Friday, March 6, 2015

WANAJESHI WALIOHUKUMIWA KIFO WAKATA RUFAA

WANAJESHI wawili waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Swetu Fundikira ambaye ni mtoto wa ndugu wa marehemu Chifu Abdallah Fundikira, wamekata rufaa kupinga adhabu hiyo.

Wanajeshi hao ambao ni ndugu , MT 75854 Koplo Ally Ngumbe wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kikosi cha Kunduchi na MT 85067 Koplo Mohamed Rashid (JKT Mbweni), wamewasilisha rufaa hiyo katika Mahakama ya Rufani.

Katika rufaa yao, wanajeshi hao wana hoja tatu wakipinga hukumu ya kunyongwa hadi kufa iliyotolewa Novemba 20, 2012 na Jaji Zainab Mruke wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Katika hoja zao, wanajeshi hao wanadai Jaji alikosea kisheria kutoa uamuzi kwa kutozingatia kanuni za kuthibitisha mashitaka pasipo kuacha shaka yoyote, ambalo ni jukumu la upande wa mashitaka.
Aidha, wanadai Jaji alikosea kisheria kwa kutoa hukumu inayoegemea ushahidi wa kimazingira, bila kuzingatia ushahidi wa utetezi wa wakata rufaa. Katika hoja nyingine wanadai alishindwa kuchanganua itirafu katika majina kwenye taarifa ya uchunguzi wa chanzo cha kifo.
Awali, wakati hukumu hiyo inatolewa walihukumiwa washtakiwa watatu akiwemo aliyekuwa MT 1900 Sajenti Roda Robert wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kikosi cha Mbweni, ambaye alifariki dunia mwaka jana mkoani Dodoma wakati akisubiri utekelezwaji wa hukumu hiyo.

Katika hukumu hiyo, Jaji Zainab alisema upande wa mashitaka umethibitisha kesi yao bila shaka na hivyo Mahakama imeona kuwa washitakiwa wote wana hatia na walimuua marehemu Fundikira kwa kukusudia.

Hata hivyo, alisema hakuna shahidi aliyethibitisha kuwa aliwaona washitakiwa wanavyomuua Swetu, bali mashahidi watatu walithibitisha kuwaona washtakiwa wakiwa na Swetu kabla ya kukutwa na mauti.

Alisema anawatia hatiani washtakiwa na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa kwa kuwa ushahidi wa mazingira umeowanyooshea kidole washitakiwa kuwa wanahusika na mauaji hayo.
Ilidaiwa Januari 23 ,2010 katika eneo la Kinondoni, Dar es Salaam, washtakiwa hao walidaiwa kumuua marehemu Fundikira.

WALEMAVU IRINGA WALIA NA ALBINO

CHAMA cha watu wenye ulemavu, mkoani Iringa kimelaani vikali mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yanayoendelea nchini na kuitaka serikali kuandaa sheria kali itakayokomesha vitendo hivyo vya kikatili.
 
Mwenyekiti wa chama hicho manispaa ya Iringa, Haluna Mbilinyi alisema kwa miaka mingi sasa walemavu wa ngozi wamekuwa wakiishi kwa hofu kubwa ndani ya nchi yao kutokana na kuuawa, huku viungo vyao vikikatwa bila huruma.
 
Mbilinyi alisema lazima sheria kali ya kuwabana watu wanaofanya ukatili huo ianishwe ili iwe fundisho kwa wale wenye mawazo finnyu kwamba viungo vya binadamu vinaweza kuwasababishia utajiri.
 
“Wakiwamaliza walemavu wangozi wanaweza kuhamia kwa walemavu wa viungo, hii ni hatari sana kwa jamii kwa sababu walemavu wenzetu wanaishi kwa kukimbia kikmbia ndani ya nchi yao wenyewe,”alisema Mbilinyi.
 
Aidha aliitaka jamii kufichua waovu na waganga wa kienyeji ambao wamekuwa chanzo kikubwa cha mauaji ya ngozo kwenye jamii.

