Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Helen Kijo-Bisimba (kulia), akizungumza na wanahabari Dar es Salaam leo, wakati akimkaribisha Mwanachama wa Kituo hicho, Ananilea Nkya (katikati) kuzungumzia utafiti wake alioufanya kuhusu namna vyombo vya habari vya Tanzania vinavyojishughulisha na maendeleo. Kushoto ni .Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga.
Mwanachama wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Ananilea Nkya (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi Dar es Salaam leo, juu ya utafiti alioufanya kuhusu namna vyombo vya habari Tanzania vinavyojishughulisha na maendeleo. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk.Helen Kijo-Bisimba na .Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga
Taarifa ya utafiti huo ikiendelea kutolewa.
Mwanahabari Hilda wa gazeti la Daily News akiwa mzigoni.
Maofisa wa LHRC wakifuatilia mkutano huo.
Na Dotto Mwaibale
UTAFITI uliofanywa na Mwanachama wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Ananilea Nkya, kama sehemu ya masomo yake ya Shahada ya Uzamivu (PhD), umebaini kuwa habari zinazotangazwa na vyombo vya habari hapa nchini hazichangii ipasavyo juhudi za taifa katika kutokomeza umaskini miongoni mwa wananchi walio wengi ambao wanaishi vijijini.
Utafiti huu umabainisha kuwa sababu kubwa ni kwamba habari zinazotangazwa na vyombo vya habari zinajikita zaidi katika matukio yanayotokea mijini, na wanaopatiwa fursa kubwa ya kutoa maoni ni wanaume ambao ni watumishi wa umma na wanasiasa.
Utafiti huu umehusisha habari 10,371 zilizotangazwa katika vyombo vya habari 15 katika muda wa mwezi mzima Febuari 2014.
Habari hizo zilitangazwa kwenye taarifa ya habari ya saa mbili usiku kwenye televisheni mbili na radio mbili za kitaifa na zilizochapishwa katika magazeti 11 ya kila siku. Utafiti ulilenga kupata majibu ya swali: Vyombo vya habari Tanzania vinaripoti masula gani ya maendeleo na kwa mtazamo wa watu gani? Kati ya habari 10,371 zilizofanyiwa utafiti 9,607 zilichapishwa magazetini.
Utafiti huu unaonesha kuwa kati ya habari 10,371 zilizochapishwa 4,750 (45.8%) zilitokea Dar es Salaam na 5,621 (54.2%) zilitoka mikoani na Zanzibar.
Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa kkoa wa Dar es Salaam ulinufaika zaidi kimaendeleo kwa sababu kama habari hizo 10,371 zingegawanywa kwa usawa kwa mikoa yote, kila mkoa ungepata fursa ya kutoa habari 368 kuhusu mambo mbali mbali yanayohusu maendeleo ya wananchi wake.
Habari hizo zingekuwa ni fursa ya mikoa kutangaza, ili kuhabarisha, kuelimisha na kuhamasisha wananchi kujadili changamoto na mafanikio ya maendeleo yao katika nyanja ya kijamii, kiuchumi na kisiasa
Kwa kufanya hivyo wadau wa maendeleo ikiwa ni pamoja na wanachi wenyewe, serikali kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa, mashirika ya kijamii (NGOs), taasisi za dini, taasisi za elimu, taasisi za fedha na wafadhili wa nje wanaochangia maendeleo ya nchi yetu wangechukua hatua sahihi na kwa wakati husika kushughulikia matatizo yanayosababisha wananchi wengi kuishi maisha ya kimaskini.
Hata hivyo badala ya vyombo vya habari vya kitaifa kuwa chachu ya maendeleo kwa kutangaza habari zinazoweza kuinua maendeleo kila mkoa, kila wilaya na kila kijiji, habari nyingi tena za kimatukio tu zisizofanyiwa uchunguzi zinaufanya mkoa wa Dar es Salaam kuchukua fursa 15 za maendeleo kupitia habari ambazo kila mkoa hapa nchini ungepata kila mwezi kujadili masuala ya maendeleo yanayohusu watu wake.
Masuala ya maendeleo yayosumbua wananchi wengi katika mikoa mingi hapa nchini ni pamoja na ukosefu wa ajira/kipato, ukosefu wa maji safi na salama, elimu bora, huduma bora ya afya, ukosefu wa umeme na barabara.
Aidha utafiti huu umebaini kuwa habari zinazotangazwa na vyombo vya habari vya kitaifa ziko zaidi katika mtazamo wa watumishi wa umma kwa sababu ndio wanaonukuliwa zaidi kwenye habari hizo.
Kati ya watu 14,637 walionukuliwa kwenye habari 10,371 zilizohusishwa kwenye utafiti, watu 8,398 (57.4%) walionukuliwa walikuwa ni watumishi wa umma, 1,945 (13.3%) ni wanasiasa 2,757 (18.8%) wawakilishi wa taasisi za kiraia na mashirika binafsi (CSOs) na wananchi wa kawaida walionukuliwa walikuwa 1,199 (10.5%).
