Wednesday, October 19, 2016

UNESCO YASAINI MIKATABA NA SERIKALI YENYE THAMANI YA DOLA MILIONI SABA KWA AJILI YA KUSAIDIA ELIMU

Katika kusaidia kuboresha elimu nchini, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limesaini mikataba miwili na serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliyo na lengo la kusaidia elimu nchini.

Mkataba wa kwanza unahusu mradi unaofahamika kama 'Empowering Adolescent Girls and Young Woman through Education' mradi ambao umedhaminiwa na Shirika la Misaada la Korea (KOICA) kwa kiasi cha pesa cha Dola Milioni tano (5,000,000), mradi ambao unataraji kufanyika katika wilaya ya Ngorongoro, Sengerema, Kasulu na Micheweni, Pemba.

Mkataba wa pili unahusu mradi wa 'XPRIZE - Promotion of Early Learning Through the use of Innovative Technologies' ambao umedhaminiwa na UNESCO kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula (WFP) kwa kiasi cha pesa cha Dola Milioni mbili (2,000,000) ambapo utahusisha watu wa miaka 15-18 ambao hawapo shuleni kutoka Arusha na Tanga ambapo watapatiwa tablet ambazo zitakuwa na programu tumishi za kujifunza.

Akizungumza wakati wa kusaini mikataba hiyo, Mkuu wa ofisi na Mwakilishi wa UNESCO, Zulmira Rodrigues alisema mipango ya UNESCO ni kuona inawasaidia watoto ambao hawasomi licha ya kuwa na umri wa kuwa shuleni wakipata nafasi ya kusoma ili kupunguza idadi ya watoto ambao hawapo shuleni duniani ambapo takwimu zinaonyesha wanazidi Milioni 263.
Mkuu wa ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues akizungumza kuhusu mradi wa Empowering Adolescent Girls and Young Woman through Education na XPRIZE - Promotion of Early Learning Through the use of Innovative Technologies.

"Tunaandika histori leo sio kwa Tanzania bali dunia nzima, maana makubaliano yataleta ushirikiano kati ya WFP, UNESCO na Wizara ya Elimu kuwasaidia watoto zaidi ya Milioni 263 ambao hawapo shuleni duniani na kutumia nafasi ya teknolojia kutafuta suluhisho la kuwasaidia watoto hawa,

"Tunaishukuru Wizara ya Elimu kwa kutuamini, nawashukuru WFP kwa kuwa pamoja nasi na kwa washirika wengine ambao wamekubali kuungana nasi kwa ajili ya kufanikisha hili," alisema Rodrigues.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Maimuna Tarish alisema msaada huo utaweza kusaidia kuboresha elimu nchini hasa katika kipindi hiki ambacho serikali inajipanga kutoa elimu kisasa kwa kutumia njia za kidigitali na hivyo ni mwanzo mzuri kwa mfumo ambao wanajipanga kuanza kuutumia.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Maimuna Tarish akitoa neno la shukrani kwa niaba ya serikali.

"Kwa niaba ya serikali ya Tanzania tunashukuru kwa msaada wenu kwa kuwa tayari kusaidia elimu ya Tanzania kwa kutumia teknolojia, tunataka kutoa elimu kwa njia ya kidigitali na nyie mmekuwa tayari kutusaidia tunawashukuru,

"Madhumuni makubwa ni kutaka kuboresha elimu na tukaona ni vyema kushirikiana na mashirika mengine ili kuwasiadia watoto kupata elimu bora kwa kufuata zile njia tatu, Kusoma, Kuandika na Kuhesabu, shuleni atafundishwa na akirudi nyumbani anaweza jifunza kusoma kwa kutumia tablet," alisema

Kwa upande wa Mwakilishi wa WFP nchini, Michael Dunford alisema WFP imekuwa ikishirikiana na serikali ya Tanzania katika maeneo mbalimbali hivyo kuwa sehemu ya kusaidia elimu nchini ni jambo kubwa na lengo lao ni kuona teknolojia inakuwa na faida kusaidia elimu kukua.

Mwakilishi wa WFP nchini, Michael Dunford akielezea jinsi WFP imeguswa hata kufikia hatua ya kuwa tayari kushirikiana na UNESCO kufanya mradi wa XPRIZE.

"WFP na Wizara ya Elimu wamekuwa wakishirikina kwa muda mrefu na hata UNESCO tunataka kutumia teknoloji kusaidia elimu, kuona jinsi gani teknoloji itatumika madarasani na WFP tayari ina watu ambao watasimamia kuhakikisha jambo hili linafanikiwa," alisema Dunford.

Nae Mkurugenzi wa KOICA nchini, Joonsung Park alisema mradi huo ni sehemu ya miradi ambayo KOICA imepanga kuifanya kwa ajili ya kusaidia kukuza elimu katika nchi ambazo zinaendelea.

Afisa Mradi wa Elimu wa UNESCO, Faith Shayo akieleza jinsi miradi hiyo itakavyofanya kazi.
Mkurugenzi wa KOICA nchini, Joonsung Park akizungumza kuhusu mradi ambao wamedhamini ambao pamoja na una lengo la kusaidia elimu na zaidi kwa wasichana.

"Huu ni moja ya miradi mitatu ambayo KOICA imekubaliana na UN kwa ajili ya kuifanya na kusaidia elimu, tumekuwa tukishirikiana na UNFPA, UNWOMAN, UNV katika kufanikisha hilo na matarajio yetu ni kuwa ushirikiano wetu uzidi kudumu na kuleta matokeo mazuri," alisema Park.
Mkuu wa ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Maimuna Tarish wakisaini mkataba wa mradi wa XPRIZE.

Mkuu wa ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira Rodrigues na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Maimuna Tarish wakisaini mkataba wa mradi wa Empowering Adolescent Girls and Young Woman through Education.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More