Umoja
wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema kuwa kazi kubwa
inayofanywa kwa sasa na Rais Dk. John Magufuli, imeipunguzia kazi CCM
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Kwamba Watanzania wamekuwa wakivutiwa na utendaji kazi wa kiongozi huyo wa nchi ikiwamo kusimamia rasilimali za nchi.
Kauli
hiyo imetolewa jana wilayani Uvinza mkoani hapa na Kaimu Katibu Mkuu wa
UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alipokuwa akizungumza na wana-CCM kwenye
mkutano wa ndani uliofanyika katika kata za Kazuramimba na Nguruka.
Alisema
kwa sasa njia imekuwa nyeupe kuelekea mwaka 2020 kwani kazi kubwa
inayofanywa na Rais Magufuli ni kielelezo tosha kwa kiongozi huyo kuwa
anastahili kupewa nchi na kuongoza kwa awamu ya pili.
Shaka
aliwataka wanachama wa CCM kutobweteka na uhakika huo na badala yake
wajitume kwa bidii, kufanya kazi ya kisiasa kisayansi na kizalendo kama
njia ya kuwatumikia Watanzania wote.
“Utendaji
wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli katika kipindi kifupi, kwa hakika
umewakosha Watanzania pamoja na kuitikisa dunia na kwa sasa wanyonge
nao wanajiona wana thamani na hadhi katika nchi yao.
“Dk.
Magufuli ametupunguzia hekaheka na kazi nzito ya kusaka kura za ushindi
wa mwaka 2020, hata viongozi na wanachama wa CCM tusibweteke na
kujiamini, wajibu wetu ni kufanya kazi na kuwatumikia wananchi,” alisema.
Aidha Shaka alivichambua vyama vya upinzani na kusema vingine ni mabaki ya ukoloni mamboleo katika ardhi ya Tanzania.
Alisema
vyama hivyo vimekuwa vikiongozwa na wanasiasa uchwara waliojitahidi kwa
miaka mingi kuvipinga vyama vya TANU, ASP na Serikali baada ya Uhuru wa
Tanganyika mwaka 1961 na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Shaka
alisema kwa sasa upinzani uliokuwapo nchini hauna lolote zaidi ya
kupoteza muda kutokana na vyama hivyo kurithi sera na mipango ileile ya
wakoloni na Sultan kwa kuwagawa wananchi.
0 comments:
Post a Comment