Friday, July 21, 2017

UVCCM: WALIOHAMIA UPINZANI WAACHE MARA MOJA KUGOMBANISHA WASTAAFU

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) umewakanya wanasiasa waliohamia upinzani toka CCM wanaoeneza maneno ya chuki na mifarakano kwa lengo la kuwagombanisha marais wastaafu  washindwe na walegee kwasababu kila Rais mstaafu alitimiza haki na wajibu wake alipokuwa madarakani.
Pia Umoja huo umeelezea kukerwa kwake na tabia ya baadhi ya viongozi wa upinzani ambao asubuhi hutamka maneno haya  na jioni wanapojisahau, hunena mengine bila ya kuwa na indhar wala kumbukumbu ya kutosha.
Onyo hilo limetolewa jana katika kijiji cha Ubinza, wilayami Uvinza mkoani hapa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Shaka Hamdu Shaka alipozungumza na wanachamawa CCM  na jumuiya zake katika ukumbi wa CCM  akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku tano Mkoani humu.
Shaka alisema wapo baadhi ya wanasiasa wa upinzani wengi wakiwa ni wale waliokihama Chana Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na vyama vingine, wanajaribu kwa namna moja au nyingine kuwafarakanisha marais wastaafu na Rais aliyeko madarakani kwasababu zao binafsi na za kisiasa bila kupima menono yao wala kutafakari kwa kina .
Aidha Shaka akimzungumzia Rais wa awamu ya kwanza Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere, alisema ameiachia heshima kubwa Tanzania katika medani za kidiplomasia na kimataifa,akashirikiana na mwenzake Hayati Sheikh Abeid Amani Karume hadi kuundwa  Muugano wa Tanganyika na Zanzibar huku nchi yetu mahali popote uendapo duniani sasa ikitajika kwa wema na heshima ya juu.
Alisema Awamu hiyo ya kwanza ya utawala wa Mwalimu Nyerere ndiyo ulioweka misingi ya utaifa, kuwaungisha watanzania, kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili kuwa ya Taifa, akajenga viwanda na kuanzisha kampuni za serikali na mashirika ya umma pia akashiriki kizalendo katika harakati za ukombzi Kusini mwa Afrika.
"Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ndiye aliyetuunganisha na kutufanya tuwe wamoja , amepigania uhuru, akaleta umoja wa kitaifa, amekomesha ukabila, udini na ubaguzi wa rangi hadi kusimama kwa Taifa letu na kuwa moja " Alisema Shaka.
Akiitaja awamu ya Pili, alisema chini ya Rais Mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi ndipo ilipofunguka milango ya biashara huria, kutolewa ruksa kwa kila mmoja kujituma na kujitegemea kiuchumi ,kuanza ujio wa wawekezaji na kutokea kwa fursa mbalimbali za kimaendeleo na  kiuchumi.
Kaimu huyo Katibu Mkuu aliutataja uongozi wa Mzee Mwinyi  ndiyo ulioanzisha mfumo wa Vyama vingi na kupanuka kwa haiba ya demokrasia, kuwepo kwa uhuru wa vyombo vya habari lakini pia utawala wa Rais huyo ndiyo uliotanua wigo kwa wananchi kujiajiri wenyewe katika sekta binafsi na kujitegemea.
Akizungumzia utawala katika awamu ya tatu  alisema ndiyo awamu ilioendesha nchi kwa msingi ya dhana ya uwazi na ukweli, kuwavutia wawekezaji, kupanuka kwa sekta ya utalii, kuanzishwa kwa miradi ya elimu ya Mmem na Mmes, kujengwa kwa daraja la mto  Rufiji, miundombinu ya barabara na kubuliwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao uliinua sana maisha ya wananchi masikini vijijini.
Shaka akizungumzia awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Dk Jakaya Kikwete alisema ndiyo iliboresha miundombinu ya barabara zinazoiunganisha mikoa yote nchini huku takwimu zikionesha kipindi chake ndicho ambacho barabara nyingi za lami zilijengwa
"Serikali ya Dk Kikwete ilisimamia vyema ujenzi wa shule za kisasa za sekondari, chuo kikuu kikubwa barani Afrika cha Udom, kuibuka vyuo vikuu vingi vya serilaku na binafsi huku katika kila Kata kukiwa na sekondari, hospitali, vituo vya afya na zahanati" Alieleza Shaka 
Alieleza  utawala huo ndiyo ambao uliiweka katika chati nchi yetu kimataifa, kulijenga madaraja makubwa ya Kigamboni, Simiyu  na Malagarasi, viwanja vya ndege vya Songwe na Mafia huku daraja la Kilombero likiwa limeachwa kwenye hatua za mwisho katika ujenzi wake ikiwemo utoaji ajira nyingi katika sekta za elimu na Afya.
Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema awamu ya tano ambayo inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli ikiwa na miaka miwili madarakani,  ndiyo inayofanya maajabu katika kupambana na vitendo vya ufisadi, kukomesha rushwa, kusimamisha nidhamu ya kazi, uwajibikaji, kununua ndege , kujenga reli kwa kiwango cha kimataifa na awamu hiyo ambayo haitasahauliwa na watanzania kwa kupigania maslahi ya umma na kushamirisha  uzalendo .
"Awamu ya tano ndiyo mwisho wa reli, kama mtu alisafiri  kwa treni toka Dar es Salaam, hapa Kigoma ndiyo mwisho wake, Rais Dk Magufuli  ni mwisho,  amefanya ya kufanya na atazidi kufanya maajabu na kuiletea nchi mageuzi hatimaye kuwa pepo mpya katika uso wa dunia na Afrika " Alisema Shaka huku akishangiliwa.
Aliwataka wananchi kuipa ushirikiano Serikali ya Rais wa awamu ya tano  katika dhamira  ya kusimamia matumizi bora ya rasilimali, kukuza haiba ya uzalendo lakini pia katika juhudi za kufanya nchi yetu kuwa ya viwanda na yenye uchumi wa kati.
Jumla ya wanachama 24 toka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, UDP na CUF kwa hiari na uamuzi wao walijiunga na CCM katika mkutano huo wa ndani na kukabidhiwa kadi mpya za CCM  na jumuiya zake.
Kaimu huyo katibu mkuu wa anaendelea na ziara yake ya kikazi katka wilaya za Kigoma Mjini na Kakonko kabla hajahitimisha ziara hiyo mkoani humu    

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More