Hata hivyo kwa vile kuzungumza kwenye vyombo vya habari ni fursa inayoweza kudidimiza au kuharakisha maendeleo, fursa hizo 14,637 zingegawanywa sawa kwa makundi yote--- wananchi, watumishi wa umma, wanasiasa, taasisi za kiraia na mashirika binafsi, kila kundi lingepata fursa 3,659 kuzungumza kupitia vyombo vya habari kuhusu masuala ya maendeleo.
Hivyo kwa mujibu wa utafiti huu maafisa wa umma walipata fursa mara tano zaidi kuliko wananchi wa kawaida kuzungunza kupitia habari zilizotangazwa na vyombo vya habari vya kitaifa.
Aidha walipata fursa mara nne zaidi kuliko wanasiasa na mara tatu kuliko wawakilishi wa taasisi za kiraia na mashirika binafsi.
Katika utafiti huu maafisa wa umma ni viongozi na watumishi wa serikali kuanzia ngazi ya kijiji/mtaa hadi taifa, mashirika ya umma, mashirika ya Umoja wa Mataifa yenye ofisi zake hapa nchini na maafisa katika balozi zenye ofisi zake Tanzania.
Wanasiasa ni wawakilishi kutoka vyama vya siasa. Taasisi za kiraia na mashirika binafsi inajumuisha vyama vya kitaaluma, vyama vya wafanyakazi, taasiasi za dini, mashirika binafsi, shule na vyuo binafsi na kundi la wananchi linajumuisha wanachi wa kawaida wanaume na wanawake.
Kadhalika utafiti unaonyesha kuwa habari zilizochapishwa na magazeti, kila habari kwa wastani ilinukuu mtu (chanzo cha habari) mmoja wakati kwa redio na televisheni, kwa wastani, kila habari ilinukuu si chini ya watu wawili.
Utafiti huo unaonyesha kuwa habari zinazotanganwa na vyombo vya habari vya kitaifa zinajihusisha zaidi na maendeleo ya wanasiasa kwa sababu habari zinazonukuu wanasiasa ndizo zinapewa umuhimu mkubwa zaidi katika vyombo vya habari.
Kati ya habari 411 zilizotangazwa kama habari Kuu (lead stories) katika vyombo hivyo 15 habari 234 (57%) zilikuwa za kisiasa, 121 (29%) zilijadili masuala ya kijamii na 56 (14%) uchumi. Hii ina maana kuwa vyombo vya habari haviyapi umuhimu masuala ya uchumi ambayo ndiyo yanafanya wananchi wengi kuwa maskini.
Kwa mfano utafiti unaonyesha kuwa kati ya habari kuu 411, habari 307 (74.7%) zilichapishwa kwenye magazeti magazetini 11 kama habari kuu. Hata hivyo kati ya habari hizo 307, habari zilizojadili masuala ya kijami mfano shule afya na umeme zilikuwa 67 (22%), uchumi ni 39 (12.5%) na 201 (65.5%) zilikuwa ni siasa.
Habari za siasa ziliandikwa kutokana na mikutano ya kisiasa, mahojiano na wanasiasa, kampeni za uchaguzi, taarifa za vyama vya siasa kwenye vyombo vya habari, makongamamo na washa za kisiasa.
Habari za uchumi ni zile zilizohusu masuala ya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, matumizi mabaya ya rasilimali za nchi, ukusanyaji kodi kupitia mashine za kieletroniki (EFD), kilimo, matatizo ya wakulima katika kupata pembejeo na masoko ya mazao yao, uchimbaji madini, utalii, viwanda, uwekezaji, matatizo ya ajira, mabadilisho ya fedha, biashara na ujasiriamali, uvuvi na misitu ikiwepo ukataji miti kupata magogo kwa ajili ya biashara ya mbao.
Habari za kijamii ni zile zilizojikita kwenye haki za binadamu, jinsia, mimba mashuleni, kuozesha kwa nguvu watoto wa kike, ukatili majumbani, biashara ya binadamu na migogoro ya ardhi.
Zilihusisha pia masuala ya elimu kama vile uhaba wa walimu, vitabu na madawati katika shule za umma (serikali), uhaba wa chakula, ajali za barabarani, miundo mbinu, masula ya kisheria, masuala ya dini, na habari za mahakamani.
Vyombo vya habari vya umma vya utangazaji vilivyohusishwa kwenye utafiti huu ni TBC 1 na TBC Taifa wakati vyombo vya habari vya watu binafsi ni pamoja na ITV na Radio One. Magazeti ya kila siku ya Kiswahili yalikuwa ni Nipashe, Mwananchi, Mtanzania, Majira, JamboLeo and Tanzania Daima. Na magazeti ya Kiingereza yalikuwa the Citizen na the Guardian na gazeti la serikali Daily News.
