Tuesday, May 23, 2017

HATUA ZA KUFUATA BAADA YA KUACHWA NA NDEGE

Na Jumia Travel Tanzania

Ni jambo la kawaida kuachwa na usafiri kama vile basi, boti, treni au ndege licha ya kufanya maandalizi ya kutosha. Baadhi ya sababu zinazoweza kuchangia mtu mpaka kuachwa na usafiri ni kama vile foleni barabarani, ajali au usafiri kupata matatizo na kukosea muda wa kuwasili.

Hali ya kuachwa na usafiri ni ngumu sana kama haijawahi kukutokea kabla na hauna mbinu mbadala ya kukuwezesha kusafiri kama ulivyokukusudia. Zipo hatua kadhaa za kufuata pindi uchelewapo ndege ambazo Jumia Travel ingependa uzifahamu na kuzizingatia pindi utakapokumbwa na changamoto kama hii.

Wasiliana na shirika la ndege unalosafiri mara moja. Kitu cha kwanza kabisa baada ya kugundua kwamba utachelewa au umechelewa ndege ambayo ulitakiwa kusafiri nayo ni kuwasiliana na shirika husika. Mara nyingi mawasiliano huwemo kwenye tiketi au tovuti ya shirika. Kwa kufanya hivyo utajua ni msaada gani wanaweza kukupatia kulingana na hali uliyopo.

Kuwa makini na sheria na masharti ya tiketi uliyokata. Kila shirika la ndege linakuwa na taratibu za uendeshaji wa safari zake. Zipo ambazo zinawasafirisha na ndege nyingine wateja wao waliochelewa, zingine siku inayofuata kama hamna kwa siku hiyo na zingine kutoza malipo ya ziada kwa kuchelewa ndege. Kwa hiyo kabla ya kukata tiketi ulizia taarifa hizo au soma kwenye tiketi yako kama zipo. 

Usihamaki/usiwe na hofu. Wewe sio wa kwanza kuachwa na ndege hali hiyo ishawakuta watu wengi hivyo vuta pumzi na tuliza akili yako ili ujue nini cha kufanya. Usipohamaki utaweza kupata suluhu ya tatizo haraka sana kama vile kuulizia cha kufanya, kuahirisha au kutafuta uwanja wa ndege ulio karibu ili usafiri na kuwahi shughuli zako kama ulivyopanga. Kwani kama kuchelewa umekwisha chelewa hakuna cha kufanya kutokana na hali hiyo.
Ulizia kwa wafanyakazi wa kampuni husika ya ndege machaguo uliyonayo. Kama umeshindwa kupata mawasiliano au haujui taratibu za shirika la ndege ulilokatia tiketi ya kusafiri basi ni vema ukauliza. Mashirika mengi yanakuwa na ofisi kwenye viwanja vya ndege au kama hawana basi ulizia wafanyakazi wa pale naamini wao wana uzoefu mkubwa wanaoweza kukupatia.

Lipia gharama za ziada baada ya kukosa ndege kama ulishafika tayari. Kama unaona kwamba utachelewa shughuli zako huko uendako basi huna budi kuongeza pesa kidogo ili uweze kusafiri na ndege inayofuata. Hii itakuwa nafuu zaidi kuliko kukata tiketi upya au kuahirisha safari. Kwa hiyo ni vema pia kuwa na fedha au chanzo za ziada pindi unapokuwa unasafiri kwani chochote kinaweza kutokea.

Tazama kama kuna ndege zingine zinazoelekea mahali uendapo. Kwa kawaida kwenye viwanja vya ndege vingi kunakuwa na ubao unaoonyesha ndege za mashirika tofauti zinazokwenda sehemu mbalimbali kwa siku hiyo. Hivyo inaweza kuwa fursa kwako kwa kufanya maamuzi ya kukata tiketi ili kuwahi shughuli zako.

Tumia muda huo kufanya mambo mengine. Kuchelewa safari haimaanisha kwamba ndiyo mwisho wa maisha. Kwa mfano upo Arusha na umechelewa ndege ya kukurudisha Dar es Salaam kwa siku hiyo, unaweza kuamua kutembelea vivutio kadhaa vilivyopo karibu na eneo hilo kama vile hifadhi ya Serengeti au Ngorongoro au hata Mlima Kilimanjaro. 
Ifahamishe hoteli utakayofikia mapema. Mara nyingine huwa tunafikia kwenye hoteli kwa mahali tunapoelekea labda uwe unarudi nyumbani. Kwa hiyo nina uhakika utakuwa umelipia hoteli wakuhifadhie chumba au kuomba usafiri wa kuja kukuchukua uwanja wa ndege. Ifahamishe hoteli utakayofikia mapema kwamba utachelewa au utafika siku inayuofuata ili kuondoa usumbufu kwao na kulipishwa gharama za ziada.

Jifunze kutokana na makosa yako. Kufanya makosa ni sehemu ya kujifunza mambo mengi maisha yetu. Hivyo basi hakikisha kwamba baada ya kuchelewa safari hii utakuwa makini zaidi wakati mwingine. Kama ulichelewa kwa sababu ya usafiri basi hakikisha unatoka mapema zaidi, kama ni ulikosea kuangalia muda basi muombe mtu wa karibu yako akukumbushe. 
Sababu ni nyingi ni zingine haziwezei kuzuilika kwa upande wa abiria na hata kwa shirika la ndege. Kuna wakati mwingine unaweza kuchelewa ndege kutokana na sababu za kiufundi za shirika lenyewe. Mara nyingi kwa sababu kama hizo abiria huwa wanafidiwa na mashirika ya ndege. Lakini kama ni sababu zako binafsi, Jumia Travel inakuasa kwamba uwe makini kwani utaishia kupoteza muda, kuvuruga mipango yako na kuingia gharama za ziada usizozitarajia.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More