Mara nyingi Rais Magufuli amekuwa akitoa kauli
akisisitiza Watu kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili wajiimarishie kipato
binafsi. Watu wanapolalamika kuwa maisha ni magumu, hakuna pesa mitaani jibu
analolitoa Rais Magufuli anasisitiza Watu kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kupambana na hali ya maisha iliyopo.
Rais Magufuli sio kiongozi wa kwanza nchini
kusisitiza juu ya Wananchi kufanya kazi kwa bidii. Kumbukumbu zinaonyesha hata
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere naye pia alikuwa akisisitiza
juu ya Watu kufanya kazi kwa bidii.
Wakati tunapata uhuru wetu mwaka
1961 kutoka kwa Waingereza kila Mtanganyika alikuwa na maana yake kichwani ya
kuelewa nini maana ya uhuru. Wapo walioamini kuwa huo ndio utakuwa mwisho
wa ubaguzi wa rangi, hadhi, kabila uliokuwa ukifanywa na Wakoloni; wengine
waliamini kupata uhuru ni kufanikiwa kuziondoa tawala mbovu,
nyonyaji na za kidhalimu za Wakoloni.
Licha ya mawazo mazuri waliyokuwa nayo baadhi
yao, lakini kwa upande wa mwasisi mwenyewe wa uhuru wetu alikuwa na
mtazamo tofauti kabisa na zilivyokuwa mawazo ya watu. Yeye Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere alikuwa na maana ya kipekee kabisa juu ya dhana nzima
ya uhuru.
Kwa upande wa Baba wa Taifa letu Mwalimu
Nyerere aliamini na kusema ya kuwa “tumefanikiwa kuwaondoa Wakoloni na hivyo
tupo huru. Na uhuru maana yake ni kazi”. Mwisho wa kunukuu.
Hapa Mwalimu Nyerere alikuwa na maana ili
tuweze kupiga hatua kimaendeleo ni lazima tuutumie huu uhuru wetu
vilivyo katika kupiga hatua kimaendeleo kupitia kufanya kazi kwa
bidii na maarifa yetu yote ili kuleta maboresho ya kina katika Nyanja zote zile
za kimaisha yaani uchumi, kijamii na kisiasa. Bila ya kufanya kazi kwa
bidii, uhuru wetu ni sawa na mzoga.
Na ndio maana Mwalimu Nyerere kama kiongozi
alianza kwa kuonyesha mfano wa dhahiri wa kuanzisha mapambano kwa vitendo dhidi
ya maadui zetu watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.
Sehemu kubwa ya mafanikio yake yalitokana
ama ni kupitia kuanzisha maazimio, mashirika, kauli mbiu na sera mbalimbali.
Hayo yote aliyafanya kwa vitendo zaidi na si porojo, lawama, maandamano, wala
manung’uniko.
Pia Mwalimu Nyerere alikuwa na falsafa ama
dhana ya kimaendeleo ambapo aliamini maendeleo sahihi hayawezi yakapatikana nje
ya uwepo wa mambo makuu manne ambayo ni “watu”, “ardhi”, “siasa safi”
na “uongozi bora”.
Naam!! “Watu” ni kiungo kimoja wapo
kikuu cha hakikisho la maendeleo chanya yeyote yale ndani ya familia, jamii ama
Taifa kwa ujumla wake. Mathalani, endapo tutakuwa na miundombinu bora ni watu
ndio wamechangia uwepo wake; ama kama tutakuwa na mazao ya kutosha kwa ajili ya
chakula, biashara na kiada basi ujue ni watu wameweka jitihada za
kutosha.
Halikadhalika kama kuna amani na utulivu
nchini basi ujue ni watu wamechangia hilo. Jamani, hata Wahenga
walisema: “usione vyaelea, ujue vimeundwa”, na waundaji wenyewe ni Wananchi
(mimi, wewe na Yule).
Licha ya uwepo wa utajiri wa nguvu kazi takribani
Watu Milioni 50 lakini bado watu hao hao ndani ya jamii wanachojua wao ni utegemezi
pekee. Kivipi?
Kwa jinsi tuanavyoishi utadhani tunawangojea
baadhi ya watu kutoka nje ya nchi ili waje watuletee maendeleo kwetu yaani
imefika kipindi kwa mtu hata kutandika kitanda chake mwenyewe anacholalia
imekuwa ni kazi kubwa kwake.
Kuna kipindi ulitolewa utafiti uliofanywa na
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) uliobaini asilimia 71 ya Watanzania wanatumia
muda mwingi kufanya shughuli zisizokuwa za uzalishaji mali wala tija kwa Taifa
hasa za kufanya starehe mbalimbali.
Hii ni hatari sana na inaonyesha
namna gani baadhi ya Watanzania tusivyojitambua. Kikubwa ambacho
kinaonekana ni kujikita mizizi ya dhana nzima ya kibaguzi
iliyojengeka akilini ama kwenye mitazamo ya watu ambapo tumediriki kuwaachia
viongozi pekee huku tukijiengua katika kapu la dhana ya neno “serikali” wakati
kiuhalisia na kimaantiki na Wananchi nao pia ni sehemu ya Serikali.