MSANII WA NYIMBO ZA INJILI, MKOANI IRINGA REHEMA CHAWE AACHIA ALBAMU YAKE YA GOSPEL



 

 Muimbaji wa Nyimbo za Injili Rehema Chawe




Muimbaji wa Nyimbo za Injili Rehema Chawe


MSANII wa nyimbo za Injili, nyanda za juu kusini Rehema Chawe ambaye ni Mwanachama wa chama cha Muziki wa Injili Tanzania (CHAMUITA), anatarajia kuzindua albamu yake ya kwanza, inayoitwa Kusamehe ni afya.

Uzinduzi huo unatarajia kufanyika Jumapili, March 8, mwaka katika kanisa la EAGT, Frelimo kwa mchungaji Mwenda, ambaye ni Mwenyekiti wa makanisa ya Kipentekoste mkoani Iringa.

Akizungumza na wanahabari, Chawe alisema uzinduzi huo utapambwa na waimbaji wengi toka nje na ndani ya mkoa wa Iringa.

Alisema mgeni rasmi katika uzinduzi huo atakuwa, ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Iringa, Enock Ugulumo.

Mwenyekiti wa CHAMUITA mikoa ya nyanda za juu kusini, Tumaini Msowoya Kibiki aliwataka wanachama wote kuwepo kwenye uzinduzi huo ili kumsindikiza mwenzao.

“Ni jukumu la waimbaji wote hususani wanachamuita kuhakikisha wanakuwepo siku ya uzinduzi ili kumuunga mkono mwanachama wenzetu,”alisema Kibiki.

Mwisho

Wednesday, March 4, 2015

ZITTO KABWE " NITAJITOA RASMI CHADEMA MWEZI MACHI"... "CUF" NDIO CHAGUO LANGU


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amesema hatma yake kisiasa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) itajulikana katika kipindi cha mwezi mmoja kutoka sasa.
Raia Mwema linafahamu kwamba tangazo hilo la kisiasa linahusu mustakabali wake wa kisiasa ndani ya Chadema, chama ambacho amekitumikia katika maisha yake yote ya kisiasa tangu akiwa mtoto wa umri wa miaka 16.
Katika mahojiano aliyofanya kwa njia ya mtandao na gazeti maarufu la Guardian la Uingereza wiki iliyopita, Zitto alisema kuna kitu kikubwa atakifanya mwishoni mwa mwezi Machi huu.
“Sijawahi kufanya kampeni yoyote kubwa ya kisiasa kupitia mtandao wa twitter katika maisha yangu ya kisiasa, lakini nataraji kuwa nitafanya hivyo katika muda wa mwezi mmoja kutoka sasa. Fuatilieni tu twitter na mtaona,” alisema Zitto pasipo kwenda kwa undani.


