Katika kusaidia Tanzania kuwa moja ya nchi ambazo wananchi wake wana lishe salama, Umoja wa Ulaya (EU) umechangia Euro milioni 9.5 (Tsh. 22 Bilioni) kwa ajili ya kusaidia kutekelezwa kwa mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula unaotekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wenye thamani ya Euro milioni 24.5 (Tsh. 57.7 bilioni) unaotarajiwa kufanyika katika mikoa ya kanda ya kati.
Akizungumza kuhusu msaada huo, Mkuu wa Ubalozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Roeland Van De Geer alisema EU imeamua kusaidia jamii ya Tanzania kupata lishe bora kwani wao wanaamini kuwa pasipo lishe bora mambo mengi ambayo yanahusu maendeleo ya taifa hayawezi kufanyika kwa kasi ambayo yanatakiwa kwenda nayo lakini pia mpango wa kusaidia lishe salama ni moja ya mambo ambayo EU imepanga kusaidia.
Mkuu wa Ubalozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Roeland Van De Geer akizungumza kuhusu mchango wa Euro milioni 9.5 (Tsh. 22 Bilioni) kwa ajili ya kusaidia kutekelezwa kwa mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP). (Picha zote na Rabi Hume)
“Kupitia mradi huu EU pamoja na WFP ziko katika nafasi nzuri ya kubaini na kuunga mkono uhusiano katika kilimo, afya, usalama wa chakula na lishe ambao hapo kabla haukuwa umeelezwa kwa kina na kufuatiliwa kikamilifu, matumaini yetu ni kuwa viongozi na wananchi kwa pamoja wataungana kufanikisha mradi huu,” alisema Van De Geer.
Nae Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Michael Dunford aliishukuru EU kwa kutoa msaada ambao utawezesha jamii ya Tanzania katika mikoa wa Dodoma na Singida kusaidiwa kupata lishe salama ikiwa ni sehemu ya Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGs).
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Michael Dunford akizungumza kuhusu mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula.
“Tunashukuru kwa mchango huu kutoka Umoja wa Ulaya kwani umeiwezesha WFP kuendelea na programu hii bunifu inayolenga kukidhi mahitaji ya watu walio hatarini zaidi na hasa watoto katika kipindi cha ukuaji wao” alisema Dunford.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya alisema mradi huo utafanyika kwa mikoa miwili ya Dodoma na Singida ambapo takwimu za kudumaa kitaifa ni aslimia 34 na Dodoma ni asilimia 34 na Singida ni 36.5 na utafanyika kwa miaka mitano.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya akielezea jinsi mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula utakavyofanyika nchini, takwimu za kudumaa na mikoa ambayo utafanyika.
Aidha Dk. Ulisubisya alisema uwekezaji huo wa WFP utahusisha kuwapa chakula, kutoa elimu jinsi ya kuzalisha vyakula vya aina mbalimbali, kuwawezesha kuwa na wanyama, jinsi ya kuwa na mazao ya kuuza na walengwa wakubwa ni kina mama wajawazito na watoto.
Mkuu wa Ubalozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Roeland Van De Geer na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Michael Dunford wakisaini makubaliano ya Umoja wa Ulaya (EU) kutoa mchango wa Euro milioni 9.5 (Tsh. 22 Bilioni) kwa ajili ya kusaidia kutekelezwa kwa mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula.
0 comments:
Post a Comment