Sunday, August 30, 2015

CHADEMA YAZINDUA KAMPENI JIMBO LA KALENGA




Na Mathias Canal, Iringa 

vijijini Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kupitia Umoja wa katiba ya Wananchi {UKAWA} kimezindua kampeni zake katika Jimbo la Kalenga lililopo mkoani Iringa kwa muktadha wa kuanza vyema mikikimikiki ya kumnadi mgombea wake ambaye mara kadhaa amesikika akisema jimbo hilo limekosa muwakilishi wa wananchi bungeni. 



Chadema/ukawa inataraji kuanza kampeni zake za kumnadi mgombea wa Urais, wagombea ubunge, na udiwani mara baada ya uzinduzi wa kampeni zinazotaraji kufanyika mwishoni mwa wiki hii. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo zilizofanyika katika eneo la Ifunda, mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema/Ukawa, Mdede Mussa Leonard amesema kuwa ameamua kugombea jimbo hilo kwa kuwa ni mkazi wa Kalenga hivyo hakusoma kwenye kitabu changamoto za jimbo na wala hana haja ya kusimuliwa. 

Amesema kuwa lengo mahususi la kugombea jimbo hilo ni kuhakikisha anaibana serikali na kushirikiana na wanakalenga wa ndani na nje ya jimbo na wadau mbalimbali wamaendeleo kuhakikisha Jimbo hilo linakwamuliwa kutoka kwenye mkwamo wa maendeleo na huduma duni za kijamii. 

Ameeleza kusikitishwa sana na ukosekanaji wa maji jimboni hapo, ukosefu wa barabara nzuri ambazo zitawasaidia wananchi kusafirisha mazao yao, gharama kubwa za elimu ambapo ameeleza kuwa serikali imefuta ada kwa shule za serikali lakini imesahau kufuta michango ambayo ndiyo imekuwa mikubwa zaidi. 

Mdede ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Kipera, Kata ya Nzihi, ana umri wa miaka 27, shahada ya udaktari ya chuo kikuu cha Afya ya tiba Bugando amewahi kuwa Rais wa chuo hicho kwa kipindi cha mwaka mmoja sawia na kuwa Rais wa vyuo vikuu vyote Tanzania bara na visiwani TAHLISO. 

Mdede amekuwa kiongozi wa ngazi mbalimbali za chama ikiwa ni pamoja na mwaka 2012-2013 alikuwa muasisi na mwenyekiti wa Chadema chuo kikuu cha Bugando, 2013 alipokuwa mwenyekiti wa chadema kwa vyuo vyote vya mkoa wa Mwanza.

Aidha Mdede ameshiriki mafunzo ya uongozi kwa marais wa vyuo vikuu vya Afrika Mashariki yaliyofanyika Arusha mwaka 2013 sambamba na kuhudhuria ziara ya mafunzo kiuongozi nchini China.

 Wakati wa uzinduzi wa kampeni jimboni humo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chadema ngazi ya Jimbo, Wilaya na mkoa, Mdede alisema kuwa jimbo hilo lina jumla ya Kilomita 4038.1, Wakazi 15079,Tarafa 3,Kata 15,Vitongoji 434, na Vijiji 75, hivyo anaamini endapo watampa ridhaa atafika kila mahali na kuhakikisha changamoto za wakazi wa jimbo hilo zinatatuliwa kwa kiasi kikubwa. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa BAVICHA mkoa wa Iringa, Leonce marto amesema kuwa serikali ya chama cha mapinduzi ambayo inamaliza muda wake imeshindwa kuwawezesha wananchi kupata hata pembejeo za kilimo, pamoja na nchi ya Tanzania kuwa na rasilimali nyingi ikiwa ni pamoja na madini, gesi, maziwa, bahari na vivutio mbalimbali ikiwa ni pamoja na mbuga za wananyama. 

Alisema Tanzania imekosa mafanikio na kuendelea kubaki nyuma kimaendeleo kwa sababu ya udhalimu na ubovu wa uongozi wa CCM ambao asilimia kubwa wanatuhumiwa katika kesi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ufisadi. 

