Saturday, October 31, 2015

Jesca: Siwezi kujiuzulu kwa shinikizo la majungu, fitina na vikundi vya uasi...


Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa Jesca Msambatavangu akizungumza na waandishi wa habari jana. 



Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Jesca Msambatavangu amesema hawezi kujiuzulu nafasi yake hiyo kwa shinikizo linalotokana na majungu, fitina na vikundi vya uasi vinavyoanzishwa ndani ya chama kwa lengo la kulinda maslai ya watu fulani.

“Hizi ni hoja zisizo na mashiko, hivi inawezekaneje mimi na hao wengine wanaowataja katika kipindi chote cha kampeni tufanye kazi ya kukihujumu chama, tuvumiliwe tuendelee na kazi hiyo, halafu tuhuma hizo zije zitolewe sasa baada ya kushindwa uchaguzi?” alisema.

Kwa kutumia vikao na taratibu zingine za katiba yake, CCM inapaswa kukaa chini na kufanya tathmini ya kina ili kujua sababu zilizopelekea wakapoteza jimbo na kata hizo.

Wanachama hao wanawatuhumu viongozi hao kuwahujumu katika Uchaguzi Mkuu wa mbunge, madiwani na rais hali iliyosababisha kipoteze jimbo hilo na halmashauri baada ya kupoteza kata 14 kati ya 18. 

Hivi karibuni, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Iringa Mjini, Ahamed Sawa alimtangaza Mchungaji Peter Msigwa aliyewania ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa mshindi baada ya kuzoa kura 43,154 dhidi ya kura 32,406 alizopata mgombea wa CCM Frederick Mwakalebela. 

Wagombea wengine na kura zao kwenye mabano ni Chiku Abwao wa ACT Wazalendo (411), Daudi Masasi wa ADC (123), Paulina Mgimwa wa Chausta (66) na Robert Kisinini wa DP (56). 

Wakiongea kwa kupokezana na bila kutaja majina yao wanachama hao waliokuwa wamebeba mabango yaliyowataka viongozi hao kuachia ngazi, walisema wanao ushahidi unaodhihirisha jinsi viongozi hao walivyofanya kazi iliyosababisha wapoteze jimbo, kata 14 na mgombea wao urais, Dk John Pombe Magufuli kupata kura 36,584 dhidi ya kura 38,860 alizopata mgombea urais wa UKAWA, Edward Lowassa. 

Katibu wa CCM Iringa Mjini, Elisha Mwampashi aliwataka wanachama hao kutumia vikao vyao vya kikatiba kuwasilisha malalamiko yao dhidi ya viongozi hao. 

“Tumieni vikao vya tawi na kata kuwasilisha ushahidi wenu na pale mtakahisi kuwepo kwa dalili za kuhujumiwa, leteni ushahidi wenu moja kwa moja kwangu ili tuuwasilishe kunakohusika haraka iwezekanavyo,” alisema.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More