Ni kweli kabisa kwamba Serikali ni chombo
cha utawala kilichoshika dola ama nchi kwa lengo la kuwaletea maendeleo
Wananchi. Na wanaoiwezesha ama kuipa mamlaka hayo Serikali ni Wananchi.
Bila ya watu hakuna serikali na pia Serikali haina uhalali wa kuwepo bila ya
kuwepo kwa watu.
Na kundi lingine linalounda Serikali ni viongozi.
Hivyo Serikali ni muunganiko kati ya viongozi na Wananchi. Daima na
tena ni dhambi kubwa sana kuwatenganisha makundi haya (Wananchi na
viongozi) katika chungu hiki Serikali.
Wananchi siku hizi wamekuwa washadidiaji
wakubwa wa siasa na bila ya wao kujitambua ya kwamba hutumia muda mwingi sana
kushindia na kulalia katika dimbwi la porojo za kisiasa bila ya kujibidiisha.
Maendeleo yatapatikanaje bila ya sisi wenyewe kujishughulisha?
Utakuta vijana walio wengi kutwa wanashinda
kwenye kucheza “pool table” na kukaa vijiweni tu; Wazee ama akina Baba nao
kutwa wanacheza “bao” ama “draft” tu; na akina Mama nao kila kukicha wapo
vibarazani wakisutana na kupashana umbea tu. Hayo ndio maisha ya kila siku ya
baadhi ya wanajamii ya kutokupenda kufanya kazi kwa bidii.
Mwananchi huyo huyo anaitegemea Serikali ije
impatie fedha mikononi bila ya yeye kujishughulisha kwa kufanya kazi yeyote
ile ya kumpa kipato. Hakuna Serikali yeyote ile duniani inayoweza kuwapatia
wananchi wake pesa lukuki bila ya wao kujishughulisha.
Kama hauamini, jaribu kufanya utafiti katika
nchi zilizoendelea utakubaliana nami kuwa hakuna Taifa lolote lile lenye raia
wasiojibidiisha kwa kutegemea mteremko kutoka kwa Serikali zao. Yatazame
mataifa kama ya Marekani, Uingereza, China au Urusi wakazi wake wanavyotambua
ya kuwa thamani ya pesa yao na uchumi wa nchi unategemea zaidi ni kwa
jinsi gani watu wa ndani (wao wenyewe) wanavyozalisha mali.
Lakini sie hatujitambui na tupo bize kwa
kujiteketeza na porojo kila uchwao. Hapa tumesaliti Mwalimu Nyerere na
alivyoamini maana ya uhurukuwa ni kufanya kazi kwa
bidii, umasikini hautatuacha kweli? Nani wa kulaumiwa ni serikali na
viongozi wake ama ni sisi Wananchi?
Hii yote inatokana na jamii kuziasi mitazamo
miongozo na falsafa za Mwalimu Nyerere (mathalani ile ya “Uhuru ni kazi”)
hali inayosababisha kiwango cha idadi ya watu maskini kuzidi kukua nchini licha
ya kujaariwa rasilimali na mali za asili kwa kuyachakachua maendeleo yetu
wenyewe. Kisa? Porojo kutawala maisha yetu.
Tusiishie kuwalaumu tu Viongozi wetu kila
kukicha huku tukisahau jinsi sisi tulivyo wavivu sana wa kupindukia. Watanzania
tulio wengi hatupendi kufanya kazi kwa bidii na kwa ubunifu.
Watanzania tulio wengi hatupendi njia nyoofu na sahihi badala yake tunapenda
njia ya mkato ya kujipatia vipato vyetu. Watanzania wengi tunapenda sana
kufanya madili, ama “michongo” kama wanavyoita watoto wa mjini.
Kwenye salam zao ama maongezi mengi ya
Watanzania ni nadra sana kukosa kusikia maneno kama vile “mambo
mengine niaje, ishu vipi ama madili yakoje”. Ni dhahiri kuwa hapa
inatafutwa njia ya mkato ya mafanikio katika maisha. Hali hii huzaa matokeo
endelevu mabovu ndani ya jamii kama vile utapeli; ujambazi; ongezeko la
mihadarati na madawa ya kulevya; mauaji ya maalbino na vikongwe; pamoja na
uchafu ama uozo mwingine kadha wa kadha unaofanana na huo.
Chanzo haswa cha uwepo wa utafutaji mambo kwa
njia ya mkato halijasababishwa na Viongozi ndani ya Serikali bali msingi wake
mkuu niWatu tulio wengi kutaka matokeo chanya yenye faida na matunda kwa
haraka na hata pia kukata tama ya kimaisha kwa haraka zaidi kutokana na
kujinyima fursa ya uvumilivu na ustahimilifu ndani yetu.
Mapambano ya maisha ni sawa na vita
kali ambapo si tu jukumu la viongozi bali hata nasi Wananchi tuna wajibu mkubwa
wa kufanya kazi kwa bidii na si kulalama tu kila kukicha.
