kuwa: “Kiwango cha mikutano ya
Tume ya Uchaguzi ni Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wane na
kila uamuzi wa Tume ni lazima uungwe mkono na Wajumbe walio wengi”.
Aidha alisema (1) Kwa sababu Tume haikukaa kwa pamoja ikiwa na
Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti na angalau wajumbe wengine wanne, na kwa
sababu maamuzi yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume yalikuwa ni yake peke
yake, maamuzi hayo kikatiba ni batili na hayana nguvu zozote.
Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF alisema waangalizi wote wa
uchaguzi ikiwa ni pamoja na SADC, AU, Commonwealth Observer Team,
European Union Election Observation Team, Waangalizi kutoka Uingereza na
Marekani, na TEMCO, wote walisema mbali na dosari ndogo ndogo uchaguzi
ulikuwa huru, wa haki na amani.
Aidha aliwaambia waandishi wa habari kwamba Mwenyekiti wa ZEC mwenyewe
naye pia alisema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki ambapo Mwenyekiti huyo
huyo alisimamia kazi ya uhakikiwa matokeo na kutia saini fomu za
matokeo yaliyohakikiwa na kuthibitishwa za majimbo 31 ya Unguja na
kuyatangaza matokeo hayo kabla.
“Kwa nini ghafla ilipofika siku ya tatu ambayo ni jana aligeuka na
kukataa kuendelea na uhakiki na badala yake kudai eti kulikuwa na mambo
kadhaa ya kufanya uchaguzi huo usiwe huru na wa haki? Tena dosari
zenyewe za tamko lake eti ni pamoja na wajumbe wake kuvua mashati na
kutaka kupigana” alisema Maalim.
Akizungumzia suala la baraza la Wawakilishi jipya Maalim Seif alisema
Kifungu 92(1) cha Katiba ya Zanzibar kinaeleza kwamba maisha ya Baraza
la Wawakilishi ni miaka mitano tokea lilipoitishwa mkutano wake wa
mwanzo hivyo Kifungu 90(1) kinaeleza kwamba mkutano wa mwanzo wa Baraza
la Wawakilishi utafanyika si zaidi ya siku 90 tokea Baraza lilipovunjwa
kwa ajili ya kuitishwa uchaguzi.
Kuna masuali kadhaa ya kujiuliza alisema Maalim Seif ikiwemo ni “Rais
yupi ataitisha Baraza?, Wawakilishi wapi wataitwa (wakati hawapo)?, Yote
haya yanaleta mgogogro wa kikatiba ambao umesababishwa na mtu mmoja
anayeitwa Jecha Salim Jecha kwa sababu tu ya kufuata maelekezo ya chama
chake cha CCM”. Alihoji Maalim Seif huku akionekana kuongea kwa
kujiamini.
Hata hivyo alisema kuna suali la muundo wa mpito ambapo kama uchaguzi
utarejewa, kama anavyotaka Mwenyekiti wa Tume, jambo ambalo alisema
halikubaliki kwa sababu ya kukosa misingi ya kikatiba na kisheria, ina
maana kuwa serikali itakuwa haipo.
Akitoa sababu za kutokuwepo Maalim Seif alisema kwanza muda wa Urais ni
miaka mitano kuanzia tarehe aliyochaguliwa kwa mujibu wa kifungu 28(2)
cha Katiba, Ingekuwa tamko la Jecha Salim Jecha ni halali, basi maana
yake hakuna Rais anayefuata kwa sababu ya kufutwa kwa uchaguzi, hivyo
hakutakuwa na kiapo cha kumuapisha rais mpya. Kwa msingi huo, msharti ya
kifungu cha 28(1)(a) hayana nafasi katika mtafaruku huu uliosababishwa
na mtu mmoja.
“Hiyo maana yake, kipindi hicho sasa kitakuwa tete na haijulikani
kikatiba ni nani ataongoza nchi? Tunasema hivyo kwa sababu vifungu vya
Katiba 33(1) na (2) havitumiki hapa kwa suala la kuwa wazi kwa kiti cha
Urais na kukaimiwa kwa nafasi hiyo”. Aliongeza.
