Friday, October 9, 2015

MFUMUKO WA BEI WAPUNGUA


Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu Ephraim Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitangaza Mfumuko wa Bei wa mwezi Septemba, 2015 ambao umepungua hadi asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.4 ilivyokuwa mwezi Agosti, 2015.
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Septemba, 2015 umepungua hadi asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.4 ilivyokuwa mwezi Agosti, 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu Ephraim Kwesigabo amesema kupungua huko kwa mfumuko wa bei kunamaanisha kuwa, kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2015 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2015.
“Kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Septemba, 2015 kumechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Septemba, 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Septemba, 2014”, amesema Kwesigabo.
Aidha, Kwesigabo amefafanua kuwa, mwenendo wa bei za baadhi ya  vyakula zilizoonyesha kupungua mwezi Septemba, 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Septemba, 2014 ni pamoja na bei za ndizi za kupika kwa asilimia 4.0, matunda (asilimia 2.7), nazi (asilimia 13.3) na mbogamboga kwa asilimia 3.5.
Ameongeza kuwa baadhi ya bei za bidhaa zisizo za vyakula zilizoonyesha kupungua mwezi Septemba, 2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Septemba, 2014 ni pamoja na bei za gesi kwa asilimia 4.9, mafuta ya taa (asilimia 11.7), senti ya sofa (asilimia 5.7), dizeli (asilimia 3.5) na vifaa vya kielektoniki kwa asilimia 1.2.
Kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki,  Mfumuko wa Bei nchini una mwelekeo unaokaribiana kwa mfano Mfumuko wa Bei wa mwezi Septemba, 2015 nchini Kenya umeongezeka kidogo hadi asilimia 5.97 kutoka asilimia 5.84 mwezi Agosti, 2015 na Uganda umeongezeka hadi asilimia 7.2 kutoka asilimia 4.80 mwezi Agosti, 2015.
Kupungua kwa mfumuko nwa bei kwa mwezi septemba kumesababishwa na Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 159.04 kwa mwezi Septemba, 2015 kutoka 149.93 mwezi Septemba, 2014. Mfumuko wa Bei wa bidhaa za Vyakula na Vinywaji Baridi kwa mwezi Septemba, 2015 umepungua hadi asilimia 9.6 kutoka asilimia 10.2 ilivyokuwa mwezi Agosti, 2015.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More