Kuna usemi mmoja unaosema “Wanaofanikiwa
zaidi ni wale walioshindwa mara nyingi” Je utashindwaje, kama
hujajaribu mara nyingi? Je mafanikio katika maisha yanapatikana kwa mara moja
tu? Haya ni maswali muhimu na ya msingi sana kwa Watanzania,
kujiuliza.
Ifike mahali tujitambue ya kwamba kelele,
tuhuma, lawama, dharau kwa viongozi wetu hazitatusaidia endapo sisi kwa sisi
hatujaamua kujibidisha ipasavyo. Utakuta ndani ya jamii fulani tupo zaidi ya
watu laki mbili lakini tunamtegemea kiongozi mmoja tu awe ni Mbunge
ama Diwani ili aweze kutuletea maendeleo. Endapo sisi tulio wengi tumeshindwa
kuwa kitu kimoja wenye nia moja ya umoja, mshikamano na tukaamua kwa dhati
kujiletea maendeleo; Je, kiongozi mmoja pekee atawezaje?
Ndugu zangu, kwanini alaumiwe dobi kutakasa
kaniki wakati tunajua rangi ya kaniki? Ni lazima tutambue ya kwamba
sisi raia pia tunahusika vilivyo na huu umaskini wetu na si vyema kuwasukumizia
mzigo wote wa lawama viongozi wetu pekee. Watanzania tulio wengi tunapoteza
muda mwingi kwa kukaa vijiweni, kushabikia siasa tu, kupiga soga na kucheza bao
muda wote. Je, tukiamua kujishughulisha kwa kuutumia muda huo ipasavyo
tungekuwa wapi kimaendeleo hivi sasa?
Waswahili walisema usimuhadithie mtu ndoto
yako uliyoota jana usiku lakini hapa ni kinyume kwani siri tunasema
na bayana tunaambizana.
Binafsi huwa Napata ukakasi pindi nionapo Serikali ina
sera na majukumu lukuki lakini Watanzania tulio wengi hatushiriki vyema na hata
hatutimizi wajibu wetu kwa wakati. Mwenye jukumu la kulifuatilia Taifa letu kwa
ukaribu na utendaji ni serikali pekee ama na Wananchi pia? Je, kwa
uwajibikaji huu, maisha bora kwa kila Mtanzania yatapatikana kweli?
Mara nyingi sera tulizonazo zinategemea zaidi
umoja, mshikamano, ushirikiano na nia ya dhati ya uwajibikaji wa pamoja
kiutekelezwaji. Kamwe maisha bora kwa kila Mtanzania hayaji kwa kuota au kupiga
soga ama kwa kungojea mpaka uone Tanzania (nchi yako) imekufanyia nini na badala
yake ujiulize wewe mwenyewe umeifanyia nini Tanzania?
Kuna wanamapinduzi, wanaharakati na watu
mashuhuri wengi tu hapa Duniani ambao hawakungoja mpaka waone nchi zao
zimewafanyia nini na badala yake walijiuliza wamezifanyia nini nchi zao?
Mwalimu Julius Nyerere, Nelson Mandela, Martin
Luther King Jnr, Kwame Nkurumah, Chifu Mkwawa ni baadhi tu ya
Wanaharakati na wakombozi wa kweli dhidi ya Uhuru na ubaguzi wa ngozi
nyeusi ambao milele na milele watabakia kuwa ni mashujaa maarufu wa
ulimwengu. Jiulize mwenyewe wewe je utakumbukwa, ama tutajivunia nini kutoka
kwako? Je, ni kwa huo ugoigoi wako ama kwa uwajibikaji wako?
Tuache uvivu na tujitume vilivyo kwa
kuchangamkia fursa na Baraka tulizojaaliwa. Mungu ametujaalia wingi wa ardhi
yenye rutuba ifaayo kwa kilimo, misitu, wanyama pori na vyanzo vingi vya
kujiletea maendeleo.
Hata kama Rais John Pombe Magufuli ni mzuri
kiasi gani hatoweza kuleta maendeleo tarajiwa kwa Watu endapo sisi wenyewe
Watanzania (Watu) hatutafanya kazi kwa bidii na badala yake tutasikia
uchumi wa Taifa umekuwa lakini pato binafsi la Mtanzania likiendelea kushuka.
Dawa ya kukuza mapato binafsi ni kwa kufanya kazi kwa bidii
kwa kuzichangamkia fursa za kiuchumi tulizojaaliwa.
Tanzania isiyo na maradhi inawezekana;
Tanzania yenye uchumi imara mpaka kwa Wananchi wake inawezekana; Tanzania yenye
huduma bora zaidi za kijamii inawezekana; Hakika Tanzania yenye maisha bora
zaidi pia inawezekana. Hii itawezekana tu endapo kila mmoja wetu atatimiza
wajibu ipasavyo kwake na kwa Taifa lake. Tuache kulalamika tu, tuanze kuchukua
hatua ya kujituma kutimiza wajibu wetu ipasavyo wa kufanya kazi kwa bidii.
0767488622
0 comments:
Post a Comment