Alisema hiyo ni kwa sababu nafasi ya Urais haipo kwa sababu itakuwa
imemaliza muda wake ifikapo tarehe 2 Novemba, 2015, siku ambayo Urais wa
Dk. Ali Mohamed Shein unakamilisha miaka mitano kamili.
Halikadhalika Maalim Seif alitaka kujua jee katika suala hilo suluhisho
ni nini? “Kutokana na hoja tulizozieleza hapo juu, ni wazi kwamba tamko
la Jecha Salim Jecha ni lake binafsi na kama tulivyotangulia kusema,
halina misingi ya kikatiba na kisheria.
Kwenye taarifa yake alisema kuwa
“… kwa uwezo nilionao …”. Masuala ya kujiuliza ni uwezo upi? Chini ya
kifungu kipi cha Katiba au Sheria ya Uchaguzi?” alihoji.
Katika kutilia nguvu hoja yake hiyo ya kisheria Maalim Seif alisema kwa
kifupi, ni kwamba Mwenyekiti wa ZEC uwezo huo hana kikatiba na kisheria
na kwa msingi huo, maamuzi yake hayo ni batili.
Kufuatilia masuali hayo ambayo majibu yake yapo kisheria Maalim Seif
alisema CUF inasisitiza kile kinachodaiwa na waangalizi wote wa
uchaguzi waliotoa taarifa zao kwamba uamuzi wa Mwenyekiti wa ZEC ni
uamuzi wake binafsi pekee na haukuwa uamuzi wa Tume, kwani hakukuwa na
kikao chochote cha Tume kilichokaa kufikia uamuzi huo.
Alisema uamuzi huo uwekwe upande na Jecha Salim Jecha amepoteza sifa ya
uadilifu ambayo ni msingi mkuu wa kazi ya Tume ya Uchaguzi katika
kusimamia maamuzi ya Wazanzibari ambao kikatiba (kwa mujibu wa kifungu
cha 9(2) (a) ndiyo wenye mamlaka ya kuwaweka madarakani viongozi wa
Serikali.
“Hivyo, anapaswa awajibike kwa hatua yake ya kuiingiza nchi katika
mgogoro pasina sababu yoyote na ajiuzulu” alisema Maalim Seif huku
akionekana na furaha katika mkutano huo wa waandishi wa habari.
Aidha alishauri Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar waendelee na
kazi ya kukamilisha uhakiki na majumuisho ya matokeo ya uchaguzi kwa
majimbo 14 yaliyobaki na kisha kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa Rais wa
Zazibar.
Alisema baada ya ukamilishaji huo alisema mshindi wa nafasi ya Urais wa
Zanzibar aapishwe, Viongozi wa CUF na CCM washirikiane kuunda Serikali
mpya ya Umoja wa Kitaifa itakayoiongoza Zanzibar katika miaka mitano
ijayo.
“Kwa maana hiyo, kitumike kifungu 42(6) cha Sheria ya Uchaguzi
kinachoeleza kwamba kama kuna matatizo yoyote katika vituo vya kupigia
kura a na matokeo hayawezi kutolewa ndani ya siku tatu; basi Tume
iendelee kuhesabu na kuhakiki kura na kutangaza matokeo ndani ya siku
tatu nyengine na shughuli za kiserikali ziweze kuendelea” aliongeza.
Katika hatua nyengine Malaim Seif alirejea tena kauli yake ya kuhimiza
Amani na kuwataka wafuasi wake na wananchama wa CUF na Wazanzibari wote
kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu na kutunza amani ya nchi yetu huku
wakitambua kwamba tutayasimamia maamuzi yao waliyoyafanya tarehe 25
Oktoba, 2015.
Baadhi ya wafuasi wa CUF wakiwa wamekusanyika
nje ya ofisi za CUF Mtendeni kusikiliza kauli za viongozi wao kuhusu
maamuzi watakayochukua baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi
0 comments:
Post a Comment