Monday, February 23, 2026

KAMPENI YA MAFUNZO KWA WAJASIRIMALI WADOGO YAZINDULIWA KUELEKEA MAADHIMISHO YA WIKI YA USALAMA NA AFYA KAZINI 2026

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, akiwasilisha hotuba yake ya kufunga mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wanachama wa kikundi cha Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU).Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, akiwasilisha hotuba yake ya kufunga mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wanachama wa kikundi cha Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU).Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi.Khadija Mwenda, akitoa maelezo ya awali kuhusu mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na Taasisi yake kwa wanachama wa kikundi cha Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU) katika haflaya kufunga mafunzo hayo.Wanachama wa kikundi cha Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU), wakifuatilia nasaha na hotuba za viongozi mbalimbali katika hafla ya kufunga mafunzo ya usalamana afya mahali pa kazi yaliyotolewa kwao na OSHA ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi yaWaziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu alikuwa Mgeni Rasmi.

Na Fredy Mgunda,Geita

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu,amezindua kampeni ya mafunzo kwa wajasiriamali wadogo ambayo ni sehemu ya programu za uhamasishaji masuala ya usalama na afya kazini kuelekea maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Aprili 28, 2026.

 

Kampeni hiyo imeanza kwa kutoa mafunzo kwa wanachama wa umoja wa Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU) wanaofanya shughuli za uchimbaji madini katika Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita ambayo yametolewa mwishoni mwa wiki (Februari 21, 2026).

 

Akifunga mafunzo hayo ya siku moja kwa wanawake zaidi ya 350, Waziri Sangu, mbali na kuwapongeza wakazi wa Bukombe kwa kuwa wachapakazi, amesisitiza juu ya umuhimu wa kuzingatia masuala ya usalama na afya katika shughuli za uchimbaji madini hususan kwa wachimbaji wadogo ambao mazingira yao ya kazi yana vihatarishi vingi na teknolojia yao ni duni.

 

“Tunafanya mafunzo haya kwa kutambua umuhimu wake kwa wachimbaji wadogo. Tumekuwa tukipata taarifa za matukio mengi ya ajali hususan kwa wachimbaji wadogo kufukiwa na vifusi wakiwa wanatekeleza majukumu yao. Hii ni kutokana na kuwa uchimbaji wenu mara nyingi hautumii teknolojia za kisasa ambazo ni ghali na upatikanaji wake ni mgumu,” amesema Waziri mwenye Dhamana ya Masuala ya Kazi na kuongeza:

 

“Nimefurahi sana kuonana na kundi la wachimbaji wanawake zaidi ya 350 kwani mara nyingi tumezoea kuona shughuli hizi zinafanywa na wanaume tu. Hivyo, ninawapongeza sana nasisi tutaendelea kuunga mkono jitahida zenu kwa kuwawezesha kufanya kazi kwa tija na katika hali ya usalama.”

 

Amemuagiza Mtendaji Mkuu Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda, kuhakikisha mpango huo wa mafunzo unakuwa endelevu na kuyafikia makundi mengi zaidi ya wachimbaji wadogo na wajasiriamali katika sekta nyingine za kiuchumi.

 

Aidha, Waziri Sangu, ametoa rai kwa wachimbaji wadogo kuzingatia masuala mbalimbali waliyofundishwa katika mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na matumizi endelevu ya vifaa kinga ambavyo baadhi vimetolewa na OSHA kupitia programu hiyo.

 

Akizungumza nje ya ukumbi wa mafunzo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi.Khadija Mwenda, amesema lengo la programu ya mafunzo kwa makundi mbalimbali ya wajasiriamali wadogo ni kuwatambua na kuwajengea uelewa wa masuala ya usalama na afya ili kuongeza kiwango cha uzingatiaji (compliance level) wa kanuni bora za usalama na afya nchini.

 

Aidha, ameahidi kuhakikisha kwamba mpango huo wa mafunzo unakuwa endelevu kwa mujibu wa maelekezo ya serikali yaliyotolewa na Waziri mwenye Dhamana ya Masuala ya Kazi nchini.

