Mhe. Naibu Waziri Dkt Hamisi Kigwangalla (MB) – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Mhe. Ndugu Onesmo Buswelu, Mkuu wa Wilaya (SIHA)
Dr Said Egwaga, Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong'oto
Dr Best Magoma, Mganga Mkuu wa Mkoa.
Bwana Saimon Msuya, Katibu wa Mkoa (TUGHE)
Wadau wa Maendeleo (WHO, USAID, CDC-EGPAF, KNCV) mliopo hapa
Viongozi kutoka KCMC, Chuo Kikuu cha Nelson Mandela na CEDHA
Mwenyekiti wa CCM (Wilaya) na viongozi wote wa chama Tawala na Serikali
Viongozi wa vyama vya upinzani
Wageni waalikwa
Wanahabari
Mabibi na Mabwana
Mhe. Mgeni Rasmi,
Awali
ya yote kwa niaba ya Wafanyakazi wa Taasisi ya Magonjwa ya Kuambukiza
ya Kibong'oto napenda kukukaribisha wewe pamoja na wageni wote mliopo
hapa katika viwanja hivi vya Taasisi. Tunashukuru sana kwa kutenga muda
wako adhimu kukubali na kuhudhuria hafla hii muhimu kwa Taifa letu na
safari ya kuboresha sekta ya Afya nchini.
Tunakupongeza
kwa dhati kwa juhudi zako ambazo zinaonekana wazi tangu ulipokabidhiwa
Wizara hiikwa kubuni njia mbali mbali ambazo zimeendelea kuboresha
utoaji wa huduma za Afya nchini likiwemo suala la uhakiki ubora wa vituo
vya kutolea huduma za afya nchini. Hongera sana
UTANGULIZI:
Hospitali
Maalumu ya Taifa ya kutibu Magonjwa ya Kuambukiza ya Kibong'oto (zamani
Hospitali ya Taifa ya Kifua Kikuu Kibong'oto) ilianzishwa mwaka 1926 na
Dr Norman Davis (Mwingereza) ikiwa ni Kituo cha kutunza wagonjwa -
waliogunduliwa kuwa na Kifua Kikuu (Sanatorium) wakati dunia ilikuwa
bado haina dawa za kutibu vimelea vinavyosababisha Kifua Kikuu. Mwaka
1952 hospitali ilizinduliwa rasmi kama kituo cha kutibu Kifua Kikuu
nchini Tanganyika pamoja na nchi zingine za Afrika Mashariki, Somalia,
Eritrea na Ethiopia.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Mwaka
2009 Hospitali ilipewa hadhi ya kuwa Kituo Bora cha utoaji wa Huduma za
Kifua Kikuu Sugu nchini – yaani “Center of Excellence for Management of
Drug Resistant TB in Tanzania” ikiwa na jukumu la kutibu wagonjwa wote
wanaogunduliwa na kifua kikuu sugu kitaifa.
Tarehe 12 Novemba
2010, Serikali ilitangaza rasmi kupitia tangazo la Gazeti la Serikali
namba.828 kuwa Kibong'oto imekuwa Hospitali Maalumu ya Taifa ya Kutibu
Magonjwa ya Kuambukiza (Super specialized Infectious Diseases Hospital –
Kibong'oto). Aidha hospitali ilikamilisha mpango Mkakati wa wa muda
mfupi na mrefu mwaka 2013 kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la
Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID).
Mhe. Mgeni Rasmi,
Kuanzia
Mwaka 2013, Hospitali ilianza kutekeleza malengo yaliyomo kwenye mpango
mkakati wa Hospitali. Juhudi kubwa imeelekekezwa kutekeleza lengo
linalohusu kuimarisha utawala bora katika hospitali kwa kuimarisha
mifumo ya uendeshaji wa Hospitali ikiwemo kuunda upya mfumo wa utawala
(organizational structure), kuanzishwa Bodi ya Udhamini, Kamati za
Uendeshaji (Executive Management Committee), Kamati ya ukaguzi wa ndani
(Internal Audit committee), vitengo mbalimbali kama vile kudhibiti
ubora, usimamizi shirikishi, mifumo ya taarifa na kitengo cha
mwanasheria wa taasisi.
