Mkurugenzi wa mawasiliano wa taasisi ya
Mfuko wa Wanawake Afrika, Anna Salado (kulia), akipakua mboga zilizopikwa
kiasili na kuungwa kwa nazi wakati yeye na ujumbe wake walipotembelea mradi wa
ukaushaji wa mboga na matunda wa wanawake wa Kata ya Mzinga mkoani Morogoro
hivi karibuni. Kushoto
ni Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Milikieli Mansweat Mahiku.
Mratibu wa mradi wa Green Voices kutoka
taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika ya Hispania, Alicia Cebada, akiwa
ameshikilia pakiti ya kisamvu kilichokaushwa na kufungashwa huku akiwapongeza
wanawake wa kikundi cha Mzinga katika Kata ya Mzinga, Manispaa ya Morogoro
kwamba wamefanya kazi nzuri sana. Mwenye fulana nyeupe ni Bi. Esther Muffui,
mshiriki kiongozi wa mradi huo.
SIYO tu mapishi ya
asili ya kisamvu kikavu kilichoungwa kwa nazi, lakini mafanikio makubwa katika
ukaushaji na usindikaji wa mboga na matunda katika mradi wa wanawake wa Kata ya
Mzinga, Manispaa ya Morogoro yamewavutia wahisani wa taasisi ya Women for
Africa Foundation kutoka Hispania.
Hali hiyo imewafanya
wanawake hao wawe katika nafasi kubwa zaidi ya kusonga mbele ikiwa wafadhili
hao watatoa tena fedha katika awamu ya pili ya mradi wa Green Voices unaotekelezwa
nchini Tanzania.
Akizungumza katika
Kijiji cha Konga kwenye Kata hiyo, mratibu wa mradi huo kutoka Hispania, Bi.
Alicia Cebada, alisema kwamba licha ya kuwa na muda mfupi tangu kuanza kwa
mradi huo, lakini wanawake hao wamefanya mambo makubwa ambayo yanastahili
kuungwa mkono.
“Hii teknolojia ya
ukaushaji wa mboga na matunda ni rahisi na inafaa sana kwa uhifadhi wa chakula,
kinachotakiwa ni kwa wanawake hawa kuwezeshwa zaidi,” alisema Alicia ambaye
aliongozana na Mkurugenzi wa habari wa taasisi hiyo, Anna Salado, na ofisa
mwandamizi wa taasisi hiyo anayeshughulikia masuaa ya ubunifu, Bi Noellia pamoja na mratibu wa Green Voices Tanzania,
Bi. Secelela Balisidya.
Alicia alisema kwamba,
changamoto ndogo wanazokabiliana nazo wamezisikia, lakini akasema katu
zisiwakatishe tamaa kwa sababu inaonyesha dhahiri wanaweza kufanya mambo
makubwa mbele ya safari.
Maofisa wa taasisi ya Mfuko wa Wanawake
Afrika kutoka Hispania wakiwa katika picha ya pamoja na wanakikundi wa Mzinga
(wenye sare). Kulia
ni mratibu wa mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela
Balisidya.
Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro,
Milikieli Mansweat Mahiku (wa nne kutoka kulia), akiwa katika picha ya pamoja
na maofisa wa Mfuko wa Wanawake Afrika na washiriki wa mradi wa Green Voices
Tanzania.
Taasisi ya Women for
Africa Foundation mbayo ni Mfuko unaoshughulikia maendeleo ya Wanawake wa
Afrika, ikiongozwa na makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa
Fernandez de la Vega Sanz, ndiyo inayofadhili mradi wa Green Voices ambao
unatekelezwa Tanzania pekee.
Hata hivyo, taasisi
hiyo inafadhili miradi 15 ya wanawake katika nchi 12 barani Afrika ambayo
imeonyesha mafanikio, huku mradi wa Green Voices ukitajwa kuwa na mafanikio
makubwa katika kipindi kifupi.
Miongoni mwa
changamoto ambazo wanawake hawa wasindikaji wanakabiliana nazo ni pamoja na makaushio ya
umeme-jua (solar power) pamoja na
masoko ya uhakika na vifaa vya kufungashia.
Mshiriki kiongozi wa
mradi huo wa Mzinga Green Voices, Esther Muffui, alisema kwamba kaushio
walilonalo kwa sasa ni dogo kuliko mali ghafi zilizopo na akaongeza kwamba
itakuwa vyema kama walau kutakuwa na kaushio moja kwa kila wanawake watatu.