Sawia na kufanyika kwa uzinduzi huo ambao unataraji kufanyika kwa ngazi ya Tarafa ambapo hiyo itakuwa awamu ya kwanza lakini utaendelea kwa awamu ya pili ngazi za vijiji mara baada ya kufanyika uzinduzi wa kampeni za chama hicho kitaifa.

Sunday, August 2, 2015

DOSARI YAJITOKEZA KURA ZA MAONI UBUNGE JIMBO LA IRINGA MJINI, MGOMBEA ATAKA MCHAKATO USITISHWE


frank Kibiki ambaye pia ni Mwanahabari wa Magazeti ya Uhuru na Mzalendo wa mkoani
frank Kibiki akionyesha walivyo kosea jina lake.


na mwandishi wetu,iringa


WAKATI kura za maoni za kutafuta wagombea ubunge katika majimbo yote nchini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) zikipigwa leo, mmoja kati ya wagombea 13 wanaotafuta nafasi hiyo Jimbo la Iringa Mjini, Frank Kibiki anataka zoezi hilo jimboni humo libatilishwe.

Wagombea wengine ni pamoja na Dk Augustino Maiga, Dk Yahaya Msigwa, Frederick Mwakalebela, Nuru Hepautwa, Michael Mlowe, Aidan Kiponda, Addo Mwasongwe, Jesca Msambatavangu, Mahamudu Mgimwa, Peter Mwanilwa na Fales Kibasa.

Akizungumza na wanahabari hii leo, Kibiki ambaye pia ni Mwanahabari wa Magazeti ya Uhuru na Mzalendo wa mkoani hapa alisema kura hizo zinapoteza uhalali kwasababu jina lake limekosewa.

“Mimi naitwa Frank John Kibiki, lakini kwenye karatasi ya kupigia kura ameandikwa mgombea mpya aliyetajwa kwa jina la Frank John Kibiri,” alisema.

Alisema kwa kuwa Frank Kibiki na Frank Kibiri ni watu wawili tofauti, hawezi kukubali kutumia jina la Kibiri ili kuhalalisha mchakato huo na endapo atafanya hivyo wagombea wenzake wanaweza kukata rufani kupinga matokeo hayo.

Kibiki alisema ameandika barua ya malalamiko yake kwa uongozi wa CCM wa Manispaa ya Iringa huku kopi ya malalamiko hayo yanayotaka uchaguzi huo ufanyike upya baada ya karatasi ya kupigia kura kusahihishwa akiipeleka kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara.

Akikiri kupokea barua ya mlalamikaji huyo na dosari iliyojitokeza kwenye karatasi hizo za kupigia kura, Katibu wa CCM Manispaa ya Iringa, Elisha Mwampashi alisema; “suala hili tulikubaliana na mgomea huyo tulimalize kwa kusahihisha kwa peni jina hilo. Baada ya kuifanya kazi hiyo kabla ya zoezi lenyewe la upigaji kura kuanza, zoezi limeendelea kama kawaida.”

Taarifa ya Mwampashi imepingwa na Kibiki mwenyewe aliyesema katika vituo 81 kati ya 90 vya upigaji kura alivyotembelea ni kituo kimoja tu cha Umati alichokuta jina lake limerekebishwa katika karatasi hizo.

Huku akiahidi kuishtaki kampuni iliyopewa kazi ya kuchapisha karatasi hizo kwa kukosea jina lake, Kibiki alisema; “katika hili sitanyamaza, nitakuwa sauti ya yoyote aliyewahi kuonewa ndani ya chama  vinginevyo nitalazimika kusubiri miaka mitano ijayo ili nishriki kwenye mchakato mwingine wa haki.” Alisema.

Wakati huo huo Katibu wa CCM wa Manispaa hiyo amezungumzia idadi ya wana CCM waliojitokeza katika mchakato huo wa kura za maoni kuwa ni ndogo ikilinganishwa na matarajio yao ya kushirikisha wanachama zaidi ya 18,000.

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More