Gazeti hilo la Uingereza limeanzisha utaratibu mpya wa kuhoji watu maarufu kwa kutumia mtandao wa twitter (twit interview) na Zitto alikuwa mwanasiasa wa kwanza kuhojiwa baada ya kubainika kuwa ndiye anayeongoza kwa kuwa na wafuasi wengi kwenye mtandao huo hapa nchini.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu nini hasa anataraji kukifanya mwishoni mwa mwezi Machi kama alivyozungumza na gazeti hilo, Zitto alisema ni mapema kwa sasa kuweka kila kitu hadharani lakini wakati ukifika kila kitu kitakuwa wazi.
“Niseme kwamba kwenye mahojiano yale nilisema hivyo kweli na nakuhakikishia kuwa kuna tukio litatokea mwishoni mwa mwezi Machi. Ni tukio gani na linahusu nini bado mapema kusema.
“Ila naomba kuahidi Watanzania kuwa watafahamu kila kitu kuhusu tukio hilo wakati ukifika. Hiyo kampeni ambayo itaendeshwa kupitia mtandao wa twitter na mingineyo, itakuwa ya kisasa na ya uhakika kuliko yoyote ambayo imewahi kuendeshwa katika historia ya Tanzania, “ alisema.
Zitto alikataa kusema lolote kama tangazo hilo litahusiana moja kwa moja na kuhama kwake kutoka Chadema kwenda ACT au chama chochote kingine cha siasa hapa nchini zaidi ya kusema; “subirini”.
Kwa sasa, Zitto ni Mbunge na mwanachama wa Chadema kwa sababu tu ya zuio ambalo Mahakama Kuu kupitia Jaji John Utamwa liliweka katikati ya mwaka jana la kufukuzwa kwake ndani ya chama hicho kutokana na kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho.
Zitto na wenzake, Profesa Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, walifukuzwa na Chadema kwa madai ya kupanga mapinduzi ya kumng’oa madarakani Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Mwigamba na Kitila wamehamia katika chama kipya cha siasa cha ACT; Mwigamba akiwa Katibu Mkuu wa muda na mwenzake mshauri na Zitto mwenyewe amekuwa akihusishwa na chama hicho.
Akizungumzia mahojiano hayo ya Zitto na Guardian, Dk. Kitila Mkumbo alisema aliyasoma mahojiano hayo lakini akasema anayejua nini kitatokea mwishoni mwa Machi ni Zitto mwenyewe.
“Mimi kama mshauri wa ACT nasema Zitto kama mwanasiasa makini ana mawazo yake na mipango yake. Mimi nasisitiza tu kwamba kama ataamua kuja ACT basi tunamkaribisha kwa mikono yote miwili.
“Tunaamini kwamba yeye ni muumini wa dhana ya Unyerere (Nyerereism) ambayo ndiyo msingi mkuu wa sera za ACT. Kama ataamua vinginevyo, sisi pia tutamuunga mkono kwa sababu tunajua itakuwa kwa nia njema,” alisema.
Katika mahojiano hayo na Guardian, Zitto aliulizwa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu siasa na Tanzania, ikiwamo changamoto za kisiasa, hifadhi za jamii na nguvu ya mitandao ya kijamii katika siasa za hapa nchini.
Zitto alisema silaha kubwa ya maendeleo ambayo Tanzania inayo kwa sasa ni wingi wa vijana ambao alisema kama watawekewa mipango mizuri na kuwezeshwa kutumika kwa kadri ya uwezo wao, Taifa litapiga hatua kubwa.
Alisema fursa hiyo ina hatari yake nyingine kwamba chini ya asilimia 20 ya Watanzania hawana ulinzi wowote wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii, jambo alilosema ni hatari kwa mustakabali wa Taifa.
Alisema pia kwamba kwa sasa Watanzania wengi wana ufahamu wa masuala ya mitandao ya kijamii, lakini akasema idadi ya wanaoitumia ni ndogo; huku akibainisha kuwa baadhi ya viongozi wa juu wa serikali hawako hata kwenye mitandao kama twitter.
Zitto ana wafuasi zaidi ya 200,000 katika mtandao wa twitter akiwa anaongoza kwa wafuasi; huku katika nchi nyingine barani Afrika wanaoongoza wakiwa marais, wanamichezo na wanamuziki maarufu kama Didier Drogba wa Ivory Coast na Wiz Kid wa Nigeria.
CHANZO; GAZETI LA RAIA MWEMA

JACKSON KISWAGA APIGA JEKI UJENZI WA MAABARA SEKONDARI YA NYABULA KALENGA


SHULE ya sekondari Nyabula imeingia katika hatua nyingine ya kukamilisha ujenzi wa maabara zake baada ya kupata msaada unaohusisha mabati 50 na mifuko ya saruji 30.

Msaada huo kwa shule hiyo inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Parokia ya Nyabula ulitolewa na mdau wa maendeleo ambaye pia ni Kamanda wa Chipukizi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa wilaya hiyo, Jackson Kiswaga.

Akikabidhi msaada huo hivikaribuni, Kiswaga aliwataka wananchi kujitokeza kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo katika maeneo yao ili kuondokana na dhana ya kila jambo kufanywa na serikali.

“Ukiwaita watu kwenye harambee ya kufanikisha kwa mfano, harusi, wengi watajitokeza na kutoa michango yao lakini ukiwaita kuchangia maendeleo yao hawajitokezi,” alisema.

