Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati), hii leo akizungumza na wanahabari baada ya kikao baina yake na viongozi wa Tanesco pamoja na wawakilishi wa kampuni zilizohusika na utengenezaji na ufungaji wa mitambo katika kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta mazito cha Nyakato Jijini Mwanza.
Kushoto ni balozi wa Norway nchini Tanzania, Hanne-Marie Kaarstad na kulia ni balozi wa Denimark hapa nchini, Einar Jensen. Mabalozi hao wamehudhuria kikao hicho ikiwa ni sehemu ya kusaidia kutatua mvutano baina ya kampuni zinazotoka katika nchi zao na Tanesco kutokana na baadhi ya mitambo iliyofungwa na kampuni hizo katika kituo cha Tanesco Nyakato Jijini Mwanza kuharibika. Mradi huo uligharibu shilingi bilioni 129 hadi kukamilika kwake na una uwezo wa kuzalisha Megawati 60 za umeme.
#BMGHabari
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati), balozi wa Norway nchini Tanzania, Hanne-Marie Kaarstad (kushoto) pamoja na kulia ni balozi wa Denimark hapa nchini, Einar Jensen (kulia)
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, ameliagiza Shirika la Umeme nchini Tanesco kufanya matengenezo kwenye mitambo yake minne ya kuzalisha umeme iliyoharibika katika Kituo cha Nyakato Jijini Mwanza kabla ya kufikia Februari 28 mwakani.
Profesa Muhongo ametoa agizo hilo hii leo Jijini Mwanza, baada ya kukutana na viongozi wa Tanesco pamoja na wawakilishi wa kampuni zilizohusika na utengenezaji na ufungaji wa mitambo hiyo kutoka nchi za Norway na Denmark ambapo pia mabalozi wa nchi hizo wamehudhuria kikao hicho.
Aidha Profesa Muhongo ameiagiza Tanesco kuhakikisha mitambo sita iliyosalia haiharibiki tena na kwamba inamaliza kazi ya kusafisha mitambo yote katika kituo hicho kabla ya kufikia mwezi Februari 28 mwakani ambapo imeelezwa kwamba baadhi ya mapungufu katika mitambo hiyo yalitokana na kutosafishwa kwa wakati. Kampuni zote mbili zimekubali kushirikiana na Tanesco katika kutekeleza makubaliano hayo.
Awali kulikuwa na mvutano baina ya Tanesco na Kampuni ya Rolls Royce ya nchini Norway iliyotengeneza mitambo hiyo pamoja na kampuni ya Semco ya nchini Denmark iliyofunga mitambo hiyo, baada ya mitambo minne kati ya 10 kuharibika ndani ya kipindi cha miaka miwili na hivyo kusababisha uzalishaji wa megawati 18 kati ya 60 zilizopaswa kuzalishwa kupungua.
Hata hivyo pande zote zinazolalamikiana zimeonekana kuwa na hoja ambapo Profesa Muhongo ameitaka Tanesco kuandika malalamiko yake na kuyawasilisha kwa kampuni Rolls Royce iliyotengeneza mitambo hiyo kabla ya februari 28 mwakani, malalamiko ambayo yanapaswa kujibiwa hadi kufikia tarehe 30 mwezi Machi mwakani ili kujua maamuz yatayofuata.
Mabalozi wa pande zote mbili, ambao ni Hanne-Marie Kaarstad kutoka nchini Norway pamoja na Einar Jensen wa Denmark, wameeleza kuridhishwa na makubaliano ya kikao hicho wakiamini kwamba mwafaka huo utasaidia uzalishaji wa umeme kama ilivyokusudiwa ili kufikisha huduma ya umeme kwa wananchi.
0 comments:
Post a Comment