Friday, November 25, 2016

MKURUGENZI WA ILEJE AWADHIBITI WAKWEPA KODI

 Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya ileje Haji Mnasi akiwa kwenye eneo husika la kukagua wakwepa kodi.
 
Hawa ni baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wialaya ya Ileje wakifutalia jambo lililokuwa likiongelewa na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya ileje haji mnasi
Hili ni moja ya malori yaliyokuwa yakikwepa ushuru kwa kufanya biashara ya kushusha mizigo vichochoroni.
Hili ni moja kati ya gari linalobeba milunda bila kulipia ushuru na mkurugenzi Haji Mnasi kufanikiwa kulikamata wakati wa zoezi maalumu la kuwatafuta wakwepa kodi waliobobea kuikimbia serikali kulipa kodi

Na Daniel Mwambene, Songwe                           

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje wampongeza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Haji Mnasi kwa kukuza uchumi wa wilaya hiyo na kufanikiwa kuwadhibiti wafanyabiashara waliokuwa wakikwepa kodi.

Pongezi hizo zilitolewa na madiwani hivi karibuni wakati wa kikao cha Kamati ya Fedha,Uongozi na Mipango kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri.

Akizungumza na blog hii diwani wa kata ya Itumba Mohamed Mwala alisema kuwa wanatambua juhudi zilizofanywa na Mkurugenzi Haj Mnasi na wafanyakazi wa halmashauri kukusanya ushuru maeneo mbalimbali na kufanikiwa kuyakamata magari aina ya maroli yaliyokuwa yakikwepa ushuru.

Naye diwani wa kata ya Ibaba Tata Kibona alisema kuwa mkurugenzi na timu yake  wamekuwa wakitembea usiku kuwatafuta wakwepa kodi hasa kwenye kata yake ambapo mara kadhaa mkurugenzi huyo amekuwa akionekana nyakati za usiku.

"mimi sijawahi ona mkurugenzi kama huyu maana anaacha usingizi wake unamkuta kwenye kata nyakati za usiku akipambana nao wakwepa kodi na amefanikiwa kuwadhibiti wafanyabiashara wote wakwepa kodi na ndio maana sasa mapato yameanza kukua kwa kasi katika wilaya yetu"alisema Kibona 

Akielezea mafanikio hayo Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Godfrey Zimubiha alisema kuwa mafanikio hayo yanachangiwa na wadau mbalimbali ukiwemo uongozi ngazi ya wilaya,kata vijiji na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Halmahauri hiyo Haji Mnasi aliwapongeza wananchi,watumishi wa ngazi zote za wilaya na madiwani wote kwa kufanya kazi kwa weledi wao na kufanikisha malengo ya wilaya hiyo hata hivyo alimshukuru mkuu wa wilaya ya Ileje Joseph Mkude  kwa ushirikiano anaoutoa

 “Nashukuru mungu sasa madiwani wa wilaya yangu wameacha siasa na wanafanya kazi kwa kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuri kwa kile anachokifanya kuleta maendeleo ya nchi yetu na ndio maana unaona hata huku kwetu pato letu la wilaya limekuwa”alisema Mnasi

Aidha Mh Mnasi aliyataja baadhi ya maeneo yaliyokuwa korofi wakati wa ulipaji wa ushuru ni kama  kata ya Ngulilo ambako kulikuwa na utoroshaji wa mazao ya mbao pamoja na kata ya Mbebe na Isongole ambako nako kulikuwa na utoroshaji wa nafaka.

Mnasi aliwaonya wafanyabiashara wanaokwepa ushuru au kodi kwa kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu na elimu itaendelea kutolewa kuanzia ngazi ya kitongoji hadi wilaya ili kuwabaini wakwepaji wa ushuru ambao wanaathiri maendeleo ya wilaya hiyo.

“Nasema kuwa nitakula nao sahani moja wafanyabiashara wote wanakwepa ushuru hadi pale watakapo acha tabia hiyo na kusaidia uchumi wa halmashauri ya wilaya ya Ileje kukua kwa kasi inayostahili”alisema Mnasi

Wilaya ya Ileje hutegemewa sana kwa uzalishaji wa mbao ambazo husafirishwa kwenda katika mkoa wa Songwe na Mbeya.



0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More