Thursday, September 7, 2017

DC KILOLO ABARIKI UJENZI WA KIWANDA CHAI WILAYANI KWAKE



MKUU wa wilaya ya Kilolo Asia Abdallah kwa kushirikiana na uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo amesafiri hadi Dar es Salaam akilenga kufufua upya jitihada za siku nyingi za kupata mwekezaji atakayejenga kiwanda kikubwa cha chai wilayani humo.

Katika safari hiyo, mkuu wa wilaya huyo aliambatana na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Aloyce Kwezi, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Valance Kihwaga na maafisa wengine wa wilaya hiyo ambao walikutana na Mkurugenzi wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Prof  Godius Kahyarara.

“Katika kuunga mkono kauli mbiu ya Rais Dk John Magufuli ya Tanzania ya Viwanda, hatutaki kuwa nyuma. Wiki iliyopita tulikuwa Dar es Salaam, tumekutana na uongozi wa NSSF na kujadiliana nao namna wanavyoweza kufadhili ukwekezaji katika shughuli hiyo,” alisema.

Akionesha matumaini ya mazungumzo na uongozi huo wa NSSF, Asia alisema maongezi na shirika hilo yanaendelea na kila hatua itakayokuwa ikipigwa, taarifa zake zitakuwa zikiwekwa kwa wananchi.


“Zinahitaji zaidi ya Sh Bilioni 4.5 kujenga kiwanda ambacho pia kitafufua kilimo cha chai wilayani kwetu; NSSF wamepokea ombi letu na wanalifanyia kazi, ahadi ikiwa ni kutupa majibu baada ya miezi sita. Tushirikiane kuomba Mungu ili mpango huu ufanikiwe kwasababu ni sehemu ya maendeleo ya Taifa,” alisema.

Mamlaka ya Chai Tanzania ilianzisha kilimo cha chai wilayani humo mwaka 1988 lakini kilikufa miaka michache baadaye kwasababu mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa fedha za uendeshaji, kiwanda, umeme na nyingine nyingi.

Taarifa ya hivikaribuni iliyotolewa na Kampuni ya Chai Kilolo inaonesha wilaya hiyo ina zaidi ya hekari 10,000 zinazofaa kwa kilimo cha chai.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Mwenyekiti wa kampuni hiyo , Valance Kihwaga inasema wanachi walioanza kukichangamkia kilimo hicho walikata tamaa kutokana na ukosefu wa soko.

Juhudi hizo za mkuu wa wilaya zimekuja ikiwa ni matokeo ya juhudi nyingi za awali za kufufua kilimo cha chai na kujenga kiwanda wilayani humo kukwama.

Februari 2012, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Profesa Peter Msolla aliwaambia wananchi wa jimbo hilo kwamba Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) na kampuni ya TKK ya Norway zilionesha nia ya kutoa Sh Bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha chai wilayani humo, nia ambayo hata hivyo haikuzaa matunda. 

Na Juni 2016 Kampuni ya kimataifa ya Café Direct yenye makao yake makuu nchini Uingereza ilijitokeza kuwekeza katika kilimo cha chai wilayani Kilolo, lakini baadaye iliingia mitini kwasababu ambazo hazikutajwa.

Viongozi walioiwakilisha kampuni hiyo, Penny Newman na Krishna Gopola walitembelea maeneo ya wilaya hiyo ambako chai ingelimwa na kiwanja walichoahidi kujenga kiwanda cha kisasa cha kusindika na kutengeneza chai.

Wakipongeza juhudi mpya za mkuu wa wilaya hiyo, baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo waliozungumza na mtandao huu walisema wanaomba Mungu mpango huo ufanikiwe kwa kuwa utatoa fursa kubwa ya ajira na utaongeza kasi ya maendeleo ya wilaya hiyo.

“Tumekuwa na kiu ya muda mrefu ya kujikita katika kilimo cha zao hili la biashara, kwa kipindi chote hicho jitihada za kufufua kilimo hicho na kujenga kiwanda zimekuwa hazifanikiwi. Labda sasa tutafanikiwa kwasababu ya mtazamo wa serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya Viwanda,” alisema mmoja wao, Clement Kayage huku akimpongeza DC huyo.

Kayage alisema Kilolo ikipata kiwanda hicho, wananchi wengi watatumia fursa hiyo kuingia katika kilimo cha zao la chai kwa kuwa watakuwa na uhakika wa soko hatua itakayopunguza umasikini miongoni mwao.

Naye Festo Mbilinyi aliwataka wana Kilolo kwa ujumla wao kuunga mkono jitihada za mkuu wa wilaya huyo na akawaomba wadau mbalimbali wenye uwezo kujitokeza kuwekeza katika sekta mbalimbali wilayani humo

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More