Aidha, katika kipindi
hicho, Hospitali kwa kushirikiana na Wizara na wadau wengine iliandaa
andiko la kusaidia kupata mchakato wa Kisheria wa kuanzishwa kwa Taasisi
hii. Tuna imani kuwa andiko hilo litakamilika katika siku za karibuni.
Napenda
kuchukua nafasi hii kukushukuru Mgeni Rasmi kwa kuwa leo hii
utakamilisha na kuhitimisha moja ya nguzo muhimu katika maendeleo na
ustawi wa Taasisi yetu ambayo ni utawala bora “Good governance” kwa
kuzindua rasmi Bodi ya Udhamini.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Nichukue
nafasi hii kukuarifu kuwa, utekelezaji wa malengo mengine yaliyomo
katika mpango mkakati unaendelea katika ngazi tofauti zinazoridhisha.
Lengo
namba moja linaeleza kuwa “Taasisi ya Magonjwa ya Kuambukiza itaendelea
kuchangia katika juhudi za taifa za kuboresha tiba kwa magonjwa ya
kuambukiza kama vile Kifua Kikuu Sugu, UKIMWI na magonjwa mengine.
Kuanzia mwaka 2009 hospitali imetibu wagonjwa zaidi ya 582 wa Kifua
Kikuu Sugu kati yao asilimia 40 wakiwa na maambukizi ya UKIMWI.
Matibabu yao kwa sasa yanaanza ndani ya masaa 24. Matibabu yanachukua
miezi 18 – 24. Tunafurahi kukutaarifu kuwa asilimia 75 ya wagonjwa hawa
wanatibiwa na kupona kabisa kiwango ambacho ni juu ya kiwango cha
asilimia 70 kichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Mpango wa kati
ni kufupisha tiba kutoka miezi 18 – 24 na kuwa miezi 9 – 11 huku
wataalam wakiendelea kusimamia tiba hiyo ili kuhakikisha matokeo mazuri
yanapatikana.
Mhe.Mgeni Rasmi,
Lengo
la pili ni kuongeza ushiriki wa jamii katika mapambano dhidi ya
magonjwa ya kuambukiza kwa kuiongezea uelewa, kuzuia unyanyapaa pamoja
na kuimarisha masuala yanayohusu jinsia. Baada ya kubaini ongezeko la
TB katika mazingira hatarishi hasa katika mgodi wa uchimbaji madini ya
Tanzanite – Mererani, Hospitali ilianzisha huduma za vikoba kwa kutumia
idara ya Afya ya Jamii kuelimisha wachimbaji wadogo wadogo wa Tanzanite.
Mpaka sasa wachimbaji wadogo wadogo zaidi ya 2,000 wameechunguzwa afya
zao. Kati ya hao asilimia 4.5 wamekutwa na maambukizi ya TB na
walipatiwa matibabu. Aidha hospitali imeshiriki katika mazungumzo kati
ya wamiliki wa migodi pamoja na wizara ya Nishati na Madini ili
kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kutumia maji kwenye mashimo ili
kuzuia vumbi inayowaathiri wachimbaji na kuathiri mapafu
(Pneumoconiosis).
Mhe. Mgeni Rasmi,
Lengo la tatu la
Mpango Mkakati wa Hospitali ni kujenga uwezo wa watumishi kutoa huduma
za hali ya juu za tiba kwa wagonjwa pamoja na kuwafuatilia wale wote
waliopo kwenye tiba. Serikali imeongeza idadi ya watumishi kwa kuajiri
na mpaka sasa watumishi waliopo ni 253; Miongoni mwao Madaktari wapo
15, mmoja ana shahada ya uzamivu katika eneo la magonjwa ya kuambukiza,5
wana shahada za uzamili katika utaalam mbalimbali, 3 wanaendelea na
masomo ya uzamili katika taaluma mbalimbali (Microbiologia, Mionzi na
magonjwa ya ndani). Pia tuna wauguzi 67, kumi kati yao ni maafisa
wauguzi, Wafamasia wawili, Wataalam wa maabara ni 12, sita kati yao ni
wataalamu wa teknologia maabara (Lab scientists), Makatibu wa Afya 2,
wahasibu 3, Afisa manunuzi 2 na wengineo.
