MGOMBEA
ubunge wa jimbo la Mafinga Mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM),
Cosato Chumi amezilalamikia kampeni na propaganda alizozihita kuwa ni chafu
zinazofanywa dhidi yake na mgombea wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), William Mungai.
Akizungumza
na wanahabari juzi mjini Mafinga, Chumi anayepewa nafasi kubwa ya kushinda katika
kinyang’anyiro hicho alisema katika mikutano yake mgombea huyo amekuwa
akimtuhumu kwa wapiga kura wa jimbo hilo kwamba anao mpango wa kufuta biashara
ya bodaboda na biashara za minada katika
jimbo hilo, mambo ambayo si kweli.
“Mimi
Cosato
Chumi, nawahakikishia kuwa makundi haya ya waendesha bodaboda, bajaji,
taxi, wauza mboga, vikundi mbalimbali, wasanii, watu wa minanda na
makundi yote
ya wajasiriamali ni makundi muhimu sana kwangu,” alisema na kuwataka
wananchi wa jimbo hilo kumpuuza mgombea huyo na propaganda zake chafu.
Alisema
makundi hayo ni muhimu kwasababu ndiyo yanayorahisha upatikanaji wa huduma hizo
kwa wananchi wa jimbo hilo na yanamchangomkubwa katika kukuza uchumi wa mtu
mmoja mmoja, jimbo hilo na Taifa kwa ujumla.
“Na
ndio maana katika harakati zangu za kuwakwamia vijana kutoka katika lindi la
umasikini, pamoja na mambo mengi niliyofanya kwa vijana hao kabla hata
sijafikiri kugombea ubunge, nilikuwa mtu wa kwanza kuja na mpango wa
kuwakopesha vijana bodaboda ili wazitumie kujikwamua na umasikini,” alisema.
Alisema
ili kumkosanisha na wapiga kura katika makundi hayo, mgombea mwenzake huyo
amekuja na siasa za chuki, ufitinishi, uchonganishi na uongo akilenga
kujinufaisha kisiasa.
Alipotafutwa
kwa simu yake ya mkononi kujibu tuhuma hizo, Mungai hakupokea simu pamoja na
kupigiwa mara kadhaa.
Akiomba
wananchi wa jimbo hilo wamchague yeye kuwa mbunge, madiwani wote kutoka CCM na
mgombea urais Dk John Magufuli, Chumi alisema: “sina sababu nyingine ya kuomba
nafasi hii ya ubunge isipokuwa ni kwa ajili ya kuwatumikia kwa uadilifu,
uaminifu na kwa bidii katika kuhakikisha tunainyanyua Mafinga kwa maendeleo ya
kasi.
Alisema
hakuna sababu kwa jimbo hilo kukosa maji, huduma za afya, umeme, barabara
nzuri, wazazi kuendelea kutoa michango ya madawati wakati wamezungukwa na msitu
wa taifa wa Saohill na wajasiriamali kuendesha biashara zao kwa uhuru endapo
watamchagua kuwa mbunge wao.
Alisema
katika taifa linaloendelea kukua na kukomaa katika siasa za vyama vingi na
demokrasia ya uwazi na uwajibikaji ni muhimu wanasiasa wakajikita katika
kuelezea sera, mipango na vipaumbele vya namna gani jimbo hilo la Mafinga
litanyanyuliwa badala ya kupakana matope, kusingiziana na kueneza tuhuma zisizo
za kweli dhidi ya wengine.
0 comments:
Post a Comment