Friday, October 23, 2015

MKURUGENZI WA MAKAMPUNI YA APEX GROUP AOMBA WANANCHI KUDUMISHA AMANI NA UTULIVU KATIKA UCHAGUZI MKUU UTAKAO FANYIKA KESHO KUTWA KOTE NCHINI


Mkurugenzi Mkuu wa Makampuni ya Apex Group na Mwanaharakati,  Joseph Mhonda (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika kesho nchini kote. Kulia ni Ofisa Habari wa Makampuni hayo, Pipino Sudi.
 Mkurugenzi Msaidizi wa Idara Habari Maelezo, Vicent Tiganya (kushoto), akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni Ofisa Habari wa Makampuni hayo, Pipino Sudi na Mkurugenzi Mkuu wa Makampuni ya Apex Group na Mwanaharakati,  Joseph Mhonda.
Mkutano ukiendelea.

Na Dotto Mwaibale

MKURUGENZI Mkuu wa Makampuni ya Apex Group na Mwanaharakati, Joseph Mhonda amewataka wananchi kupiga kura kwa amani ili kulinda amani iliyopo nchini hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini kote kesho kutwa.

Akizungumza Dar es Salaam leo  Mkurugenzi huyo alisema amani ya nchi inapaswa kuzingatiwa katika kipindi hiki cha siku ya kupiga kura , siku ya kutangazwa washindi na siku ya kusubiria majibu ya mshindi.

"Siku hizi tatu ni ngumu sana lakini ni vyema wananchi wakawa makini katika kulinda amani na upendo wa nchi yetu kwani hii ndiyo nguzo kubwa katika kipindi hiki," alisema.

Mhonda pia alizungumza kuwa katika kutangazwa matokeo hayo pia ni vyema matokeo hayo wananchi kuyakubali kwa moyo mmoja kwani kutokubali matokeo kunaweza kuleta mkanganyiko wa amani.

Alisema amani ya nchi ikilindwa itakuwa ni vyema hasa katika masuala ya kuleta maenedeleo ya nchi hasa ukizingatia kuwa nchi inaenda kutafuta maendeleo.

Akizungumzia suala la kulinda kura Mhonda alisema  kila chama kinatakiwa kuwaamini mawakala ambao wamewaweka katika vituo na si kutaka kulinda  nje.

"Watu wanaosema kuwa kura zinatakiwa kulindwa watakuwa hawawaamini wale mawakala ambao wanaweka katika vituo vya kuwapiga kura ili kusimamia kura zao,"alisema.

Akizungumzia suala la mita 200 alisema hiyo ni sheria ambayo ipo katika tume ya uchaguzi  hivyo haina budi kutekelezwa.

Mhonda alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuchagua kiongozi bora ambaye atakuwa mstari wa mbele kupigania maendeleo ya wananchi.


0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More