Wednesday, June 29, 2016

Taarifa ya Lugumi Yapigwa Kalenda Tena Bungeni

Ripoti ya sakata la mkataba wa kampuni ya Lugumi Enteprises na Jeshi la Polisi, ambayo ilikuwa iwasilishwe kwenye mkutano unaoendelea wa Bunge, sasa itawasilishwa kwenye mkutano ujao.

Makamu mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Hilary Aeshi alisema ripoti hiyo itaunganishwa katika taarifa za kamati ambazo kwa utaratibu huwasilishwa kwenye mkutano huo.

Sakata hilo linahusisha utekelezaji mbovu wa mkataba wa kufunga mashine za kielektroniki za kuchukulia alama za vidole kwenye vituo 108 vya polisi.

Hadi wakati Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akifanya ukaguzi wa mkataba huo wa Sh37 bilioni uliosainiwa mwaka 2013, ni vituo 14 tu vilivyokuwa vimefungwa mashine hizo, lakini mzabuni alishalipwa Sh36 bilioni.

Baada ya sakata hilo kuibuliwa, wabunge walitaka liwasilishwe kwenye mkutano unaoendelea mjini Dodoma, lakini PAC ikaunda kamati ndogo ambayo sasa inatakiwa iwasilishe ripoti ya uchunguzi wake.

Hadi jana asubuhi ripoti ya kamati hiyo ndogo, iliyoundwa na wajumbe tisa, ilikuwa bado haijawasilisha ripoti yao.

Hata hivyo, Aeshi ambaye pia ni mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), alisema alitarajia kukabidhiwa ripoti hiyo na kamati ndogo jana na baada ya hapo kazi ya uchambuzi wa kamati nzima itaanza.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More