Tuesday, May 23, 2017

DC MUFINDI ASISITIZA MPANGO WA CHAKULA CHA MCHANA KWA WANAFUNZI.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Jamhuri William anahutubia
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Jamhuri William akimvisha zawadi ya Begi mmoja kat ya Wanafunzi wa darasa la kwanza  waliofanya vizuri kwenye stadi za kuandika ,kusoma na kuhesabu

Na Ofisa Habari Mufindi

Serikali Wilayani Mufindi Imewataka wajumbe wa kamati za Shule na viongozi wa Serikali za vijiji kwa kushirikiana na wazazi, kutekeleza mpango wa utoaji chakula cha mchana kwa wanafunzi wanapokua shuleni kwa lengo la kuongeza ufanisi wakati wa kujifunza na kuleta matokeo chanya.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mh. Jamhuri William, wakati wa maadhimisho ya siku ya kusoma ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi iliyofanyika Kata ya Nyololo Wilayani humo.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema, mpango wa utoaji wa chakula Shuleni ambao wazazi hutakiwa kuchangia kwa mujibu wa sera ya  Elimu pasipo malipo, husaidia kuleta usawa kati ya walionacho na wasionacho, kuimarisha mahudhurio na kutunza muda wa ratiba za shule na kusisitiza kuwa endapo mambo haya yote yatafanyika kiusahihi yanamchango mkubwa wakati wa ujifunzaji ulio bora kwa wanafunzi darasani.

Maadhimisho ya siku ya kusoma katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi yanalengo la kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji wa stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu (K. k. k) huku yakiambatana na maonyesho ya Elimu na utoaji zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye kuandika, kusoma na kuhesabu.

Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imekua miongoni mwa Halmashauri ambazo shule zake zinafanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kwani mapema mwaka jana Halmashauri ya Mufindi ilishika nafasi ya sita (06) kwenye mitihani ya darasani la nne (04) kati ya Halmashauri (185) pia mwaka (2014) iliweka rekodi ya kukumbukwa ambapo shule yake ya kata ya Igowele iliongoza  kitaifa kwa kushika nafasi ya kwanza kwenye mtihani wa kidato cha sita (06)

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More