“Hapa Mzinga wanawake
na jamii nzima wanalima mboga mboga na matunda kwa wingi, lakini kaushio
tulilonalo ni moja tu ambapo haliwezi kutosheleza mahitaji, kama tutawezeshwa zaidi
na walau kukawepo kaushio moja kwa kila wanawake watatu itasaidia sana hata
jamii nzima ya hapa,” alisema.
Ujumbe huo
ulifurahishwa zaidi baada ya kupata mlo wa mboga kavu zilizoungwa kwa nazi na
karanga pamoja na wali wa nazi, ambapo siyo tu walishangazwa na mapishi hayo ya
asili, bali pia walistaajabu namna ukaushaji huo usivyoathiri ubora wa mboga hizo.
Mratibu wa mradi wa Green Voices kutoka
Hispania, Alicia Cebada, akiuliza jambo kuhusu namna ya ukaushaji wa matunda.
Mshiriki kiongozi wa kikundi cha Mzinga
Women Group, Esther Muffui (wa pili kushoto), akitoa maelezo ya namna ya
kukausha matunda katika mradi wa Green Voices kwenye Kata ya Mzinga mjini
Morogoro.
Naibu Mstahiki Meya wa
Manispaa ya Morogoro, Milikieli Mansweat Mahiku, alisema kwamba, atahakikisha
anasimamia kwa bidii ili teknolojia hiyo iweze kusambaa kwa wanawake wote wa
manispaa hiyo, ambayo inafahamika kwa uzalishaji wa mboga na matunda kwa wingi.
Mhe. Mahiku, ambaye
pia ni Diwani wa Kata ya Mzinga, alisema kwamba, kuanzishwa kwa mradi huo
kutawachochea wanawake wengi kuingia kwenye ujasiriamali wa kilimo cha mboga
mboga na matunda, kwa kuwa sasa hayawezi kupotea kama zamani.
Aidha, aliahidi kwamba,
yeye na madiwani wenzake watahakikisha asilimia 10 ya fedha za maendeleo katika
halmashauri wanapatiwa wanawake na vijana wanaofanya miradi endelevu yenye tija
na inayolenga kutunza mazingira kama wanavyofanya wanawake hao wa Mzinga.
“Sasa hivi bajeti ya
maendeleo ya halmashauri imeongezwa hadi asilimia 60, sasa kati ya fedha hizo,
asilimia 10 ni miradi ya wanawake na vijana, ambayo kama tutaisimamia vyema na
kuielekeza kwenye miradi endelevu kama hii italeta tija.
“Kama wahisani hawa
wamejitokeza na wamekuja kutoka Hispania, sisi kama serikali nasi tunapaswa
kuunga mkono jitihada hizi ambazo zina tija kubwa,” alisema Mstahiki Meya.
Hata hivyo, aliitaka
jamii kubuni miradi mbalimbali endelevu na kuacha kuisubiri serikali ifanye
kila kitu.
Mradi huo wa ukaushaji
wa mboga na matunda umeanzishwa mwezi Machi mwaka huu baada ya Bi. Esther na
wanawake wengine 14 kupatiwa mafunzo nchini Hispania ya ujasiriamali unaoendana
na utunzaji wa mazingira na uelewa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Miradi mingine inayotekelezwa
kupitia Green Voices Tanzania ni kilimo cha viazi lishe Ukerewe, usindikaji wa
mihogo Kisarawe, ufugaji nyuki Kisarawe, utengenezaji wa majiko banifu
Mkuranga, kilimo cha matunda Uvinza – Kigoma, kilimo cha uyoga Boko na Bunju,
Dar es Salaam, kilimo hai cha mboga mboga Kinyerezi, Dar es Salaam, ufugaji
nyuki Dakawa, Morogoro, na utengenezaji wa majiko ya umeme-jua Kilimanjaro.
Bi. Esther Muffui, mshiriki kiongozi wa
kikundi cha Mzinga Women Group mjini Morogoro kinachotekeleza mradi wa Green
Voices kwa ukaushaji wa mboga na matunda, akieleza jambo wakati ujumbe kutoka
taasisi ya Mfuko wa Wanawake Afrika ulipotembelea mradi huo hivi karibuni.
Matayarisho
ya mboga mbichi kabla ya kuikausha.
Hapa sasa mboga inasambazwa tayari kwa
kuwekwa kwenye kaushio.
Na walipatiwa zawadi maalum kwa ukumbusho. Hapa Alicia Cebada akivishwa skafu yenye rangi za bendera
ya Tanzania.
Maofisa wa Mfuko wa Wanawake Afrika, Alicia
na Anna Salado wakiserebuka katika ngoma ya Kirugulu.
0 comments:
Post a Comment