Utafiti unaonyesha pia kwamba habari zilizochapishwa katika vyombo vya habari vya Tanzania zilitawaliwa na mfumo dume ambapo kati ya watu 14,655 walionukuliwa katika taarifa 10,371 kwenye vyombo vya habari 15, wanawake walikuwa 2,646 (18%) na wanaume 12,009 (82%).
Utafiti unadhihirisha jinsi ambavyo maoni yanayohusu maendeleo yanayowasilishwa kupitia habari yanavyotawaliwa na wanaume.
Watu 14,637 walionukuliwa kwenye taarifa za habari walinufaika na nafasi ya vyombo vya habari kama fursa ya maendeleo kwa sababu waliweza kuwasilisha maono yao ambayo yalichagiza mipango ya maendeleo ya taifa .
Hii inadhihirisha kwamba hoja/maoni yaliyotolewa na watu hao 14, 637 yangehesabiwa kuwa fursa za maendeleo na kugawanywa kwa uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume kama makundi ya kijamii kila kundi lingepata fursa 7,318 ya kuzungumzia masuala ya maendeleo kwa mtazamo wao.
Hivyo basi kwa dhana kwamba idadi ya wanaume walionukuliwa katika taarifa za habari ni 82% na wanawake ni 18%, inamaanisha kwamba wanaume walikuwa na nafasi mara tano Zaidi ya wanawake katika kupata fursa kwenye vyombo vya habari kama sehemu ya kuwasilisha maoni yao ambayo yalichechemua mipango ya taifa ya maendeleo.
Hii inaonyesha jinsi ambavyo wanawake ambao ndio sehemu kubwa ya idadi ya watu nchini Tanzania wanakosa fursa. Utafiti huu umeonye wanawake wanakosa fursa mara tano ikilinganishwa na wanaum,e katika kuzungumza kwenye vyombo vya habari .
Utafiti huu unaonyesha kuwa masuala ya kimaendeleo yanayowagusa wanawake kama kundi kubwa katika jamii linalojumuisha zaidi ya 51% ya idadi ya watu nchini yameendelea kutokushughulikiwa. Kwa mfano , kutokana na hali hiyo wanawake walio katika umri wa kuzaa wameendelea kuhatarisha maisha kwa vifo ambavyo vingeweza kuzuilika wakati wa kujifungua.
Sambamba na hilo wanawake wengi wameendelea kutumia muda mwingi kutembea umbali mrefu wakitafuta maji na kuni kwa sababu ya kutokuwepo kwa mabomba ya maji na umeme. Na hivyo kudumaza uchumi wa faimilia zao na taifa.
Kwa upande wa magazeti kati ya watu 12,822 walionukuliwa 2371 (18.5%) walikuwa wanawake na 10,451 (81.5) walikuwa wanaume.
Hii inamaana kuwa taarifa za habari zilizochapishwa kwenye magazeti 11 ya kila siku, kwa wastani wanaume walikuwa na fursa mara nne zaidi kulinganisha na wanawake kutoa maoni yao juu ya masuala ya maendeleo.
Hata hivyo, gazeti la Daily News lilikuwa na 24% ya wanawake ambao maoni yao juu ya maendeleo yalipenyeza kwenye uwanda wa habari. Hii inamaanisha kwamba kupitia taarifa za habari za Daily News. Wanaume walikuwa na nafasi mara tatu Zaidi ya kujadili masuala ya kimaendeleo kuliko wanawake.
Katika upande mwingine, gazeti la Mtanzania na the Citizen uwakilishi wa wanawake ilikua 16%, na 16.2% kwa kila moja ambapo hii inaonyesha ni jinsi gani magazeti haya mawili yalimpa mwanaume nafasi mara tano Zaidi ya mwakamke katika kujipambanua katika masuala ya kimaendeleo.
Kadhalika utafiti unaonyesha kuwa habari zinaandikwa zaidi na wanaume . Utafiti unaonyesha kwamba wanahabari 8,094 walihusika katika ukusanyaji wa taarifa zilizotumika kuunda taarifa za habari 10,371 ambazo zilitolewa kwenye vyombo vya habari 15 vilivyofanyiwa utafiti katika utafiti huu. Miongoni mwa walioandika bahari hizo, wanahabari 3,039 (37.6%) walikuwa wanawake na 5,053 (62.4%) walikuwa wanaume.
Hii inaonyesha jinsi ambavyo waandishi wa kiume wanapata fursa karibu mara mbili ikilinganishwa na wanahabari wa kike katika kuandaa habari juu ya masuala ya maendeleo. Hii inatoa maana kwamba waandishi wanawake wamepoteza fursa kuandaa habari zinazohusu maendeleo ya nchi kwa mtazamo wa wanawake ambazo zingeweza kuibua masuala yanayoathiri wanawake katika maendeleo na kuweza kushughulikiwa.
0 comments:
Post a Comment