Monday, April 23, 2018

WATAKA SHERIA YA WATIA MIMBA WANAFUNZI IONGEZWE MENO

Na: Amina Hezron,  Morogoro

Wito umetolewa kwa serikali kuhakikisha wanawadhibiti na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika wamebaka au kuwapa mimba wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari nchini.

Baadhi ya wadau wa Elimu Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya mkutano huo.
 Wakizungumza kwa nyakati tofauti wadau wa elimu wilaya ya mvomero mkoani Morogoro wakati wa mkutano ulioandaliwa na mtandao wa elimu Tanzania TEN /MET ili kupeana mrejesho wa namna ya kukabiliana na changamoto za mimba za utotoni kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari.


Katika mkutano huo wa wadau  wamebaini ushiriki wa karibu wa wazazi na watoto wao haupo kwa kiasi kikubwa jambo linaloelekea kuendelea kuwepo kwa changamoto hiyo.


Kwa upande wake afisa elimu wa wilaya hiyo Bi. Maajabu Nkamyemka amesema kwa wilaya ya mvomero takwimu zinaonesha hadi April 6 mwaka huu takribani mimba 90 zimebainika kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambapo miongoni mwa hizo mimba 13 ni kutoka shule za msingi.

Aidha Bi. Nkamyemka amesema kuwa ni jukumu la wazazi na walimu kwa kushirikiana na wanafunzi kuhakikisha wanawafichua wale wote ambao ni wahusika bila kuwafumbia macho ili sekta husika kupambana nao ili kutokomeza janga hilo.

"kwa kuwa binti akipewa ujauzito huwa tunahangaika tu na aliyempa ujauzito, na yule mwenye ujauzito tunamuacha sasa bhas sasa kwa kuwa wazazi hawataki kuleta ushirikiano tutamfungulia kesi mwanafunzi mwenye mimba pamoja na wazazi ili wazaz wawachunge watoto wao ipasavyo "Alisema Nkamyemka.
Wadau hao wa elimu wakiwa ndani ya mkutano huo 
Naye mratibu elimu wa kata za mhonda na Kweuma bwn, Heriamini Mariki amesema kuwa kumekuwa na changamoto ya mimba hasa kwa wanafunzi, wa sekondari jambo ambalo kwa kiasi kikubwa wazazi ndiyo chanzo cha tatizo hilo huku akitaja sababu zinazochangia kuwa ni pamoja na uelewa finyu wa wazazi na wakati mwingine umaskini kwa baadhi ya kaya nyingi wilayani humo.

 “Sisi kama wadau wajibu wetu mkubwa ni kuwapatia elimu wazazi juu ya athari za kutokaa karibu na watoto wao na kuwa wawazi juu ya madhara ya kufanya ngono wakiwa na umri mdogo" alisema Mariki

Naye diwani wa kata ya mhonda Bw. Abdallah Hassani Khalifa ametoa rai kwa Serikali kujenga hosteli kwa shule za kata ili kuondokana na tatizo la mimba za utotoni linaloikumba nchi nzima kwa kiasi kikubwa, huku akiwataka wazazi na walimu wanawapa  watoto wanafunzi ushirikiano wa kutosha na ulinzi kwani ndiyo haki pekee wanaotakiwa kuzipata ili kufanya vyema katika masomo yao.


0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More