 

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Mwenyekiti wa WAWABU, Bi. Regina Kabogo, wameishukuru serikali kwa uwezeshaji waliopata wa mafunzo na vifaa kinga huku wakiiomba serikali kuwafanyia upembuzi yakinifu wa hali ya upatikanaji wa dhahabu katika vitalu 13 vinavyomilikiwa na umoja huo.

 

“OSHA wametufundisha vitu vingi sana kuhusiana na usalama na afya katika shughuli zetu za uchimbaji madini na wametupatia baadhi ya vifaa kinga vya muhimu jambo ambalo litatuhamasisha kufanya kazi kwa bidii ili kujiongezea kipato binafsi pamoja na mapato ya serikali,” ameeleza Bi. Regina Kabogo.

 

Mafunzo yalitolewa na OSHA kwa wanachama wa WAWABU yamehusisha mada mbalimbali zikiwemo dhana ya usalama na afya mahali pa kazi, vihatarishi vya usalama na afya katika sekta ya madini, sheria ya usalama na afya mahali pa kazi pamoja na misingi ya huduma ya kwanza mahali pa kazi kwa nadharia na vitendo.

MIGODI MIKUBWA NCHINI IMETAKIWA KUWEZESHA WACHIMBAJI WADOGO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, akiwasilisha hotuba yake mbele ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Mkoa wa Geita, Menejimenti ya Mgodi wa Geita na watendaji wa Ofisi yake katika ziara ya kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi na Sheria nyingine za kazi katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, akiwasilisha hotuba yake mbele ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Mkoa wa Geita, Menejimenti ya Mgodi wa Geita na watendaji wa Ofisi yake katika ziara ya kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi na Sheria nyingine za kazi katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML).
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Geita, Menejimenti ya Mgodi wa Geita na watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu katika ziara ya kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi na Sheria nyingine za kazi katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML), Bw. Ashraf Suryaningrat, mara baada ya kuhitimisha ziara ya kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi na Sheria nyingine za kazi katika Mgodi huo.


Na Fredy Mgunda,Geita

Wito umetolewa kwa makampuni makubwa ya uchimbaji madini nchini kuwekeza katikakuwawezesha wachimbaji wadogo katika nyanja mbalimbali ikiwemo teknolojia za kisasa na usimikaji wa mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi ili kujenga uchumijumuishi unaotokana na sekta ya madini.

Wito huo umetolewa na serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, alipofanya ziara ya kufuatilia utekelezaji wa Sheria yaUsalama na Afya Mahali pa Kazi na Sheria nyingine za kazi katika Mgodi wa Dhahabuwa Geita (GGML).

Waziri Sangu ameipongeza menejimenti ya Mgodi huo kwa kuzalisha ajira nyingi kwaWatanzania ambapo GGML imeajiri jumla ya wafanyakazi 2,366 moja kwa moja na4,629 wameajiriwa kupitia wakandarasi mbalimbali wanatoa huduma katika Mgodi waGGML.

Sambamba na pongezi hizo, Waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi ameutakaMgodi huo kuhakikisha kwamba shughuli zake zinakuwa na athari chanya katikauchumi wa jamii zinazowazunguka kwa kutoa fursa za kazi za muda mfupi ikiwemokuwezesha miradi mbalimbali ya kijamii.

Aidha, Waziri Sangu ameipongeza GGML kwa kuchagua suala la usalama na afya kwawafanyakazi kuwa tunu yao ya kwanza katika shughuli zao za uchimbaji na uchakatajiwa madini jambo ambalo limewafanya kujenga mifumo madhubuti ya kulinda afya nausalama wa wafanyakazi inayozingatia matumizi ya teknolojia za kisasa.