Mhe. Mgeni rasmi,
Lengo
la nne ni kuanzisha kituo cha mafunzo cha kutibu magonjwa ya kuambukiza
katika ngazi ya uzamili (Post graduate courses) na fellowship programu.
Kwa kuanza, tumetoa mafunzo kwa watumishi zaidi ya 1,000 kutoka
hospitali mbalimbali nchini juu ya tiba sahihi ya Kifua Kikuu Sugu.
Lengo ni kuwawezesha kusimamia tiba ya kifua kikuu sugu kwa wagonjwa
wanaotoka hospitali ya Kibong'oto.
Pia kuna mazungumzo
yanaendelea baina yaChuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson
Mandela ili Hospitali iwe kituo cha mafunzo kwa wanafunzi wa shahada ya
uzamili katika sayansi ya magonjwa ya binadamu.
Aidha
tulianzisha mafunzo ya muda mfupi ya Mawasiliano Bora kwa wagonjwa na
watumishi wa Afya “Health Communication skills” kwa kuwajengea uwezo wa
kuwasiliana vizuri na wagonjwa ili kuimarisha mahusiano na ufuasi wa
dawa za Kifua Kikuu Sugu ambayo tiba ni ya muda mrefu
Matokeo ya hili lengo ni kuwa na wataalamu bingwa katika Nyanja ya magonjwa ya Kuambukiza
Mhe. Mgeni Rasmi,
Lengo
la tano ni kuanzisha kituo cha utafiti wa magonjwa ya kuambukiza
Kibong'oto. Hospitali –ikishirikiana na wadau kama NIMR, KCMC, Chuo
Kikuu cha Virginia (USA) na Shirika la Afya Duniani kitengo cha utafiti
magonjwa ya nchi joto (WHO – TDR kufanya tafiti mbalimbali zenye
kuimarisha utambuzi wa magonjwa ya TB na magonjwa mengine ya kuambukiza.
Aidha kuna machapisho ya kisayansi yamefanyika kutokana na tafiti hizi.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Lengo
la sita ni kuendeleza Hospitali ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong'oto
kuwa Taasisi Bora katika kutibu magonjwa ya Kuambukiza na kufanya iwe ya
mfano nchini.
Katika lengo hili hospitali imeendelea kutoa
ushauri kwa vituo vilivyogatua huduma hizi na kuvifanyia usimamizi
shirikishi katika mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia
Hospitali imeendekea kufanya vikao vya robo mwaka kwa wataalam wa Tiba
ya Kifua Kikuu Sugu ili kujua ufanisi wa tiba baada ya wagonjwa
kuruhusiwa, lengo likiwa ni kuendelea kufuatilia ubora wa huduma
zinazotolewa kwa kuzingatia viwango na miongozo ya Taifa. Hospitali
inashirikiana na vituo hivi kutatua changamoto zinazowakabili watoa
huduma.
Pamoja na huduma za moja kwa moja,
Hospitali imeendelea kusambaza dawa za za kifua kikuu sugu kwa wagonjwa
wote ambao wanaendelea na matibabu katika vituo vya tiba nchi nzima.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Lengo
la saba la mpango mkakati ni kuanzisha na kuboresha mifumo ya utawa
bora katika Hospitali hii likiwa na shabaha ya kuifanya taasisi. Uwepo
wa Bodi ya Wadhamini, mfumo wa utawala wa Taasisi pamoja na usimamizi wa
kazi zinazotekelezwa lilishakamilika kwa kuandika nyaraka mbali mbali.
