MBUNGE wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe, amesema hatma yake kisiasa ndani ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) itajulikana katika kipindi cha mwezi mmoja
kutoka sasa.
Raia Mwema linafahamu kwamba
tangazo hilo la kisiasa linahusu mustakabali wake wa kisiasa ndani ya Chadema,
chama ambacho amekitumikia katika maisha yake yote ya kisiasa tangu akiwa mtoto
wa umri wa miaka 16.
Katika mahojiano aliyofanya
kwa njia ya mtandao na gazeti maarufu la Guardian la Uingereza wiki iliyopita,
Zitto alisema kuna kitu kikubwa atakifanya mwishoni mwa mwezi Machi huu.
“Sijawahi kufanya kampeni
yoyote kubwa ya kisiasa kupitia mtandao wa twitter katika maisha yangu ya
kisiasa, lakini nataraji kuwa nitafanya hivyo katika muda wa mwezi mmoja kutoka
sasa. Fuatilieni tu twitter na mtaona,” alisema Zitto pasipo kwenda kwa undani.
Gazeti hilo la Uingereza
limeanzisha utaratibu mpya wa kuhoji watu maarufu kwa kutumia mtandao wa
twitter (twit interview) na Zitto alikuwa mwanasiasa wa kwanza kuhojiwa baada
ya kubainika kuwa ndiye anayeongoza kwa kuwa na wafuasi wengi kwenye mtandao
huo hapa nchini.
Akizungumza na gazeti hili
kuhusu nini hasa anataraji kukifanya mwishoni mwa mwezi Machi kama
alivyozungumza na gazeti hilo, Zitto alisema ni mapema kwa sasa kuweka kila
kitu hadharani lakini wakati ukifika kila kitu kitakuwa wazi.
“Niseme kwamba kwenye
mahojiano yale nilisema hivyo kweli na nakuhakikishia kuwa kuna tukio litatokea
mwishoni mwa mwezi Machi. Ni tukio gani na linahusu nini bado mapema kusema.
“Ila naomba kuahidi Watanzania
kuwa watafahamu kila kitu kuhusu tukio hilo wakati ukifika. Hiyo kampeni ambayo
itaendeshwa kupitia mtandao wa twitter na mingineyo, itakuwa ya kisasa na ya
uhakika kuliko yoyote ambayo imewahi kuendeshwa katika historia ya Tanzania, “
alisema.
Zitto alikataa kusema lolote
kama tangazo hilo litahusiana moja kwa moja na kuhama kwake kutoka Chadema
kwenda ACT au chama chochote kingine cha siasa hapa nchini zaidi ya kusema;
“subirini”.
Kwa sasa, Zitto ni Mbunge na
mwanachama wa Chadema kwa sababu tu ya zuio ambalo Mahakama Kuu kupitia Jaji
John Utamwa liliweka katikati ya mwaka jana la kufukuzwa kwake ndani ya chama
hicho kutokana na kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho.
Zitto na wenzake, Profesa
Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, walifukuzwa na Chadema kwa madai ya kupanga
mapinduzi ya kumng’oa madarakani Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Mwigamba na Kitila wamehamia
katika chama kipya cha siasa cha ACT; Mwigamba akiwa Katibu Mkuu wa muda na
mwenzake mshauri na Zitto mwenyewe amekuwa akihusishwa na chama hicho.
Akizungumzia mahojiano hayo ya
Zitto na Guardian, Dk. Kitila Mkumbo alisema aliyasoma mahojiano hayo lakini
akasema anayejua nini kitatokea mwishoni mwa Machi ni Zitto mwenyewe.
“Mimi kama mshauri wa ACT
nasema Zitto kama mwanasiasa makini ana mawazo yake na mipango yake. Mimi
nasisitiza tu kwamba kama ataamua kuja ACT basi tunamkaribisha kwa mikono yote
miwili.
“Tunaamini kwamba yeye ni
muumini wa dhana ya Unyerere (Nyerereism) ambayo ndiyo msingi mkuu wa sera za
ACT. Kama ataamua vinginevyo, sisi pia tutamuunga mkono kwa sababu tunajua
itakuwa kwa nia njema,” alisema.
Katika mahojiano hayo na
Guardian, Zitto aliulizwa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu siasa na
Tanzania, ikiwamo changamoto za kisiasa, hifadhi za jamii na nguvu ya mitandao
ya kijamii katika siasa za hapa nchini.
Zitto alisema silaha kubwa ya
maendeleo ambayo Tanzania inayo kwa sasa ni wingi wa vijana ambao alisema kama
watawekewa mipango mizuri na kuwezeshwa kutumika kwa kadri ya uwezo wao, Taifa
litapiga hatua kubwa.
Alisema fursa hiyo ina hatari
yake nyingine kwamba chini ya asilimia 20 ya Watanzania hawana ulinzi wowote wa
Mifuko ya Hifadhi za Jamii, jambo alilosema ni hatari kwa mustakabali wa Taifa.
Alisema pia kwamba kwa sasa
Watanzania wengi wana ufahamu wa masuala ya mitandao ya kijamii, lakini akasema
idadi ya wanaoitumia ni ndogo; huku akibainisha kuwa baadhi ya viongozi wa juu
wa serikali hawako hata kwenye mitandao kama twitter.
Zitto ana wafuasi zaidi ya
200,000 katika mtandao wa twitter akiwa anaongoza kwa wafuasi; huku katika nchi
nyingine barani Afrika wanaoongoza wakiwa marais, wanamichezo na wanamuziki
maarufu kama Didier Drogba wa Ivory Coast na Wiz Kid wa Nigeria.
CHANZO; GAZETI LA RAIA MWEMA
0 comments:
Post a Comment