WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amekemea matukio ya mauji yanayoendelea nchini na kusema kuwa hakuna dini inayofundisha vitendo hivyo viovu.
Alisema serikali inawaomba viongozi wa dini nchini kuendelea kushirikiana nayo kutoa elimu kwa waumini wao kama njia ya kukomesha mauaji dhidi ya watu wasiokuwa na hatia nchini.
Akizungumza Dar es Salaam jana katika fainali ya mashindano ya kimataifa ya kuhifadhi Koran nchini, alisema ni wajibu kwa Watanzania kushikana kulinda amani ya nchi.
“Napenda nigusie mambo machache ambayo nimeyaona; ni hivi karibuni nchi yetu ilingia katika mtihani ambao wengi wenu kupitia vyombo vya habari mliarifiwa juu ya kuuawa kwa waumini wema waliokuwa wakifanya ibada ndani ya msikiti kule mkoani Mwanza.
“Katika siku za hivi karibu kumekuwa na matukio mabaya mbele ya macho yetu na nchi yetu imefika mahala hadi watu wanafuatwa majumbani na kuchinjwa jambo ambalo kwetu sisi kama Serikali tuna kazi ya kulinda uhai wa kila Mtanzania.
“Linapotokea suala kama hili hatuwezi kula wala kulala mpaka tuone juhudi za dhati katika kukomesha unyama wa aina hii,” alisema Majaliwa.
Alisema Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama inaendelea kushughulikia tatizo hilo kwa umakini na akawataka Watanzania kuendelea kutoa ushirikiano.
Akizungumzia utendaji wa Serikali ya awamu ya tano, alisema watendaji wengi ni wapya huku akiomba kukoselewa inapokosea jambo ambalo litasaidia kujenga Serikali imara na yenye mshikamano.
Mashindano hayo ya kuhifadhi Koran yalihusisha washiriki 21 kutoka mataifa mbalimbali duniani huku kijana, Rashid Ally (8) kutoka Tajikistan akiibuka mshindi wa kwanza.
0 comments:
Post a Comment