“DAKTARI tunakufa” yalikuwa ni maneno pekee yaliyotolewa ndani ya dakika 15 na Consolata Mwakikuti baada ya kushuhudia pacha mwenzake Maria Mwakikuti akitangulia kukata roho katika tukio la kusikitisha lililotokea mjini Iringa juzi.
Pacha hao walioungana ambao habari zao zilikuwa gumzo katika vyombo mbalimbali vya habari toka udogo wao hadi sasa, walifariki majira ya saa 2.30 na saa 3.00 usiku wa Jumamosi wakiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa waliokokuwa wakiendelea na matibabu.
Akizungumza na wanahabari jana mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Museleta Nyakirito alisema pacha hao walikuwa na tatizo kwenye njia ya hewa hatua iliyosababisha wafikwe na mauti.
Dk Nyakirito alisema Maria alikuwa wa kwanza kufa na wakati akikata roho, pacha mwenzake Consolata alitoa maneno hayo (Daktari tunakufa) kwa uchungu na baadaye akaa kimya na ndani ya Dakika 10 na 15 baada ya mwenzake kufa naye akafa.
“Juhudi za kunusuru maisha ya pacha hao zilikuwa zikiendelea katika hospitali hii tangu walipofikishwa hapa Mei 17, mwaka huu wakitokea hospitali ya Taifa ya Muhimbili walikokuwa wakipata matibabu,” alisema.
Alisema Januari, mwaka huu mapacha hao walilazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa wakisumbuliwa na magonjwa ya akina mama (hakuyataja) na ndipo walipopewa rufaa ya kwenda Muhimbili walikokuwa wakitibiwa kwa zaidi ya miezi miwili kabla ya kurejea Iringa.
Alisema walirudishwa Iringa na kufikishwa katika hospitali hiyo majira ya saa 1.30 usiku wakiwa wamesindikizwa na daktari mmoja, muuguzi mmoja, mtaalamu wa wagonjwa mahututi (ICU) pamoja na teknishani wa mambo ya gesi (Oksijeni).
“Kwa taratibu zetu, baada ya kufariki walipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ambako miili yao imehifadhiwa hadi sasa wakati taratibu zingine za wanafamilia zikiendelea,” alisema.
Taratibu za mazishi
Akizungumza na wanahabari baadae Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela alisema mazishi yanatarajiwa kufanyika Jumanne au Jumatano katika makaburi ya Kanisa Katoliki, katika kijiji cha Tosamaganga nje kidogo ya manispaa ya Iringa.
“Tunamsubiri Sista Mkuu wa Maria Consolata , Sista Jane ambaye yupo safarini akitokea Dar es Salaam kuja Iringa na atakapofika le oleo tutapanga taratibu za mwisho za mazishi yao” alisema.
Kasesela alisema kabla ya mazishi yao, mapacha hao wataagwa katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) walikokuwa wakisoma shahada ya ualimu.
Aliomba kama kuna ndugu wa mapacha hao popote pale nchini wajitokeze kushiriki mazishi hayo ili kuwapa faraja katika safari yao ya mwisho.
“Hatuna taarifa za ndugu wowote toka tumewafahamu mapacha hao, tunachojua wamekuwa wakilelewa kanisa Katoliki kwa msaada wa wadau mbalimbali kwa maisha yao yote,” alisema.
Wakati huo huo, Kasesela amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli kwa rambirambi yake ya Sh Milioni 5 aliyotoa kuomboleza kifo cha mapacha hao.
Nao wanafunzi wa chuo cha RUCu waliokuwa wakisoma na pacha hao wamesema wameupokea msiba huo kwa masikitiko makubwa.
“Baada ya kupokea taarifa hizi, chuo kilikuwa kama kimemwagiwa maji. Hakuna aliyeamini taarifa hizo japokuwa ukweli ndio huo. Mungu azilaze roho zao peponi,” alisema mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la Rose.
Maria na Consolata walizaliwa wilayani Makete mkoani Njombe mwaka 1996.
Walisoma shule ya Msingi Ikonda Makete na kuhitimu na kufaulu mtihani wa darasa la saba mwaka 2010, kisha wakajiunga na shule ya Maria Consolata iliyopo Kilolo mkoani Iringa ambapo walihitimu kidato cha nne mwaka 2014.
Baada ya hapo walijiunga na shule ya Sekondari ya Udzungwa wilani Kilolo walipohitimu kidato cha sita mapema mwaka 2017 na wote kufaulu kwa kupata daraja la pili na hatimaye Septemba 2017 wakajiunga na Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (Rucu) walipokuwa wakisomea fani ya ualimu mpaka mauti inawafika.