Thursday, February 23, 2017

MAITI ISIYOJULIKANA YAKUTWA MTO RUAHA WAKATI WA KUTAFUTA MAITI MBILI ZA WANAFUNZI WA SHULE YA MSIGI MAPINDUZI

Maiti  ya  mtu  asiyejulikana  ikipelekwa  kuhifadhiwa  chumba cha maiti  Hospitali ya  mkoa  wa Iringa


Mkuu  wa  wilaya ya  Iringa  Richard Kasesela  akijiandaa  kusaidia kushusha maiti ya mtu  asiyefahamika aliyoopolewa  mto Ruaha  Iringa  leo
Mkuu wa wilaya ya  Iringa  Richard  kasesela  kulia  akisaidia kushusha maiti ya mtu asiyefahamika  aliyoopolewa  mto Ruaha  leo  wakati wa zoezi la  kutafuta  miili ya  wanafunzi wawili wa shule ya Msingi Mapinduzi wal;iozama maji toka jumamosi  iliyopita
JITIHADA  za  kuwatafuta   wanafunzi    wawili wa shule ya  Mapinduzi  katika Manispaa ya  Iringa  walikufa maji  jumamosi ya  wiki  iliyopita zimeendelea  kugonga mwamba baada ya  kuitafuta  miili  ya  watoto  hao kwa  zaidi ya  siku tano  pasipo mafanikio .

 Imeelezwa  kuwa  wanafunzi hao  walikuwa sita  wakiogelea  katika mto  Ruaha  eneo la  Isakalilo siku ya  jumamosi na mmoja kati  yao alizidiwa na maji   hayo na  mmoja  wapo  alijitosa katika  maji  kwa ajili ya  kumuokoa  mwezake na  ndipo  wote  wawili  walizama na kufa maji .

Akitoa taarifa ya tukio  hilo kwa   mkuu  wa  wilaya ya  Iringa Richard kasesela na mbunge wa  viti maalum mkoa  wa Iringa  Ritta kabati   waliofika  kushirikiana na  wananchi wa kata ya  Isakalilo na Mwangata  kutafuta  miili ya  watoto hao jana  ,mwenyekiti  wa mtaa wa  Kohondombi  A  Jumanne Ngasakwa  alisema  kuwa  jitihada za  kutafuta  miili ya  watoto hao  zilianza toka  siku ya  jumamosi kwa  kushirikiana na  kikosi cha  zimamoto na uokoaji  mkoa  wa Iringa .

Mwenyekiti huyo  alisema  watoto hao  waliokufa maji ni  wanafunzi wa darasa la saba katika  shule ya  msingi Mapinduzi ambao  majina yao ni  Somado Chuma na May Angaime  na  kuwa  wenzao  wanne  waliosalimika katika  tukio  hilo walitoweka na hadi  sasa majina  yao hayafahamiki .

Alisema  kuwa  kumekuwepo na tabia ya  watoto hao  kufika katika  eneo hilo la mto  Ruaha  kuogelea na  wakifukuzwa  na  wananchi  wanaofanya  shughuli za  kilimo katika  maeneo hayo  huwa  wanawatolea  lugha  chafu  na  kuwa  siku ya  tukio  hilo kuna mama mmoja  alikuwa  akilima maeneo hayo na alipojaribu  kuwafukuza  walimshambulia kwa  lugha  chafu  na kumtishia kumpiga mawe  jambo  lililopelekea  mama  huyo  kuwakimbia  watoto hao .


Akitoa  pole kwa  wananchi hao  mbunge Kabati  alisema  kuwa  ni vema  kuweka utaratibu  wa  kuwazuia  watoto hao  kuongelea katika  mto  huo kwani  hili  si tukio la kwanza  kutokea kwenye mto huo kwa  watoto kufa maji .

Pia  alisema   kutokana na  jitihada za utafutaji wa miili ya watoto  hao  kuwa ngumu ni  vizuri  kikosi cha  Zima moto na uokoaji  kuwa na vifaa vya kuzamia katika  maji kuliko kufika  eneo  hilo  bila  kuwa na vifaa vya  kisasa kama mtungi wa   hewa na  vifaa vingine .

" Kuna  haja  ya  suala la  vitendea  kazi za  zimamoto na uopkoaji  serikali  kulifanyia kazi kwa  haraka kwani majanga  ya  watu  kufa maji katika  mto  ruaha na maeneo mengine ya  mkoa  wa Iringa ni  mengi hivyo  nitakwenda  kulisemea  bungeni  jambo  hilo "

Mstahiki  meya wa Manispaa ya  Iringa Alex  Kimbe  alisema  kuwa wanaangalia  uwezekano wa  kupiga marufuku  watoto  kuogelea katika  mto  huo Ruaha  ili  kuepusha  majanga  kama hayo  .

Japo  aliwataka  wazazi  wote wa Manispaa ya  Iringa  kuwaonya  watoto  wao kwenda  kucheza katika mto  huo  Ruaha  ambao maji  yake ni mengi na ni hatari kwa  usalama  wao .

Mkuu  wa  wilaya ya  Iringa  Kasesela  alisema  wilaya  yake  imepata  majanga  makubwa mawili  kwa siku  moja  hiyo ya  jumamosi kuwa  mbali ya  tukio  hilo la  watoto kuzama maji  pia wanafunzi  wengine   wawili wa shule ya msingi Mibikimitali   walipoteza maisha kwa  kupigwa na radi  wakiwa  nje ya nyumba vya madarasa .

Hata   hivyo  mkuu huyo  wa  wilaya  aliwapongeza wananchi  wa kata ya  Isakalilo na Mwangata  ambao  wameendelea  kujitolea  kuitafuta  miili ya  watoto hao toka  siku ya  tukio hadi  jana  na  kuwataka  kuendelea  kuisaka  miili  hiyo  ambayo kimsingi ilipaswa  kuibuka baada ya  siku ya tatu  ila hadi  sasa ni  zaidi ya  siku  tano bado haijapatikana .

Alisema  tayari  amewaagiza  maofisa watendaji  wa maeneo mbali mbali ya wilaya ya  Iringa ambayo mto  huo  unapita  kuanza kuisaka miili ya watoto hao  ili kufanyiwa mazishi  .
 
Wakati  huo  huo  mkuu  wa  wilaya ya  Iringa  Richard kasesela  amewataka  wananchi ambao  wamepokelewa na  ndugu yao  wa  kiume  anayekadiliwa  kuwa na miaka  zaidi ya 30  kufika  katika  Hospitali ya  mkoa  wa Iringa  kutambua mwili  ambao  umeopolewa katika mto Ruaha  leo  wakati  wa zoezi la  kutafuta  miili ya  watoto wawili  waliozama maji .
 
Mwili huo  umekutwa na majeraha  na  inasadikika  kuwa kabla ya kutupwa kwenye maji aliuwawa  kwa  kipigo na  watu  wasiofahamika

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More