Alisema katika dunia ya ushindani, elimu ndio ufunguo muhimu zaidi wa maisha kwakuzingatia kwamba ukishakuwa nayo hakuna mtu wa kukupokonya.

“Elimu ni kila katika katika ulimwengu huu unaolinganishwa hivisasa na kijiji kimoja. Elimu ni maisha, elimu ni maendeleo kwahiyo nitoe wito kwa wazazi, walezi na kila mwenye uwezo wa kufanya kazi aone umuhimu wa kuchanngia maendeleo yake,” alisema.

Alisema katika soko la ajira duniani kote waajiriwa wanapimwa au kupatikana kutokana kwa kuzingatia vigezo vya elimu vinavyotakiwa.

“Kwahiyo tukiulizwa vipaumbele vyetu, tunaweza kusema elimu elimu elimu kwasababu hiyo pekee ndio inayoweza kutumika kubadili mazingira yetu na kutuletea maendeleo,” alisema.

Kiswaga alisema kwa kuzingatia hilo ataendelea kusaidia maendeleo ya sekta ya elimu wilayani humo na kwingine kote atakakoombwa kwa kuzingatia nafasi atakayokuwa nayo.

Akishukuru kwa msaada huo, Padri wa Parokia ya Nyabula Philipo Kindole alisema utasaidia harakati zao za kukamilisha ujenzi wa maabara katika shule hiyo na akaomba wadau wengine kujitokeza kuichangia sekta hiyo.

Thursday, February 26, 2015

MTOTO MCHANGA AUAWA NA KUTUPWA KICHAKANI MKOANI MOROGORO

Matukio ya kutupa watoto wachanga yameendelea mkoani Morogoro ambapo mtoto mchanga wa siku moja ameuwa na kutupwa vichakani katika eneo la kichangani mjini Morogoro.

Mtoto huyo mwenye jinsi ya kike anaonekana ametupwa kwa saa kadhaa zilizopita ambapo wakizungumzia tukio hilo baadhi ya mashuhuda wamelalamikia kuongezeka kwa matukio ya watoto wachanga kutupwa  ambapo wameomba wazazi kuwahurumia watoto   wasio na hatia huku baadhi ya wakinamama waliokuwepo katika tukio hilo wameonyesha kusikitishwa na kueleza wakati mwingine inatokana na baadhi ya wanaume kukwepa majukumu.
 
Naye mwenyekiti wa mtaa na diwani wa kata ya kichangani John Waziri walioshuhudia tukio hilo wamesema tukio hilo si la kuvumilika na kuomba wananchi kuwafichua wanaowabainika kuzaa na kutupa watoto  kwa lengo la kukwepa majukumu na pia kuomba wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kufanikisha kupatikana kwa mtuhumiwa.
 
Jeshi la polisi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na wamefika katika eneo la tukio na kuchukua mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro.

UKAWA WAITAKA SERIKALI KUSITISHA ZOEZI LA UPIGAJI KURA YA MAONI YA KATIBA PENDEKEZWA

Viongozi wa vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi UKAWA umeitaka serikali kusitisha zoezi la upigaji wa kura ya maoni ya katiba kutokana na zoezi hilo kutokidhi vigezo vya kisheria na badala yake ielekeze nguvu na rasilimali fedha katika zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ili kuliepusha taifa kuingia katika machafuko.

Viongozi wakuu wa vyama vinavyounda umoja huo wa katiba ya wananchi ukawa wakiongozwa na Profesa Ibrahimu Lipumba wa chama cha wananchi CUF na Freeman Mbowe wa chama cha demokrasia na maendeleo Chadema, chama cha NLD Dr Emmanuel Makaidi, chama cha NCCR mageuzi Mosena Nyambabe wameitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari.
 
Mwenyekiti wa CUF Prof Ibrahimu Lipumba amemtaka rais Prof Jakaya Mrisho Kikwete kutoa kauli ya kuusitisha mchakato wa kura za maoni ya katiba pendekezwa kwa kuwa zoezi hilo kwa sasa haliwezi kutekelezeka April 30 ya mwaka huu kama rais alivyotangaza licha ya kutokuwa na mamlaka ya kutangaza tarehe ya kufanyika kwa kura hizo za maoni.
 
