Monday, October 19, 2015

Vijana wa CCM Washambuliwa Kwa Mapanga Wakati Wakienda Kuandaa Mkutano wa Mbunge wao


VIJANA wawili wanaoaminika kuwa ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Nzega, wamejeruhiwa na watu wasiojulikana baada ya kuvamiwa walipokuwa wakielekea kuandaa mkutano wa kampeni wa mgombea ubunge wa Nzega Mjini kwa tiketi ya chama hicho, Hussein Bashe.

Tukio hilo lilitokea saa tano usiku, Oktoba 15 mwaka huu katika kijiji cha Mbogwe ambapo vijana hao walijeruhiwa kwa mapanga na watu wasiofahamika na mmoja alivunjwa mguu.
 
Mganga wa zamu katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega, Dk Gwambaye Kimanuka alithibitisha kupokea majeruhi hao wawili na kusema walijeruhiwa vibaya sehemu za mwili.

Dk Kimanuka alisema jitihada mbalimbali za kuwapatia huduma zilifanyika lakini kutokana na majeraha walilazimika kuwahamishia Hospitali ya Rufaa kwa matibabu zaidi. 
 
Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Mariki Shaabani na Azizi Abudallah, wote wakazi wa Nzega Mjini.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nzega, Amos Kanuda alisema tukio hilo limepokelewa kwa masikitiko makubwa na kuiomba Polisi kulifuatilia ili wahusika wakamatwe.

Kanuda pia aliiomba polisi kuimarisha ulinzi na usalama katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu ili kila raia atumie haki yake kujitokeza kwa usalama kupiga kura kumchagua kiongozi anayemtaka.

Aliwataka wananchi na wanachama wa chama hicho kuwa wavumilivu na kudumisha amani na mshikamano katika kipindi hiki cha uchaguzi. Polisi mkoani hapa imethibitisha kutoka kwa tukio hilo na kusema watu wawili wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.

Wakati huo huo, vijana wawili wanaodaiwa kuwa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamegongwa na gari wakiwa katika shughuli za chama na kujeruhiwa vibaya. Watu hao wamelazwa katika kito cha Afya cha Eden kwa matibabu zaidi.

Mgombea ubunge wa Nzega Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Charles Mabula, alieleza kusikitishwa kwake kutokea kwa ajali hiyo iliyojeruhi wapiga kura wake. Polisi mkoani Tabora wamethibitisha pia kutokea kwa ajali hiyo.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More