“Ninawapongeza kwa kuweka usalama na afya kama tunu yenu ya kwanza na hiiimejidhirisha katika wasilisho lenu mlilofanya hapa ambapo masuala ya usalama naafya yamechukua nafasi ya juu zaidi ya biashara mnayofanya,” ameeleza Waziri Sangu na kuongeza:

“Pongezi hizi inastahili pia Taasisi ya OSHA ambayo imekuwa ikiwaongoza katikakutekeleza hayo kupitia usimamizi mzuri wa Sheria Na.5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 na miongozo mbalimbali chini ya sheria hiyo ambayowamekuwa wakiitoa kupitia kaguzi zao za mara kwa mara.”

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Geita,Hashim Abdallah Komba, amesema OSHA ni miongoni mwa Taasisi zenye msaadamkubwa katika kuwezesha shughuli mbalimbali za kiuchumi kufanyika kwa tija katikaMkoa wa Geita.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema ziara hiyo, inalenga kuona jinsi OSHA inavyoshirikiana na wadau wake kutekeleza Sheria yaUsalama na Afya mahali pa kazi ambayo dhima yake kuu ni kulinda nguvukazi ya Taifa dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi pamoja na kulinda uwekezaji kupitiakuzuia uharibifu wa mali.

Awali, menejimenti ya GGML iliwasilisha taarifa juu ya shughuli zao iliyoainisha jinsiafya na usalama wa wafanyakazi unavyozingatiwa katika shughuli husika. Miongonimwa masuala yaliyoelezwa katika taarifa hiyo ni pamoja na historia ya mgodi ambapoimeelezwa kuwa madini katika mgodi huo yaligunduliwa mnamo mwaka 1898 nauchimbaji rasmi kuanza mwaka 1999.

Wednesday, February 11, 2026

OSHA YAJA NA MPANGO WA KUWEZESHA BIASHARA NA UWEKEZAJI NCHINI

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akizungumza na washiriki wa kikao kazi baina ya OSHA na Maafisa Biashara wa Mikoa na Wilaya za Kanda ya Kaskazini
Meneja wa Usalama Mahali pa Kazi wa OSHA, Mhandisi Robert Mashinji, akiwasilisha mada kuhusu usajili wa maeneo ya kazi na utekelezaji wa majukumu ya OSHA kwa ujumla katika kikao kazi baina ya OSHA na Maafisa Biashara wa Mikoa na Wilaya za Kanda ya Kaskazini.
Meneja wa Kitengo cha Sheria OSHA, Bi. Pendo Berege, akiwasilisha mada kuhusu Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 katika kikao kazi baina ya OSHA na Maafisa Biashara wa Mikoa na Wilaya za Kanda ya Kaskazini.
Washiriki wa kikao kazi baina ya OSHA na Maafisa Biashara wa Mikoa na Wilaya za Kanda ya Kaskazini wakifuatilia mawasilisho toka kwa wataalam wa OSHA kuhusu Sheria na Usalama na Afya Mahali pa Kazi pamoja na utekelezaji wa majukumu ya OSHA kwa ujumla.


Na Fredy Mgunda.

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umezindua mpango wake wa kushirikiana na Maafisa Biashara wa Mikoa na Wilaya katika kuwezesha biashara na uwekezaji nchini.

Mpango huo unahusisha utaratibu wa kuunganisha mifumo na kubadilishana taarifa za biashara na miradi mbalimbali ya uwekezaji ili kurahisisha ufikishaji wa huduma za urasimishaji biashara na ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi.

Mpango huo wa OSHA umewekwa wazi na Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Khadija Mwenda, alipohitimisha semina ya kujenga uelewa wa pamoja baina ya OSHA na Maafisa Biashara wa Mikoa na Wilaya zote za Kanda ya Kaskazini ambao umefanyika kwa siku moja katika Ofisi za OSHA zilizopo Jengo la PAPU Jijini Arusha.

Bi.Mwenda amesema mpango huo umeibuliwa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa akielekeza Taasisi za serikali kushirikiana katika utendaji ikiwemo kuhakikisha kwamba mifumo mbalimbali ya serikali inasomana.

