Saturday, September 9, 2017

KAMPUNI YA BIMA YA BUMACO YAILIPA KAMPUNI YA BATCO MAMILIONI



Na Binagi Media Group
Kampuni ya Bima ya BUMACO imeilipa kampuni ya mabasi ya BATCO inayofanya safari zake katika ya mikoa ya Mara na Mwanza, kiasi cha shilingi Milioni 140 ikiwa ni malipo ya bima baada ya basi la kampuni hiyo kupata ajali ya moto.

Halfa ya kukabidhi hundi ya fedha hizo imefanyika leo kwenye ofisi za kampuni ya Bumaco zilizopo Jijini Mwanza, na kushuhudiwa na wageni mbalimbali akiwemo Meneja wa Mamlaka ya Bima Kanda ya Ziwa ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Meneja wa kampuni ya Bumaco Kanda ya Ziwa, Godlisten Muro amesema kampuni hiyo imekuwa ikilipa madai ya bima kwa wakati, lengo ikiwa ni kuwanusuru wateja wake na majanga mbalimbali yanayowakabiri na hivyo kuwataka wananchi kuondoa dhana kwamba bima hazilipi.

Meneja wa Mamlaka ya Bima Kanda ya Ziwa, Sharif Ali Hamad ameipongeza kampuni ya bima Bumaco kwa namna inavyolipa kwa wakati fidia za wateja wake na hivyo kuwasihi wananchi wakiwemo wafanyabiashara kujiunga na mfumo wa bima ili kunufaika na fidia pindi wapatapo majanga.

“Basi la Batco lilipata ajali tarehe 10.06.2017 na leo tarehe 08.09.2017 wanalipwa fidia ya shilingi Milioni 140, ukiangalia tangu kupata ajali hadi kulipwa fidia ni kipindi cha miezi mitatu”. Amesema Hamad na kuongeza kwamba hatua hiyo inaonesha ni jinsi gani kampuni ya Bumaco inavyoshughulikia kwa haraka madai ya wateja wake.

Mkurugenzi wa kampuni ya mabasi ya Batco, Baya Kusanja Maragi amewasihi wafanyabiashara wenzake kujiunga na kampuni ya bima ya Bumaco kwani imekuwa ikimlipa kwa wakati madai yake ya bima, ambapo pia tarehe 14.02.2015 basi lake lilipata ajali na akalipwa madai yake ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
Meneja wa Mamlaka ya Bima Kanda ya Ziwa, Sharif Ali Hamad, akionyesha hundi halisi ya malipo kutoka kamouni ya bima ya Bumaco kwa ajili ya kampuni ya mabasi ya Batco ambayo basi lake liliungua moto mwezi wa sita mwaka huu.
Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Bumaco wakiteta jambo kwenye hafla hiyo ambapo kushoto ni Ayoub Richard na kulia ni Livinus Mberwa.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More