Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Helen Kijo- Bisimba (katikati), Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Uwajibikaji, Imelda Urio (kulia) na Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga , wakionesha jarida la kupinga adhabu ya kifo wakati wa uzindi wake Dar es Salaam leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Helen Kijo- Bisimba (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, wakati akisoma tamko la kupinga adhabu ya kifo. Kulia ni Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Uwajibikaji, Imelda Urio na kushoto ni Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga.
Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Uwajibikaji, Imelda Urio (kulia), akisisitiza jambo kwenye mkutano huo.
Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga akizungumza katika mkutano huo.
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.
Na Dotto Mwaibale
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimefungua kesi ya kikatiba kuhusiana na ulinzi wa haki ya kuishi na urekebishwaji wa sheria ya kanuni ya adhabu juu ya ulazima wa kutolewa kwa adhabu ya kifo katika makosa ya uhaini na mauaji.
Kesi hiyo imefunguliwa dhidi ya mwanasheria mkuu wa serikali wakitaka ufafanuzi zaidi juu ya adhabu ya kifo, wakibainisha kuwa adhabu hiyo haimpi nafasi mtuhumiwa kujirekebisha bali ni ya kulipiza kisasi.
Kituo hicho kimesema endapo Tanzania itatekeleza hukumu ya kifo kwa sasa inamaanisha watu wapatao 228 na zaidi watapoteza maisha yao huku wengine 244 wanasubiria maamuzi ya rufaa zao.
Akizungumza wakati akitoa tamko la kupinga adhabu ya kifo Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Hellen- Kijo Bisimba alisema hadi mwaka 2015 jumla ya watu 472 walikuwa wamehukumiwa kunyongwa.
Alisema kituo kinaiomba serikali kurekebisha sheria ya kanuni ya adhabu na sheria ya ugaidi yenye kutoa adhabu ya kifo kwa makosa ya mauaji, uhaini na ugaidi.
Dk. Bisimba alisema kituo kina sababu za kupinga adhabu hiyo ya kifo na hawafurahii watu kuua wengine na ndio maana hawapendi pia hata muuaji auawe.
“Adhabu ya kifo ni vigumu kuhakikisha kuwainatekelezwa tu kwa wale watu ambao huwezi kuirekebisha kwani mfumo wa utoaji haki huwa pia na mianya ya makosa na hivyo maisha ya mtu yanaweza kupotea bure,” alisema Dk. Bisimba na kuongeza kuwa hakuna ushahidi wowote kuwa adhabu hiyo inaweza kuzuia watu wengine kutokutenda makosa kama hayo.
Alisema licha ya adhabu hiyo kutokutekelezwa nchini kwa takriban miaka 22 , taaarifa zinaonesha kuwa watu 72 ambao walishawahi kunyongwa kutokana na adhabu hiyo.
Hata hivyo aliiomba serikali kutengeneza utaratibu wa kuelimisha jamii juu ya kuheshimu haki za binadamu hususani haki zakuishi na kuweka mazingira ya kuiheshimu haki hiyo, pia ibadilishe sheria kwa kuondoa adhabu ya kifo na kuweka adhabu mbadala kwenye makosa ya jinai na kwa wafungwa waliopo mfano vya muda mrefu gerezani.
0 comments:
Post a Comment