waandishi wa habari kutoka mikoa ya nyanda za juu kusini wakipata
mafunzo ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia yanayoendeshwa na TAMWA
CHAMA cha Waandishi wa habari Wanawake (TAMWA) kimeishauri
serikali kusimamia vyema haki za
binadamu, sambamba na kutoa adhabu kali kwa ajili ya kutatua tatizo la unyanyasaji
wa kijinsia nchini.
Vilevile waandishi wa habari nchini wametoa ombi kwa baraza
la habari Tanzania (MCT) pamoja na TAMWA kufikiria kuziwezesha klabu za
waandishi wa habari za mikoani vyombo vya usafiri ili kusaidia kutumia vyombo
vya usafiri wa viongozi (sources).
Hayo yalisemwa jana katika semina ya Tamwa iliyofanyika
mjini hapa na kuwashirikisha waandishi wa habari kutoka mikoa ya Iringa,
Njombe, Mbeya na Ruvuma.
Akizungumza katika semina hiyo, mwezeshaji wa Tamwa, Wence
Mushi alisema serikali inapaswa kuchukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kutoa
adhabu kali kwa ajili ya kuondokana na tatizo la unyanyasaji wa kijinsia hususani
kwa watoto, wanawake na watu wenye ulemavu wa ngozi.
“Kama sheria za haki
za binadamu hazitasimamiwa vizuri na maafisa Ustawi wa Jamii bado ukatili wa
aina yoyote utaendelea katika mazingira tunayoishi, hadhi ya wanawake na
kuonekana kama ni chombo cha starehe itaendelea kwa sababu haki hazisimamiwi
ipasavyo,”alisema Mushi.
Mushi aliwataka wanahabari kuendelea kuibua mambo ya
kikatili yanayofanywa na baadhi ya watu hasa kwa watoto, wanawake na walemavu
wa ngozi ili kuipa elimu jamii na kushinikiza serikali kuchukua hatua katika
ukatili huu.
“Kuna taasisi na mashirika yanayojihusisha na kutetea haki
za watoto hivyo ni vyema waandishi kila wanapoona matukio kama hayo yanatokea
wakayaibua ili kuyatokomeza kwa kuchukuliwa hatua,”alisema Mushi.
Kwa upande wake mwandishi Geofrey Nilahi kutoka gazeti la Tanzania Daima, Songea alisema kuwa wanahabari ni chachu ya mabadiliko kama tukiibua mambo ya kikatili yanayofanywa na kushinikiza yafanyiwe mabadiliko hasa katika usimamizi wa sheria na kuchukuliwa hatua kwa wahalifu.
“Wanahabari ni chombo muhimu sana na ili kutokomeza ukatili
wa aina yoyote ni lazima kalamu zetu zitumike kukemea mambo yasiyostahili
kutedwa na kufuata haki za binadamu ili kuleta usawa katika jamii,” alisema.
Festo Sikagonamo mwakilishi wa ITV Mbeya alisema kuwa endapo
wanahabari wakiwezeshwa na TAMWA
kufuatilia habari juu ya ukatili wa
kijinsia pamoja na mauaji ya watu wenye ulemavu hakika mabadiliko yatakuja
kupitia kalamu zetu.
Waandishi
wa habari walioshiriki mafunzo hayo, waliiomba Tamwa kuwawezesha vyombo vya
usafiri vyama vya waandishi wa habari za mikoani (Press Clubs) kwa ajili ya
kufuatilia habari katika maeneo ya vijijini ambako wanaamini ndiko habari
nyingi zinapopatika.
“Tukiwezeshwa
usafiri tunaamini tutaleta habari za kuelimisha jamii, tutaibua mambo
mbalimbali na baadaye kuyapatia ufumbuzi kupitia viongozi husika,” alisema
George Tarimo mwandishi wa habari Nipashe Iringa.
0 comments:
Post a Comment