Wednesday, May 23, 2018

MBUNGE CHUMI AITAKA SERIKALI KUPELEKA MAAFISA WENGI KWENYE BALOZI ZA NJE

Mbunge wa Mafinga Mjini Cosato Chumi ameishauri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano kupeleka Maafisa wa kutosha kwenye Balozi za Tanzania maeneo mbali mbali Duniani.

Akichangia katika Wizara hiyo, Chumi alisema kuwa Balozi kama New York ambako kuna shughuli nyingi za Umoja wa Mataifa zinazohitaji ushawishi hasa katika masuala ya kutunza amani kwenye maeneo ya migogoro kama DRC.

UN imekuwa ikipunguza bajeti ya shughuli za Umoja wa Mataifa katika Bara la Afrika kama vile bajeti ya kulinda amani Afrika na fedha za kugharamia shughuli za iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Rwanda-ICTR (International Criminal Tribunal for Rwanda)

Chumi ambaye kabla ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Mafinga Mjini alikuwa Mtumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje, alisema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2018/19 mapendekezo kwa ajili ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Rwanda, ilikuwa  dola za kimarekani 215m lakini kutokana na kukosa utetezi wa kutosha, Mahakama hiyo ikatengewa kiasi cha dola 88m tu.

Kiasi hiki cha dola 215m kingeweza kuongeza mzunguko wa fedha hapa nchini, sasa tumekuwa na Maafisa wachache hivyo tukakosa nguvu ya kutetea na kushawishi na matokeo yako ikatengwa dola 88m

Akizungumzia mabadiliko (reforms) yanayoendelea ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mbunge huyo alisisitiza ushiriki madhubuti wa Tanzania ili kusudi Bara la Afrika kupata nafasi mbili za   kura ya Veto kwenye Umoja wa Mataifa kama ilivyo kwa nchi za Marekani, Uingereza, China, Urusi na Ufaransa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Umoja wa Mataifa umekuwa ukipunguza bajeti ya ulinzi wa amani Afrika, hivyo ni muhimu ushiriki na ushawishi wetu kama Taifa lenye nguvu na heshima kwenye nyanja za kidplomasia Afrika, Asia na  Duniani kwa ujumla ukazingatiwa

Chumi alifafanua kuwa, kumekuwepo na jitihada za kuihamisha iliyokuwa Mahakama ya Makosa ya Rwanda kwenda The Hague, Uholanzi jambo ambalo litaondoa fursa mbalimbali kwa Taifa na kufuta historia muhimu kwa Taifa letu, hivyo upo umuhimu wa kushiriki kwenye mchakato huo wa mabadiliko ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ufanisi na weledi.

Akizungumza badae, Chumi alisema kuwa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa linaundwa na nchi 15 lakini katika hizo nchi tano zina kura ya turufu, ambapo na nchi nyingine kumi huchaguliwa miongoni mwa nchi wanachama na hutumikia Baraza kwa mzunguko wa  miaka miwili.

kwa ilivyo sasa, katika zile nchi tano, moja ikikataa, mambo hayaendi, na Afrika yenye nchi zaidi ya robo haina mwakilishi katika zile nchi tano zenye kura ya turufu, ndio maana ni muhimu sana kama Taifa tukashiriki ipasavyo, na ushiriki huo utakuwa madhubuti kama Wizara itapeleka maafisa kwenye Ubalozi wetu wa New York na Balozi nyingine zote

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More