Aidha, ameeleza kuwa mpango huo unalenga kutekeleza agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, alilolitoa Desemba 22, 2025 ambapo aliwataka waajiri/wamiliki wa maeneo ya kazi kote nchini kuhakikisha maeneo yao ya kazi yanasajiliwa OSHA ndani ya siku 90 kuanzia mwezi Januari 2026 ili kurahisisha usimamizi wa masuala ya usalama na afya katika maeneo husika.

“Lengo kuu la mpango huu ni kuhakikisha kuwa Taasisi ya OSHA inafanya kazi kwa kushirikiana na wenzetu ambao ni Maafisa Biashara wa Mikoa na Wilaya wote tukiwa kama Taasisi wezeshi katika biashara na uwekezaji,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA na kuongeza:

“Tumekuwa na kikao kizuri sana ambacho kimetufungulia zoezi letu ambalo tumepanga kulifanya nchi nzima. Mpango huu utakapokamilika sote tutakuwa na uelewa wa pamoja ambao utapelekea taasisi zetu kuwa wawezeshaji zaidi badala ya kuwa wadhibiti wa shughuli za biashara na uwekezaji nchini.”

Kwa upande wao washiriki wa semina hiyo ambao ni Maafisa Biashara wa Mikoa na Wilaya zote za Kanda ya Kaskazini ikihusisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga, wamepongeza mpango huo na kuahidi kushirikiana na OSHA kufanikisha mpango huo.

“Tumefurahia sana mafunzo ya leo,hakika tumetoka na ufahamu mpana kuhusiana na kazi za OSHA na tumeona kuna umuhimu mkubwa sana kwa wafanyabiashara na wawekezaji kujisajili katika mfumo rasmi ili waweze kuweka salama sehemu zao za kazi,” ameeleza Bw. Elisha Erasto, Mkuu wa Idara ya Biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo.

“Tunaishukuru sana OSHA kwa semina ya leo na kwaniaba ya washiriki wenzangu ninapenda kusema kwamba tutashirikiana na OSHA ili kufanikisha mpango huu unaolenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini na hivyo kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa 2050,” amesema Bi. Lulu Kaaya, Afisa Biashara Mkoa wa Arusha.

OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) yenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 inayoweka utaratibu wa kitaifa wa usimamizi wa masuala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi.

 

Monday, January 12, 2026

WANAFUNZI VYUO VIKUU WAMETAKIWA KUJIEPUSHA NA NDOA ZA REJAREJA, DKT MSOWOYA

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, Dkt Tumaini Msowoya akiongea na wanafunzi wa chuo kikuu cha Iringa wakati wa kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa masomo katika chuo hicho.
Baadhi ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Iringa wakimaliza Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, Dkt Tumaini Msowoya wakati akitoa hotuba yake 
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, Dkt Tumaini Msowoya akikabidhi kiasi cha shilingi milioni mbili kwa uongozi wa chuo kikuu cha Iringa zilizotolewa na Dikson Mwipopo, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, kwa ajili ya kuwaunga mkono wanafunzi hao. 


Na Fredy Mgunda, Iringa.


Wanafunzi wa vyuo vikuu wametakiwa kujiepusha na ndoa za rejareja,makundi ya hovyo yenye viashiria vya kuharibu masomo na maisha kwa wanafunzi wenye ndoto ya kuja kulitumikia taifa la Tanzania na nje ya Tanzania.

Akizungumza wakati kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza chuo kikuu cha Iringa,Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, Dkt Tumaini Msowoya alisema kuwa wanafunzi wanapaswa kuepukana na ndoa za rejareja, makundi ya hovyo na kuwa wazalendo kwa ajili ya maisha yao.


Dkt Msowoya amesema baadhi ya wanafunzi hujikuta wakitumbukia kwenye ndoa za rejareja na kusahau lengo la masomo kutokana na tamaa za kifedha na kuishi maisha mazuri chuo jambo ambalo limekuwa likipoteza dira ya masomo kwa wanafunzi wengi.