Lengo hili limekamilika kwa ushirikiano mkubwa sana na wadau wa
Kimaendeleo USAID. Leo hii tunajivunia kuzindua Bodi ya Hospitali.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Lengo
la nane la mpango mkakati ni kuboresha miundo mbinu ya majengo ili
kuwezesha shughuli za Tiba, Mafunzo pamoja na tafiti ziweze kufanikiwa.
Katika lengo hili tunaishukuru Serikali kwa kufanya uwekezaji mkubwa
katika kuboresha majengo kuanzia mwaka 2004. Mwaka 2010, kazi
ziliongezeka katika Hospitali na kusababisha wao kufanya utafiti na
kujua uhitaji mkubwa uliopo wa majengo.
Majengo
haya yanajumuisha upanuzi wa maabara iwe ya kisasa kwa ajili ya ugunduzi
wa magonjwa ya kuambukiza na kufuatilia mwenendo wa magonjwa, Hosteli
kwa wanafunzi wa fellowship, Kumbi za mikutano na sehemu za kufundishia
(Resource center) pamoja na nyumba za watumishi.
Mipango
yetu ni kuendelea kutafuta njia mbadala ya kuingia ubia na mashirika
kama vile Shirika la Nyumba la Taifa, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na
mengine ili kuweza kujenga majengo ambayo yatafanyiwa tathmini ya
uwekezaji (RETURN ON INVESTMENT).
Andiko
(business plan) limeshafikishwa kwa mchumi wa Wizara ili afanye tathmini
ya kichumi juu ya suala la uwekezaji katika majengo.
Mhe. Mgeni Rasmi,
Lengo la tisa ni Kutafuta vyanzo vya fedha ambavyo ndiyo vitakavyotumika kufanikisha malengo mengine nane.
Vyanzo
vikubwa vya raslimali fedha katika Hospitali hii ni Serikali (fedha za
uendeshaji, miradi ya maendeleo, fedha ya uchangiaji huduma za afya),
Wadau wa maendeleo (Mfuko wa Dunia , East Africa Public Health
Laboratory Network Project , Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali
Norway – LHL International, CDC, USAID pamoja na WHO – TDR).
Kwa
kipindi chote, hospitali imekuwa ikitegemea fedha ya uendeshaji wa
Hospitali kutoka Serikali Kuu ambapo kwa miaka minne mfululizo fedha
hizi zimekuwa hazitoshi kuendesha shughuli za Hospitali hata kutishia
wadau wa maendeleo kutokuamini kuwa fedha wanayotoa inaweza kutumika
kufanya shughuli nyingine tofauti na malengo halisi yaliyowekwa. Pamoja
na mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya muda mfupi wa kutekeleza
Mpango Mkakati wa Taasisi ambao umezingatia Mpango Mkakati wa tatu na
sasa wa nne wa Wizara, Matokeo makubwa sasa na Sera nyingine za Wizara,
bado tuna changamoto mbalimbali ambazo tunaamini kwa kushirikiana na
Bodi ya Hospitali tutaendelea kupunguza na hatimaye kuondoka kabisa.
Nazo ni:
Madeni mbali mbali ya watumishi na wazabuni waliotoa huduma kuanzia mwaka 2010 mpaka Juni 2016 yanafikia Bilioni 1.068
Upatikanaji wa sheria ya kuanzisha Taasisi
Masuala
yanayohusu maslahi ya watumishi kama vile upandishwaji vyeo,
malimbikizo ya mishahara pamoja na ubadilishwaji wa kada za watumishi
waliojiendeleza
Kuhuishwa kwa muundo wa Taasisi
Mhe.
Mgeni Rasmi napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kukubali mwaliko
wetu wa kuja kuzindua Bodi ya Hospitali ya Magonjwa Ambukizi
Kibong'oto.
Tumefarijika sana.
Imeandaliwa na Uongozi wa Hospitali na kusomwa kwenu na
Dkt. Riziki Michael Kisonga
KAIMU MGANGA MKUU
HOSPITALI YA MAGONJWA YA KUAMBUKIZA KIBONG'OTO
0 comments:
Post a Comment