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo Chadema Freeman Mbowe ameitaka serikali kuelekeza fedha kidogo zilizopo katika zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kuwa zoezi hilo linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kutosha na kusitisha kabisa zoezi la kura za maoni ya katiba ili kuiepusha nchi na kile alichodai kuwa ni machafuko yanayowea kuzuilika.
 
Hivi sasa taifa liko katika maandalizi ya kushiriki katika zoezi la kura za maoni ya katiba pendekezwa linalotarajiwa kufanyika alhamis ya April 30, 2015 kama ilivyotangazwa na mh rais wa jamhuri ya mungano wa Tanzania licha ya uwepo wa kauli za kulipinga zoezi hilo kutoka hasa katika vyama vya siasa vya upinzania na baadhi ya vyama vya kiraia kwa sababu kadha wa kadha

JESHI LA POLISI LAPATA AIBU KUBWA, POLISI WAKE AKUTWA AKIFANYA MAPENZI HADHARANI AKIWA AMEVAA SARE ZA JESHI HILO

polise 
 
 
Unakumbuka ile Stori ya askari Asuma Mpaji na Veronica Nazaremo kufukuzwa kazi Mkoani Kagera baada ya picha zao kusambaa mitandaoni wakionekana kupigana mabusu? safari hii nakuletea tena stori inayofanana na hiyo ambayo imetokea Nchini Uingereza.

Polisi wa nchi hiyo ya Uingereza waliamua kumshtaki mwenzao baada ya kufanya kitendo cha kudhalilisha jeshi la nchi la nchi hiyo kwa kufanya tendo la ndoa tena mbele za watu akiwa na sare za kazi.

Kitendo hicho kimemfanya kufukuzwa kazi bila kupewa taarifa za awali haraka baada ya kwenda kwenye shughuli zake za kila siku za usalama na kufanya kitendo hicho huku akijua ni kinyume na sheria tena akiwa amezungukwa na watu.

Msaidizi mkuu wa kituo hicho Russ Middleton alisema wanaamini hatua hiyo itakua fundisho kwa wengine kutokana na kitendo hicho cha udhalilisha.

Kwa upande mwingine polisi mwingine nchini Uruguay naye alikumbwa na mkasa unaofanana na huo baada ya kucheza na mwanamke akiwa uchi katika kituo chake cha kazi.

Picha ya askari huyo zilinaswa na mitandano mbalimbali na kujikuta zikisambaa kwa kasi hali iliyosababisha ashtakiwe kwa kosa hilo.

SERIKALI ISIMAMIE VYEMA HAKI ZA BINADAMU KWA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI

   waandishi wa habari kutoka mikoa ya nyanda za juu kusini wakipata mafunzo ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia yanayoendeshwa na TAMWA

CHAMA cha Waandishi wa habari Wanawake (TAMWA) kimeishauri serikali  kusimamia vyema haki za binadamu, sambamba na kutoa adhabu kali kwa ajili ya kutatua tatizo la unyanyasaji wa kijinsia nchini.

Vilevile waandishi wa habari nchini wametoa ombi kwa baraza la habari Tanzania (MCT) pamoja na TAMWA kufikiria kuziwezesha klabu za waandishi wa habari za mikoani vyombo vya usafiri ili kusaidia kutumia vyombo vya usafiri wa viongozi (sources).

Hayo yalisemwa jana katika semina ya Tamwa iliyofanyika mjini hapa na kuwashirikisha waandishi wa habari kutoka mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Ruvuma.

Akizungumza katika semina hiyo, mwezeshaji wa Tamwa, Wence Mushi alisema serikali inapaswa kuchukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kutoa adhabu kali kwa ajili ya kuondokana na tatizo la unyanyasaji wa kijinsia hususani kwa watoto, wanawake na watu wenye ulemavu wa ngozi.