"Najua mna miaka zaidi ya 18 hivyo sio watoto Kwa mujibu wa kawaida lakini je, ndoa ndiyo imekuleta chuoni? Wazazi wako wanajua umeoa au kuolewa huku?" amesema na kuongeza, Dkt Msowoya

"Niliwahi kufanya utafiti kuhusu maisha ya wanafunzi wa vyuo vikuu nikagundua wengi wanaishi na wenza ilhali familia zao hazijui. Hii ni hatari,"

Dkt. Msowoya aliwahimiza wanafunzi kuipenda nchi yao, kusoma kwa bidii na kuepuka makundi yenye viashiria hasi katika masomo na maisha kwa ujumla.

Katika hafla hiyo, alitoa mchango wa shilingi milioni mbili (2,000,000) zilizotolewa na Dikson Mwipopo, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, kwa ajili ya kuwaunga mkono wanafunzi hao. 


Sunday, January 11, 2026

USHIRIKI WA WANANCHI WAIMARISHA UPANDAJI MITI SAO HILL

 
Wananchi wanaozunguka Shamba la Miti Sao Hill wameendelea kunufaika kielimu na kiuchumi kupitia ushiriki wao katika shughuli za uchukuaji miche ya miti zinazofanyika katika bustani za miche zilizopo Tarafa ya Kwanza Irundi na Tarafa ya Tatu Ihalimba.
Wananchi wanaozunguka Shamba la Miti Sao Hill wameendelea kunufaika kielimu na kiuchumi kupitia ushiriki wao katika shughuli za uchukuaji miche ya miti zinazofanyika katika bustani za miche zilizopo Tarafa ya Kwanza Irundi na Tarafa ya Tatu Ihalimba.
Wananchi wanaozunguka Shamba la Miti Sao Hill wameendelea kunufaika kielimu na kiuchumi kupitia ushiriki wao katika shughuli za uchukuaji miche ya miti zinazofanyika katika bustani za miche zilizopo Tarafa ya Kwanza Irundi na Tarafa ya Tatu Ihalimba.



Na Fredy Mgunda, Mufindi.

Wananchi wanaozunguka Shamba la Miti Sao Hill wameendelea kunufaika kielimu na kiuchumi kupitia ushiriki wao katika shughuli za uchukuaji miche ya miti zinazofanyika katika bustani za miche zilizopo Tarafa ya Kwanza Irundi na Tarafa ya Tatu Ihalimba.

Shughuli hizo ni sehemu ya mpango endelevu wa upandaji miti unaotekelezwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa lengo la kuendeleza misitu ya kupandwa, kuongeza uzalishaji wa rasilimali za misitu na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Said Singano, alisema uchukuaji wa miche unafanyika kwa kuzingatia taratibu na kanuni za kitaalamu ili kulinda ubora wa miche.

“Tunasisitiza miche ichukuliwe kwa uangalifu mkubwa ili isiharibu mizizi, kwa sababu ubora wa miche ndiyo msingi wa mafanikio ya upandaji miti mashambani,” alisema Singano.

Shughuli hizo pia zimeongeza uelewa wa wananchi kuhusu mchango wa Shamba la Miti Sao Hill katika uhifadhi wa mazingira, mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji endelevu wa mazao ya misitu kwa manufaa ya Taifa.

Mmoja wa wananchi walioshiriki zoezi hilo, Bw. Joshua Ng'umbi kutoka Kijiji cha Igowole Wilaya ya Mufindi, alisema ushiriki wake umemsaidia kuongeza kipato na kupata ujuzi mpya katika shughuli za misitu.

“Mbali na kupata ajira, nimejifunza kuchagua miche bora na namna sahihi ya kupanda miti ili iweze kuota vizuri na kukua kwa ubora unaoweza kuleta kipato kizuri wakati wa uvunaji,” alisema Bw. Joshua.

Kwa ujumla, zoezi la uchukuaji miche katika Tarafa za Irundi na Ihalimba limeendelea kuleta manufaa makubwa kwa Shamba la Miti Sao Hill na wananchi kwa kuimarisha juhudi za upandaji miti, kutoa ajira na kukuza uelewa wa masuala ya misitu na uhifadhi wa mazingira.

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More