 “Kama sheria za haki za binadamu hazitasimamiwa vizuri na maafisa Ustawi wa Jamii bado ukatili wa aina yoyote utaendelea katika mazingira tunayoishi, hadhi ya wanawake na kuonekana kama ni chombo cha starehe itaendelea kwa sababu haki hazisimamiwi ipasavyo,”alisema Mushi.

Mushi aliwataka wanahabari kuendelea kuibua mambo ya kikatili yanayofanywa na baadhi ya watu hasa kwa watoto, wanawake na walemavu wa ngozi ili kuipa elimu jamii na kushinikiza serikali kuchukua hatua katika ukatili huu.

“Kuna taasisi na mashirika yanayojihusisha na kutetea haki za watoto hivyo ni vyema waandishi kila wanapoona matukio kama hayo yanatokea wakayaibua ili kuyatokomeza kwa kuchukuliwa hatua,”alisema Mushi.

Kwa upande wake mwandishi  Geofrey Nilahi kutoka gazeti la Tanzania Daima, Songea alisema kuwa wanahabari ni chachu ya mabadiliko kama tukiibua mambo ya kikatili yanayofanywa na kushinikiza yafanyiwe mabadiliko hasa katika usimamizi wa sheria na kuchukuliwa hatua kwa wahalifu.

“Wanahabari ni chombo muhimu sana na ili kutokomeza ukatili wa aina yoyote ni lazima kalamu zetu zitumike kukemea mambo yasiyostahili kutedwa na kufuata haki za binadamu ili kuleta usawa katika jamii,” alisema.

Festo Sikagonamo mwakilishi wa ITV Mbeya alisema kuwa endapo wanahabari wakiwezeshwa na  TAMWA kufuatilia habari  juu ya ukatili wa kijinsia pamoja na mauaji ya watu wenye ulemavu hakika mabadiliko yatakuja kupitia kalamu zetu.

Waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo, waliiomba Tamwa kuwawezesha vyombo vya usafiri vyama vya waandishi wa habari za mikoani (Press Clubs) kwa ajili ya kufuatilia habari katika maeneo ya vijijini ambako wanaamini ndiko habari nyingi zinapopatika.

“Tukiwezeshwa usafiri tunaamini tutaleta habari za kuelimisha jamii, tutaibua mambo mbalimbali na baadaye kuyapatia ufumbuzi kupitia viongozi husika,” alisema George Tarimo mwandishi wa habari Nipashe Iringa.

Wednesday, February 25, 2015

FFU watumia mabomu kutuliZa vurugu Ilula ,magari yachomwa moto ,mahabusu waachiwa silaha zaporwa



KIJANA WA KITANZANIA AUNDA REDIO STESHENI

 - SHUJAAZ! Shujaaz Banner
DJ Tee (19) ni kijana mwenye ndoto kubwa katika maisha yake. Baada ya kuona mahangaiko ya vijana kuelekea kwenye mafanikio, wengi wakiwa wamemaliza shule na vyuo bila kupata kazi, ameamua kuunda redio stesheni ghetoni kwake aliyoipa jina la Shujaaz, ili aweze kushea ideas na vijana wote nchini Tanzania kuhusu mbinu mbalimbali za kuingiza pesa, kuwapa stori za vijana wanaochakarika katika maisha yao pamoja na kuwaburudisha.
"Nimeamua kuiita Shujaaz kwa sababu, naamini kuwa kijana ambaye anajituma na kuweka mfano bora kwenye jamii ni shujaa". Alisema DJ Tee. "Ndoto zangu zinakaribia kuwa kweli".
Story ya kijana huyu inapatikana kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kupitia kijarida cha Shujaaz, kitakachokuwa kinasambazwa kupitia gazeti la Mwanaspoti, kuanzia JUMAMOSI HII ya tarehe 28. Kwenye kijarida hicho, utapata ideas mbali mbali ambazo vijana wanaweza kuzifuata na kujiingizia kipato. Pia, kutakuwa na stori za vijana wengine kama Pendo, Semeni na Pepe ambao ni mashabiki wakubwa wa DJ Tee na redio show yake ya Shujaaz.
DJ Tee akiwa studio
DJ Tee akiwa studio.
Kijana huyu ameamua kujiita DJ Tee ili asijulikane na watu wake wa karibu, kwa kuwa ana-hack airwaves za redio stesheni ili aweze kusikika. Sikiliza redio stesheni uipendayo kuanzia wiki ijayo, huwezi jua, inawezekana DJ Tee akawa hewani!
Wewe pia USIKOSE kuwa sehemu ya mafanikio na harakati za kijana huyu kwa kujiunga naye. Pata nakala yako ya Shujaaz kuanzia Jumamosi hii (28/02/2015) kupitia gazeti la Mwanaspoti. Pia, jiunge naye kwenye ukurasa wake wa Facebook kwa jina DJTee255 ili upige naye story na wewe uweze kushea idea zako za hustle. Unaweza pia ukampata Instagram na Twitter kwa jina @djtee255
Studio
Studio.

WATANZANIA WAASWA KUTHAMINI BIDHAA ZINAZOZALISHWA NDANI YA NCHI



KAIMU MENEJA WA SIDO MKOA WA IRINGA, MR NIKO MAHINYA AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI OFINI KWAKE
KAIMU MENEJA WA SIDO MKOANI IRINGA, NIKO MAHINYA AKIWA NA MHANDISI WA KARAKANA YA SIDO IRINGA, MICHAEL MATONYA WAKATI WAKITEMBELEA UTENDAJI KAZI WA KARAKANA HIYO
FUNDI WA KARAKANA YA SIDO ELAYSON TARIMO AKIANGALIA MASHINE YA KUNOA VYUMA, AMBAYO ILIKUWA IKINOA MAJEMBE YA KUKATIA CHAI
MSIMAMIZI WA KARAKANA YA KUTENGENEZEA MASHINE MBALIMBALI YA SIDO MKOANI IRINGA, LEONARD LUMATO AKIENDELEA NA KAZI KATIKA KARAKANA HIYO
KIJANA AKIENDELEA NA KAZI NDANI YA KARAKANA

NA FRANK KIBIKI, IRINGA


SHIRIKA la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO), mkoani Iringa limewataka watanzania kujenga utamaduni wa kupenda bidhaa zinazotengenezwa ndani, badala ya zile zinazoingizwa kutoka nje ili kukuza uchumi wan chi.
 
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa, Kaimu meneja wa SIDO mkoani Iringa, Niko Mahinya alisema ikiwa watanzania wataenzi bidhaa zinazotengenezwa ndani itakuwa rahisi kuinua uchumi wa nchi, na mtu mmoja mmoja.
Alisema shirika hilo limekuwa likitengeneza bidhaa nyingi, zikiwemo mashine na pembejeo za kilimo lakini, kutokana na dhana ya kununua bidhaa za nje wamekuwa wakikabiliana na tatizo kubwa la soko.
 
“Tunazalisha mashine mbalimbali, zikiwemo zana za kilimo kama vile, mashine za kusagia nafaka, kuchujia mafuta ya alizeti, kukamulia asali na nyingine nyingi lakini changamoto kubwa ni soko la bidhaa za ndani,”alisema
 
Aidha alisema itakuwa vyema kama serikali itaweka utaratibu au sera itakayofanya watu wajenge tabia ya kuheshimu, kupenda na  kutumia bidhaa za ndani.
 
Kwa upande wao baadhi ya wajasiriamali na wakulima walisema kuwa mara nyingi wamekuwa wakinunua mashine za kichina kutokana na bei yake kuwa chini ingawa hazina ubora.
 
“Bidhaa za nje ni bei ndogo kuliko zile zinazotengenezwa ndani, hii ndiyo sababu inayofanya wengi tutumie bidhaa za kichina ambazo hata hivyo hazidumu kwa muda mrefu,”alisema LeoniKA Sanga, mmilikiwa kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti, mjini Iringa.
 
Aliiomba serikali kutoa ruzuku kwa SIDO ili bidhaa zinazotengenezwa zishushwe bei yake na kuweza kuwahudumia wajasiriamali na wakulima wadogo.

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More